Na Penzi Nyamungumi, Zanzibar
MAKAMU wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein, amekemea tabia ya baadhi ya watu visiwani Zanzibar, kuendeleza sera za udini kinyume na taratibu za nchi ambazo zinasisitiza uhuru wa kila mtu kuabudu dini anayotaka.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kwa-Mabata uliopo katika Manispaa ya Zanzibar, Makamu wa Rais alisema kwa mujibu wa Katiba, Tanzania haina dini bali wananchi wake wana dini zao na wanaruhusiwa kuabudu dini yoyote wanayoitaka mradi hawavunji sheria.
“Inaelekea hapa kuna uchochezi wa kidini. Kama mtu anataka kuchochea kupitia dini, Tanzania haitampa nafasi na aondoke mwenyewe arejee huko alikotoka,” alisisitiza.
Dk Shein alisema Serikali haiko tayari kuona vurugu za kidini wakati taratibu zipo wazi katika kuendesha masuala ya kidini nchini.
“Hatutaki vurugu za kidini, taratibu za kidini zipo wazi, tusianzishe zogo jingine, tuelewane,” alionya Dk. Shein kufuatia makaratasi yanayodaiwa kuchochea vurugu za kidini yaliyosambazwa na watu wasioeleweka.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais alisifu maendeleo yaliyofikiwa katika visiwa vya Unguja na Pemba na kwamba mafanikio yote hayo kwenye huduma za jamii na miundombinu ya barabara na mawasiliano yanatokana na uongozi bora wa Rais Amani Abeid Karume.
Alimpongeza Rais Karume kwa mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye nyanja mbali mbali katika kutekeleza Ilani ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana.
Aliwataka wananchi wasibabaishwe na maneno ya wapinzani na kwamba watulie, wasichokozane, badala yake washikamane na kushirikiana ili kujenga Taifa lao.
Katika ziara yake jana katika mkoa wa Mjini Magharibi, Makamu wa Rais alikagua kilimo cha umwagiliaji wa mpunga katika Bonde la Mtwango na chama cha kuweka na kukopa.
Vile vile alizindua ujenzi wa hospitali ya daraja la pili iliyoko Jimbo la Mpendae na Sh4 milioni kusaidia ujenzi huo na akatoa Sh2.5 milioni na kompyuta moja kwa tawi la CCM la Kinuni