Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Rambirambi au Unafiki?
http://www.habaritanzania.com/articles/1836/1/Rambirambi-au-Unafiki?
By Mzee Mwanakijiji
Published on 11/16/2006
 
Kitendo cha viongozi wa ngazi za juu wa serikali yetu kwenda kutoa rambirambi kwa familia ya Hassan Mbonde huko Kawe, kwa njia kinaonekana ni cha kibinadamu, kiungwana, na kinachoonesha kujali. Hata hivyo kwa mtu anayeangalia kwa karibu kitendo hiki kimejaa unafiki, uzandiki, na kinachozua maswali mengi zaidi.

Je ilikuwa ni ajali?
"Ajali haina kinga" waswahili walisema, kale kadaladala kugonga gari la RC yawezekana kuwa ajali (ingeweza kuwa gari la mtu yeyote kwani hiyo ni mashine tu), lakini kitendo cha mtu kuamua kutoka ndani ya gari lake, kujibizana na dereva, kumfuata hadi kwenye gari lake, kuweka kidole kwenye trigger, kulenga mahali pa kichwa na kufyatua huwezi kuita ajali, unless neno "ajali" limepoteza maana yake!!

Je aliua kwa kukusudia?
Jibu langu ni ndiyo. Hakuna mtu anayenyosha bastola iliyo na risasi, na kuweka kidole kwenye trigger huku ameielekeza kwa mtu/watu na baadaye kufyatua, mtu/watu wakafa halafu huyo mtu aseme hakukusudia kuua!! Kama lengo lake ilikuwa ni kumtishia huyo kijana, angefanya kama wanavyofanya mapolisi au hata watu wengine kabla ya kuamua kumlenga mtu kujitetea. Wanafyatua risasi hewani kutishia!!! Unapozidiwa nguvu hapo ndipo unapoua ukitetea maisha yako, and that is a defence.

Je ni mauaji ya kujitetea maisha?
Hilo lingekuwa na ukweli endapo tu, yule kijana angetajwa mahali popote kuwa alibeba silaha (ya aina yoyote) na kumtishia Bw. Mkuu wa Mkoa. Hadi hivi sasa hakuna ushahidi wowote kuwa Hassan alifanya hivyo. Kinachojulikana alipigwa risasi (iwe moja, mbili, au kumi) akiwa ameketi kwenye kiti cha gari huku amefunga vioo!

Je Bunduki inahitajika kuonesha nia ya kosa (mens rea)
La hasha, mazingira peke yake yanatosha kuonesha kama mtu alikusudia kutenda tendo ovu (actus reus) au la. Mtu akikutwa juu ya paa la nyumba ya mtu mwingine huku akiwa ameshikilia gudulia la petroli akimimina, na baadaye kushika kiberiti na kuwasha nyumba hiyo na baadaye akakutwa amesimama pembeni anaangalia huku nyumba inaungua, mkononi amebakia na njiti zilizoungua, na ana harufu ya mafuta na mashahidi wapo waliomuona akifanya hivyo, na ikathibitika kuwa ndani ya nyumba kulikuwa na mtoto wa miaka 4 aliyeuawa kwa moto, polisi hawahitaji guduria la mafuta lililotumika kumwaga mafuta!!!

Je kitendo cha viongozi kwenda kutoa rambirambi ni kuokoa vurugu?
Kwa nje kitendo hicho kinapongezwa, ni cha kibinadamu na ni cha kiungwana. Hata hivyo, ukichunguza kwa karibu utaona kuwa ndani ya kitendo hicho kumejaa unafiki, uzandiki, na wa hali ya juu. Lengo lake ni moja tu nalo kumuonesha mtuhumiwa kuwa anajutia tendo lake (kitu ambacho hakibadilishi uzito au ubaya wa tendo hilo) na kujaribu kwa namna fulani kumuombea msamaha kwa wafiwa. Kitendo cha viongozi kutoa ahadi za kuisaidia familia n.k kina lengo moja tu nalo ni kuwanyamazisha wanafamilia (siyo kuzuia vurugu). Je watu waliokuwa wanalia mwanzoni kuwa famiilia imempoteza mtu pekee ambaye ndiye alikuwa anawasaidia kwa kila inahitaji nini zaidi ya mtu kuwapa uhakika wa chakula na malazi ya hapo baadaye?

Je ni watu wangapi ambao wanafiwa na baba zao, jamaa zao wanaosadia familia zao lakini huo RAis, makamu, meya, mawaziri, n.k wakijipanga msururu kuahidi misaada?

Ukweli ni kuwa, viongozi hawa wote wanafanya wanayofanya si kwa sababu wana uchungu kuwa Mbonde ameuwa kinyama, siyo kwa sababu familia inahitaji msaada sana, siyo kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuwasaidia tena.. La hasha!! Viongozi hawa wanafanya wanachofanya kwa sababu anayetuhumiwa kuua ni NANI.

UKWELI NI HUU
Kama muuaji wa Hassan angekuwa Mmachinga fulani, jambazi fulani n.k unadhani viongozi hawa wangepanga foleni kwenda huko Kawe? Je alipouwa yule mwandishi wa habari wa The East African, viongozi wangapi wangazi za juu walienda kutoa pole kule na kuahidi kuisadia familia yake? Sitashangaa kuna viongozi walioenda kutoa pole, sitashangaa kuna mawaziri walioenda kutoa rambirambi kule, ila WANGAPI KATI YA HAO WALIKWENDA WAKIFUATANA NA WAANDISHI WA HABARI NA WAPIGA PICHA?

Kama hamuyaoni mazingaombwe, basi inabidi mkalie ndimu!!!

M. M. Mwanakijiji