Na Burhani Yakub,Mkinga
MVUA za vuli zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha madhara wilaya ya Muheza mkoani Tanga, baada ya mafuriko kukumba Kijiji cha Msimbazi kata ya Mtimbwani wilayani hapa na kuua mtu mmoja na wakazi wengine 120 kukosa mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kuzolewa na maji.
Habari zilizopatikana kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa watu hao bado wamezingirwa na maji na kwamba hawana chakula, dawa na uwezo wa kuwasiliana na maeneo mengine.
Kufuatia maafa hayo Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mohamed Abdulaziz jana aliitisha mkutano wa dharura wa wafanyabiashara wa Jiji la Tanga na kuwaomba kutoa msaada wa kijamii kwa wahanga wa maafa hayo ya Kijiji cha Msimbazi.
Hivi karibuni wakazi 152 wa Kata ya Bwembwera wilayani Muheza nao walikumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Abdulaziz alisema kutokana na kuzingirwa na maji wahanga hao wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na dawa ofisi yake tayari imepeleka kilo 2,600 za unga wa sembe, kilo 500 za maharage na mahema kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga.
"Nimekuiteni kwa mambo makuu mawili kwanza kukujulisheni kuwa wenzetu wapo katika maafa na pili wanahitaji msaada wa chakula,dawa na hifadhi hivyo tusaidiane kuwastiri,"alisema Abdulaziz.
Baada ya maelezo hayo wafanyabiashara hao waliamua kuunda kamati ndogo ya kukusanya misaada kwa pamoja ili kuikabidhi serikalini.
Kabla ya kuundwa kamati hiyo mmiliki wa kampuni ya Usafirishaji ya Raha Leo, Selemani Abdallah alimkabidhi mkuu wa mkoa wa Tanga tani sita za unga na maharage kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao.
Juzi mwandishi wa habari hizi ambaye aliongozana na mkuu wa mkoa kwenda katika kijiji hicho kwa kutumia helkopta alishuhudia watu wakiwa hawana chakula na dawa kutokana na eneo hilo kuzingira na maji.
Watu hao waliozingirwa na maji kwa muda wa wiki moja sasa wameishukuru serikali kwa jitihada ilizochukua kuwapelekea huduma muhimu.
Wakizungumza katika eneo hilo watu hao walisema kutokana na hali ya eneo hilo kutopitika walishakata tama ya kuokolewa lakini walishangaa kuona helkopta ya jeshi la polisi ikiwa na mkuu wa mkoa wakiletewa chakula.
"Kwa kweli kuokoka kwetu kulikuwa ni ndoto kwani maji yametuzunguka hatuna pa kukimbilia hatukutegemea kupata msaada wowote kwa kuwa eneo hili halifikiki kutokana na maji," alisema mmoja wa wahanga hao.
Walisema kuzingirwa kwao na maji hayo kumetokana na mafuriko ya mito miwili ya Msimbazi na Pangalawe na kusababisha njia zote kutopitika na kuwafanya wakose huduma muhimu kama chakula na matibabu.
Katika mafuriko hayo mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Bahatisha Ali amekufa maji huku moja ya majengo yaliyosombwa na majini ni makanisa mawili na msikiti mmoja.
Kwa kipindi cha wiki moja sasa mvua zimekuwa zikinyesha katika maeneo mbalimbali mkoani hapa huku taarifa za mafuriko zikiendelea kuripoitwa hali inayowatia wasiwasi wananchi waishio kwenye maeneo yaliyo karibu na mito na mabondeni