Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com
Mtanzania mwenzangu,
Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikiandika sana masuala ya kujisomea,kupenda kuhoji masuala mbalimbali yanayotuzunguka,kujipenda sisi wenyewe kama watu,kunyanyuana wenyewe kiuchumi,kudumisha umoja, kujenga moyo wa kizalendo kwa nchi yetu,kupiga vita rushwa kwa kuanzia na sisi wenyewe nk
Masuala yote niliyoyataja hapo juu yana umuhimu wa pekee katika maendeleo ya jamii zetu.Lakini kama ulivyo ujenzi wa nyumba,ili nyumba iwe imara na isije anguka pindi upepo unapozidi ni sharti iwe na msingi imara. Katika haya yote msingi wa elimu unaweza kuchukua nafasi kubwa sana.
Kimsingi elimu ndio taa na pia ndio kiza,inategemea tu unaiona vipi,umefundishwa nini,na nani,kwa jinsi gani na mambo kama hayo. Lakini cha muhimu kabisa ni kwamba elimu ni lazima iende sambamba na mazingira yanayomzunguka mtu.
Nchi yetu inasemekana kwamba ni nchi huru. Ndio maana kila ifikapo 9 December huwa tunashuhudia gwaride la heshima likifuatiwa na hotuba kadha wa kadha.Usisahau pia jinsi ambavyo hadithi za kupigania uhuru zinavyokuwa zinapamba moto nyakati kama hizo. Ukweli utabakia siku zote kwamba mapambano ya kumg’oa mkoloni lilikuwa ni jambo muhimu sana. Uhuru ni jambo ambalo yeyote alionao hana budi kuulinda kwa hali na mali.
Ubinadamu bila uhuru ni kama usiku wa kiza. Tatizo letu kubwa limekuwa matumizi ya uhuru wetu.Tumeutumiaje? Tumeutumiaje katika masuala ya elimu kwa mfano?Tumebadilisha kwa namna gani mfumo wetu wa elimu kutoka kwenye ule aliotuachia mkoloni?
Kama unaungana na mimi kutambua kwamba hakuna mabadiliko yoyote basi naomba pia uungane na mimi kukiri kwamba pana tatizo kubwa ambalo kizazi hiki cha sasa hakina budi kulifanyia kazi ama sivyo baada ya miaka mingine 40 ya uhuru hadithi itakuwa ni hii hii ya leo.
Nimewahi kushuhudia mijadala mikali sana ya waafrika huku ughaibuni wengine wakidai ni bora mkoloni arejee,wengine wakisema mkoloni hakuwahi kuondoka na wengine wakisema wazi kwamba kamwe mkoloni asirejee. Kila mmoja katika makundi hayo hapo juu anajua kwanini anatoa hoja anazotoa.Aisifiaye mvua imemnyea! Huu bado ni mjadala mkali sana.
Pengine siku moja nitauandikia ili na mimi nitoe hoja zangu kamili.Lakini kwa wakati huu napenda kujiuliza,je wanaosema mkoloni hakuondoka kamwe wana maana gani? Je,wanazungumzia jinsi ambavyo kwa mfano mfumo mzima wa elimu ni ule unaothamini mazingira ya kikoloni kuliko yetu? Si ni ukweli kwamba historia tunayowafunza wenetu hatujaiandika sisi wenyewe bali mkoloni,alivyotaka yeye?
Si ni kweli kwamba sisi hatuna mashujaa wa hisabati wala fizikia,kemia nk na ndio maana majina ya wagunduzi hao wanabakia kuwa kina Isaack Newton na wenzake? Na je si ni ukweli kwamba elimu yetu hamsaidii mtanzania kuelimika bali kujua kusoma na kuandika pekee? Utabisha kwamba wanafunzi wa tanzania wengi wanasomea mitihani tu na wala sio kuelimika? Je tuwalaumu wanafunzi au viongozi na washika dau wengine wa elimu?
Kwa bahati mbaya sana nadhani hatuwezi kuwatupia lawama wanafunzi kwani wao sio watunga mitaala. Kama mitaala ya elimu haiendani na mazingira ya mwanafunzi basi ni wazi mapenzi na moyo wa kutaka kujifunza zaidi unakuwa haupo.
Kwanini nitake kujua zaidi kuhusu Mississipi Valley Authority kama sina hata mfano wa kitu hicho nchini kwangu? Ipo mifano mingi sana ya elimu bila kuelimika na elimu ambayo haimuandai mwanafunzi kuweza kuyatumia mazingira yanayomzunguka kwa faida yake.
Ni wahitimu wangapi wa kitivo cha uhandisi kwa mfano kutoka pale mlimani ambao wameweza kuitumia elimu waliyoipata chuoni kujitafutia ajira binafsi? Wataanzia wapi kama vitabu vyote walivyokuwa wakivitumia chuoni ni kutoka magharibi ambapo mazingira ni tofauti kabisa na tuliyonayo hapo?
Nimewahi kusema umuhimu wa kuangalia misaada tunayopokea. Kama tunapokea vitabu kutoka Marekani au Canada au popote pale duniani ni lazima tujiulize,je vitabu hivi vinaendana na mazingira yetu? Vinatufunza kuelimika?
Tutawezaje kufanya mapinduzi ya kiuchumi kama wanafunzi wa leo hawafundishwi masuala muhimu kama ya uwekezaji,ununuzi wa hisa na kadhalika tangia wakiwa wadogo? Dunia gani tunawaandalia hawa katika haya mapambano ya utandawazi ambao hatuna tena jinsi ya kuupinga?
Mwisho naomba tuketi chini na kujiuliza kikamilifu,hivi ni mifumo mingapi ya kikoloni ambayo tumeibadilisha tangu aamue kuondoka kimwili na kubakia kimawazo kupitia utumwa wa kiakili na ukoloni mamboleo? Tusiangalie elimu kama elimu tu bali kama mfumo mzima,mfumo muhimu. Hapo ndipo inabidi kuziangalia kimakini sera zetu za elimu.
Tunaposema elimu bure kwa wote tunazungumzia elimu ya kiukombozi au elimu ambayo mwisho wake ni kutengeneza kizazi kinachozidi kuthamini cha wenzetu kuliko chetu? Au tunatengeneza kizazi cha manamba wa wageni wanaokuja kwa kasi na gea ya uwekezaji?
jeffmsangi@sympatico.ca
www.harakati.blogspot.com