Na Hakimu Mwafongo, Iringa
WATU tisa wanaodaiwa kuwa ni majambazi, wakiwamo askari wawili wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga wamekamatwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuwavamia wafanyabishara watatu na kupora Sh25 milioni.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Mohamed Mbwana, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku katika eneo la Ndiuka, Kata ya Ruaha mjini hapa.Alisema majambazi hao walikuwa na silaha mbalimbali ikiwamo bastola ambayo imekamatwa, kisu, nondo na bunduki inayotumia risasi za shortgun.
Akielezea tukio hilo, Kamanda Mbwana alisema watu hao waliwavamia wafanyabiashara wa vifaa vya elektroniki kama televisheni na redio katika maeneo ya katikati ya mji, Sisty Materu (45), Fideleis Ngandu (32) na Basley Materu (36) ambao walikuwa wakirudi nyumbani kwao katika eneo la Ndiuka.Alisema wafanyabiashara hao walikuwa wanajiandaa kwenda Dar es Salaam jana asubuhi kununua mali kwa ajili ya maduka yao yaliyopo Miyomboni.
Alisema walipofika jirani na kwao, ghafla walivamiwa na watu hao na Sisty aliyekuwa akiendesha gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Chaser T771 ACS alipigwa risasi katika kiganja cha mkono na kusimamisha gari.Mbwana alisema waliposimama majambazi waliwavamia na huku askari wa JKT wakiwa wamevalia sare zao, waliwapiga kwa nondo na wakataja kuwa kuwa wamehifadhi fedha hizo kwenye buti ya gari.
Majambazi hao walichukua fedha hizo zilizokuwa zimefungwa kwenye mfuko wa plastiki na kutokomea nazo.Aliongeza kuwa wasamaria wema walijitokeza na kuwapeleka polisi na hospitali ya Mkoa wa Iringa ambako wamelazwa katika wodi namba nne na hali zao zinaendelea vizuri.Kamanda Mbwana alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa msamaria kuwa majambazi hao wanafanya mapatano na dereva teksi ili waende Mafinga, ndipo polisi walipofika katika eneo hilo na kuwakamata baadhi yao.
Alisema polisi waliwakamata watu wanane na wengine ambao idadi yao haikujulikana walikimbia wakiwa na bunduki iliyokuwa ikitumika.Alisema pia walifanikiwa kukamata bastola, kisu, fedha zote sh25 milioni na gari aina ya Toyota Mark II ikiwa na na namba za usajili T328 AKB ambayo inadaiwa kuwa ilisaidia kutorosha majambazi waliotoroka na bunduki.