Na Muhibu Said
ZIARA ya Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Shein kuhani msiba wa dereva, Hassan Mbonde, anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni Ditopile Mzuzuri, umeibua upya kilio kutoka kwa mjane wa marehemu, ndugu, jamaa na marafiki waliokuwapo nyumbani hapo jana.
Mjane, Joha Mohamed, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, walishikwa na majonzi na kuangua kilio kwa kupaza sauti, pale Dk Shein alipokwenda kumfariji mjane huyo.
Hali hiyo iliyodumu kwa dakika kadhaa, ilitulizwa na Dk Shein baada ya kuingia katika chumba hicho na kumpa pole mjane huyo wa marehemu.
Dk Shein ambaye katika ziara hiyo alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, alimtaka mjane huyo kuwa na subira katika kipindi kigumu kinachowakabili na kumuahidi kuwa serikali iko bega kwa bega na wafiwa.
Baada ya kutoa kauli hiyo, Dk Shein, aliwataka ndugu hao wa marehemu kusoma papo hapo moja ya sura iliyoko ndani ya Kur'ani Tukufu inayowasifu watu wanaosubiri, maarufu kama "Suratul Asr".
Awali, kaka mkubwa wa marehemu, Kesy Abdul, alimweleza Dk Shein kuwa, familia ya marehemu inawashukuru viongozi wote wa serikali kwa kushitushwa na msiba uliowafika na jinsi wanavyoshirikiana nao bega kwa bega.
"Tunashukuru viongozi kwa kushitushwa na msiba na kuja kutufariji," alisema Kesy.
Baadaye, Kesy aliwaambia waandishi wa habari kuwa mbali na kwenda kuwafariji, Dk Shein, amewaahidi pia kuipelekea ubani wa msiba familia ya marehemu kupitia kwa wasaidizi wake.
Dk Shein ameingia katika mlolongo wa viongozi sita wa kitaifa na Mkoa wa Dar es Salaam waliokwenda kuhani msiba huo, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo aliyetoa Sh500,000 kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Wengine ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, ambaye ametoa viroba 10 vya mchele na mafuta ya kula kwa kwa ajili ya kufanikisha kisomo cha hitma ya kumuombea marehemu iliyoandaliwa na kiongozi huyo Jumamosi wiki hii. Hitma nyingine ya marehemu itafanyika Desemba 10, mwaka huu.
Vile vile Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Abuu Jumaa nao wamekwishafika kuhani msiba huo.
Kiongozi aliyefika kwenye msiba huo wakati wa mazishi na kutoa ubani wake wa Sh100,000 alikuwa ni Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema.
Kapteni Ditopile yuko rumande akikabiliwa na tuhuma za mauaji ya dereva huyo, ambaye alipigwa risasi na kufariki dunia eneo la njia panda ya Kawe na Bagamoyo, jijini Dar es Salaam Novemba 4, mwaka huu.
Wakati huo huo, polisi wanadaiwa kupekua nyumbani kwa mmiliki wa daladala ambalo dereva wake, Hassan Mbonde, anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na Ditopile kutafuta bastola iliyotumika katika mauaji hayo.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam na kuthibitishwa na mmiliki wa daladala hilo, Thomas Mwita, zinaeleza kuwa askari hao ambao idadi yao haijafahamika, walipekua nyumba hiyo iliyoko eneo la Kawe Mzimuni, wakidai kuitafuta bastola hiyo inayodaiwa kupotea katika eneo la tukio.
Hata hivyo, Mwita mwenyewe hakupenda kuingia kwa undani wa suala hilo lakini mmoja wa majirani zake alidai kusikitishwa na kitendo hicho akisema kuwa kilijenga hofu kwa watu wanaoishi katika eneo hilo.
"Tulijua hili suala litatuletea matatizo hasa kwa upande wa watu wanaoelekea kutoa ushahidi kwenye tukio hili kwani polisi kuja na silaha pale ni kutaka kutisha tu," alieleza jirani mmoja.
Mwita ambaye ni mmiliki wa daladala hilo aina ya Toyota Journey, linalofanya safari kati ya Ubungo na Tegeta, siku ya tukio, alikuwa kondakta wa gari hilo na alipambana na Ditopile katika eneo la tukio.
Kitendo hicho kinadaiwa kuchukuliwa na askari hao siku chache baada ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, kukaririwa na vyombo vya habari akitangaza kutokuonekana kwa kwa bastola hiyo.
Kamishna Tibaigana, alirejea kauli hiyo Ijumaa wiki iliyopita ofisini kwake alipotakiwa na waandishi wa habari kueleza iwapo bastola hiyo imekwisha kupatikana au la na kueleza kuwa bastola hiyo iliyotumika katika mauaji ya dereva huyo ilipotea katika eneo la tukio.
Kamishna Tibaigana, alisema hadi sasa walichofanikiwa kukipata, ni magazini ya bastola hiyo na maganda risasi ya zilizofyatuliwa katika tukio hilo.
Bastola hiyo ni kielelezo kimojawapo cha msingi kinachotegemewa kutumiwa na polisi kama ushahidi katika kesi ya mauaji inayomkabili Ditopile.
Alipoulizwa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jamal Rwambow, alisema hana taarifa za askari hao kufanya upekuzi nyumbani kwa Mwita.
"Sina taarifa, hivyo unavyoniambia ndio ninasikia," alisema Kamanda Rwambow