Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Ushindani waitisha TPDC
http://www.habaritanzania.com/articles/1791/1/Ushindani-waitisha-TPDC
By Ramadhan Semtawa
Published on 11/11/2006
 
USHINDANI wa kibiashara katika soko la mafuta umelitisha Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) na sasa limedai linafanya mambo yake chini kwa chini kwa kuogopa washindani.

Na Ramadhan Semtawa

USHINDANI wa kibiashara katika soko la mafuta umelitisha Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) na sasa limedai linafanya mambo yake chini kwa chini kwa kuogopa washindani.

Hatua hiyo inatokana na TPDC kuwasilisha ripoti yake ya kibiashara Wizara ya Nishati na Madini, huku ikikataa kuitoa hadharani.

Taarifa kutoka ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na TDPC, zinasema katika ripoti hiyo, TPDC imetoa mwelekeo wa kibiashara kuanzia ununuzi, miundombinu na wadau itakaoshirikiana nao katika kuingiza mafuta.

"Tayari TPDC imekwisha kuwasilisha ripoti yake, ina mambo mengi, kikubwa inatoa mwelekeo wa kibiashara kuanzia ununuzi wa mafuta hadi kuyaingiza nchini," kilisema chanzo hicho kutoka wizarani.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Yona Killagane, alisema hadi sasa mipango yote ya utekelezaji wa agizo la serikali kuhusu uagizaji mafuta inakwenda vizuri.

Hata hivyo, Killagane alisema kutokana na ushindani mkubwa wa kibiashara, shirika lake haliwezi kuanika hadharani mipango yake ya kibiashara.

Killagane alisema TPDC itafanya biashara katika mfumo wa ushindani tofauti na miaka ya nyuma wakati dola ilipokuwa ikihodhi uchumi, hivyo ni lazima ichukue tahadhari kutoka kwa washindani wake.

"Hadi sasa utekelezaji agizo la serikali unakwenda vizuri, ripoti zetu za kibiashara hatuwezi kuziweka hadharani kwa sababu washindani wetu wanaweza kuzitumia na kutukwamisha katika baadhi ya mambo," alisisitiza Killagane.