Na Salma Salma, Zanzibar
NGURUWE na mazao yake wamepigwa marufuku kuingizwa Zanzibar katika kile kilichoelezwa kuwa ni tishio la ugonjwa wa mafua ya ndege.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Mafua ya Ndege, Dk Ali Rabia, alisema nguruwe, kama walivyo jamii ya ndege pamoja na kuku, wapo katika orodha ya mifugo ambayo inatajwa kuwa inaweza kusambaza virusi vya mafua ya ndege.
“Kutokana na kuwepo kwa hatari ya kuenea kwa mafua ya ndege, tumepiga marufuku uingizaji wa nguruwe pamoja na nyama yake kutoka sehemu zote nje ya visiwa hivi,” alisema afisa huyo katika semina ya siku moja na waandishi wa habari juu ya hatari ya ugonjwa wa mafua ya ndege.
Rabia alisema nguruwe anaweza kuathirika na virusi vya mafua ya ndege kama vitakuwa vimeshambulia jamii ya kuku na kumpata yeye kirahisi kwa kuchanganyika na mafua yake.
Hatua ya serikali imekuja baada ya Zanzibar kuwa moja ya sehemu ambazo matumizi ya nyama ya nguruwe ni makubwa, hasa kutokana na kasi ya kuongezeka kwa hoteli za kitalii.
Ufugaji wa nguruwe Zanzibar umekuwa unaongezeka siku za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali kutokana na nyama hiyo kuuzwa kwa wingi katika hoteli za kitalii.
Mbali na nguruwe, tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepiga marufuku uingizaji wa aina yote ya jamii ya ndege, ikiwemo kuku na mayai kama moja ya hatua za kukabiliana na maradhi hayo.
Hivi karibuni, SMZ kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maliasili, iliteketeza kwa moto mayai zaidi ya 60,000 ya wafanyabishara wa visiwani hapa, yenye thamani ya zaidi ya Sh6 millioni ambayo huingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara.
Rabia alisema Serikali ya SMZ tayari imeunda timu ya pamoja ya kupambana na maradhi hayo ambayo ipo chini ya Afisi ya Waziri Kiongozi na moja ya mikakati yake ni kutoa taarifa kwa jamii kuhusu maradhi hayo.
“Tunalazimika kutoa elimu kuhusu hatari ya ugonjwa wa mafua ya ndege kutokana na hatari zake kwa jamii pamoja na uchumi kwa ujumla,” alisema Dk Rabia.
Wakati huo huo, Dk Rabia alifafanua kuwa kuku 300 waliokufa katika eneo Kizimbani mwaka huu, hawakufa kwa mafua ya ndege, bali ni kutokana na ukiukaji wa taratibu za ufugaji.
Maradhi ya ugonjwa wa mafua ya ndege yameathiri na kushambulia zaidi nchi za bara la Asia ambako mamia ya watu wamepoteza maisha yao huku mifugo mingi iliyoambukizwa ugonjw ahuo ikiteketezwa.