Mwandishi wetu
GHARAMA za umeme nchini haziwezi kushuka endapo umeme unaopatikana utaendelea kutokana na jenereta za kutumia gesi na mafuta.
Akitoa mada ya hali ya umeme nchini jijini Dar es Salaam jana, Kamishina Msaidizi wa Nishati Mbadala katika Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava, alisema uzalishaji wa umeme wa gesi ya Songosongo unagharimu dola za Marekani senti 4 kwa uniti moja, wakati umeme wa IPTL ni senti 14.
Alisema njia nyingine ambayo gharama zake ni kubwa katika kuzalishia umeme ni jenereta zinazotumia mafuta, ambazo zinazalisha umeme kwa gharama ya dola za Marekani senti 35.
Umeme unaopatikana kwa gharama nafuu ni ule unaozalishwa kutoka katika vyanzo vya maji unaogharimu dola za Marekani senti 2.5.
Alisema hivi sasa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linawatoza wateja wake wastani wa dola za Marekani senti 6.7 (Sh86) kwa uniti moja, wakati uzalishaji ni wastani wa dola za Marekani senti 10.2 hivyo, kuifanya ipate hasara ya dola za Marekani senti 3.5 kwa kila uniti inayouzwa.
Mapema akifungua semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, alisema wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo Kimataifa (UNDP) wanaweka mikakati ili ipatikane nishati mbadala vijijini.
Alisema katika kutekeleza hilo saula hilo, wameanzisha mradi wa majaribio wa kuzalisha umeme huo katika vijiji viwili mkoani Kigoma ambao uzasaidia wakulima kuendesha mitambo ya kusindika mazao.
Naye afisa wa UNDP anayeshughulikia nishati vijijini, Bariki Kaale alisema Tanzania haipaswi kupata tatizo la ukosefu wa umeme wakati ina vyanzo vingi vya nishati hiyo.
Alisema ili kumaliza tatizo hili watanzania wanapaswa kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia njia mbadala kama vile umeme unapatikana kwa kutumia mafuta ya miti ya jatropha na upepo katika maeneo ya vijijini.