Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete atwishwa msalaba
Kikwete atwishwa msalaba
By Habari Tanzania | Published  11/12/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Kulwa Karedia

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtwisha msalaba mzito Rais Jakaya Kikwete, kwa kudai Uchaguzi Mkuu sasa urudiwe Zanzibar.

Chama hicho kimemtwisha msalaba huo Kikwete, kikisema kwamba ndiye mwokozi pekee anayeweza kusaidia katika hatua iliyofikia ya mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Akihutubia mamia ya wananchi katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam jana baada ya maandamano makubwa, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kuitishwa Uchaguzi Mkuu ndiyo njia pekee itakayosaidia kumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo Zanzibar.

“Sisi tunasema njia pekee ya kumaliza tatizo hili la mpasuko wa kisiasa Zanzibar ni kuitisha Uchaguzi Mkuu wakati wowote kuanzia sasa, ili tumalize tatizo hili, kwa vile Zanzibar ni yetu sote, lazima tushirikiane ili kuepuka machafuko,” alisema Maalim Seif.

Alisema hatima ya uchaguzi huo ipo mikononi mwa Rais Kikwete, aliyemtaja kuwa na dhamana yote ya kutoa baraka za kurudiwa uchaguzi huo, lakini akataka uchaguzi huo usimamiwe na waangalizi kutoka Umoja wa Mataifa (UN).

“Mwokozi wa suala hili ni Rais Jakaya Kikwete peke yake, afanye hima kuzikumbusha mamlaka husika ili uchaguzi ufanyike haraka. Lakini kubwa zaidi uchaguzi huu usimamiwe na waangalizi kutoka Umoja wa Mataifa, kwani wao ndio wanaweza kutoa haki badala ya wale tuliowazoea katika chaguzi zilizopita,” alisema Maalim Seif.

Katibu Mkuu huyo, alisema kauli za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, zimeonyesha dhahiri kutaka kurudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Rais Kikwete katika kuupatia ufumbuzi mpasuko wa kisiasa visiwani humo.

Alisema chama chake na Rais Kikwete hawajawahi kudai serikali ya mseto, hivyo wanashangaa Rais Karume kusema hakuna cha serikali ya mseto.

“CUF na Rais Kikwete hawajawahi kukutana hata siku moja ndugu zangu kudai serikali ya mseto, bali hizi ni propaganda za Rais Karume kutaka kutuvurugia mwenendo wetu wa kufikia kilele cha mafanikio katika siasa,” alisema Maalim Seif.

Alisema anaamini wazi, Rais Karume alitoa kauli hiyo kwa kudhamiria na kwa matakwa yake, wala hakutumwa na Rais Kikwete, kwa vile Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele kuwaunganisha Watanzania kuondokana na wasiwasi uliotanda Zanzibar.

Maalim aliyekuwa akishangiliwa mara kwa mara, alisema kwamba kutokana na hali hiyo, siku zote amekuwa mstari wa mbele kudai haki na usawa wa wananchi wote, asikubali kupotoshwa na watu wachache kwa manufaa yao.

Maalim Seif alisema yupo tayari kwenda jela, kufungwa na hata kufa kwa ajili ya kutetea haki za Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, kwa vile wao ndio waliompatia dhamana hiyo.

“Natamka wazi leo nipo tayari kufungwa, kufa na kuzikwa hapa hapa na wala sitakimbia nchi yangu kwa kuhofu usalama wangu, nilishawahi kufungwa siku za nyuma, nasema jukumu hili mlinipatia ninyi ili kutetea haki zenu, sisi ni jasiri, hatutaki kuona damu inamwagika,” alisema Maalim.

Alisema siku zote chama chake kimekuwa na matatizo makubwa, yakiwamo ya kudhulumiwa na kuibiwa kura nyingi katika chaguzi zilizofanyika, na kwamba sasa yupo tayari kukutana ana kwa ana na Rais Karume, ili wazungumzie matatizo ya Zanzibar na hatimaye wafikie muafaka, ambao utaunganisha visiwa vya Unguja na Pemba kuwa kitu kimoja, badala ya hali ya sasa.

“Nipo tayari kukutana na Rais Karume ili tuzungumzie matatizo yaliyopo visiwani Zanzibar, na kamwe mimi na Watanzania wenzangu hatukubali kuona nchi inaingia kwenye machafuko ya umwagaji damu kwa faida ya watu wachache, sasa imefika hatua ya kumaliza chuki,” alisema Maalim Seif.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustine Mrema, akihutubia katika mkutano huo, alisema kuna wana CCM wameanza kumgeuka Rais Kikwete, akiwamo Rais Karume na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, aliowaita wanamtandao.

Mrema alimtaka Rais Kikwete amchukulie hatua kali za kinidhamu Rais Karume kwa kutaka kuvuruga umoja wa kitaifa uliopo tangu uhuru.

Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Polisya Mwaiseje, alimtaka Rais Kikwete aitishe haraka Baraza la Taifa la Majadiliano ili waweze kujua chanzo cha matatizo ya Zanzibar na anayehusika ashughulikiwe kikamilifu.

Naye Profesa Abdallah Safari, alisema kuingia tena katika Uchaguzi Mkuu ujao ni sawa na kwenda machinjioni kuchinjwa, kutokana na wapinzani kuporwa haki zao za msingi. Alitaka wapinzani waitikise CCM kama Rais wa Venezuela, Hugho Chavez, anavyoitikisa dunia.

Maandamano hayo ya jana yalikuwa ya amani na utulivu mkubwa, yakianzia eneo la Manzese, huku wandamanaji wakiwa na mabango yakiwa na ujumbe mbalimbali.

Baadhi yalisema: “Kikwete, jukumu la amani ni letu sote…Karume acha kauli za uchochezi na “Seif, Karume ni hazina tuitumie.” Yalipita Barabara ya Morogoro, Kawawa hadi viwanja vya Karume, Ilala ambapo lengo kuu lilikuwa kulaani kauli ya Rais Karume kuwa serikali yake haitaunda serikali ya mseto.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.