Na Waandishi Wetu, Dar, Zanzibar
POLISI jijini Dar es Salaam na Zanzibar wameyaruhusu maandamano yaliyoandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF) yaliyopangwa kufanyika leo, lakini wameingiza masharti kadhaa na kukitaka chama hicho kiyafuate.
Maandamano hayo yaliitishwa na chama hicho kulaani kauli ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ya kukana kuwapo mpasuko wa kisiasa na kuundwa serikali ya mseto visiwani humo.
Mbali na kulaani kauli ya Karume, maandamano hayo yanayofanyika leo Dar es Salaam na kesho Zanzibar, yanalenga kuunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kukiri kuwapo na kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa visiwani humo.
Jijini Dar es Dar es Salaam, maandamano hayo yataanza leo saa 4.00 asubuhi katika eneo la Mazese na Zanzibar yataanza muda huo kesho asubuhi katika eneo la Komba Wapya.
Hata hivyo, polisi wa Zanzibar na Dar es Salaam, wamebadili njia zitakazotumiwa na waandamanaji badala ya zile zilizotangazwa awali na uongozi wa CUF.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa njia walizoarifiwa na CUF katika maandamano yao zimebadilishwa kwa sababu za kiusalama.
Alisema awali barua yake polisi, CUF iliarifu kuwa maandamano hayo yangeanzia Magomeni Mapipa na kupita katika barabara za Morogoro, Msimbazi, Uhuru na kuishia katika Uwanja wa Karume ambako viongozi wakuu wa chama hicho watahutubia mkutano wa hadhara.
Tibaigana alisema kwa vile maeneo mengi katika barabara za Msimbazi na Uhuru zina wafanyabiashara wengi, wana hofu watu waovu wanaweza kutumia mwanya wa maandamano kujichanganya na waandamanaji na kufanya vitendo vya uhalifu dhidi ya wafanyabiashara.
Hivyo, alisema baada ya kukutana na Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa CUF, Mbarallah Maharagande, walikubaliana maandamano hayo yaanzie Manzese na kupita katika barabara za Morogoro na Kawawa na kuishia katika uwanja huo.
Pia alisema kutokana na ufinyu wa eneo la nje ya Uwanja wa Karume, wana hofu waandamanaji wanaweza kuingilia barabara za Uhuru na Kawawa na hivyo, kusababisha msongamano wa magari.
Kutokana na hali hiyo, alisema wamekubaliana pia na kiongozi huyo wa CUF kwamba, wahakikishe barabara hizo zinapitika na kwamba, polisi nao watatoa ulinzi kuanzia mwanzo wa maandamano hayo hadi mwisho wake.
Kwa upande wa Zanzibar, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakari Khatib Shaaban, alisema polisi imekubali kufanyika kwa mkutano na maandamano baada ya uongozi wa polisi kukutana na uongozo wa Chama cha CUF, kuzungumzia masharti ya kufanyika kwa mandamano na mkutano huo.
Alisema wamekubaliana na CUF kuwa mkutano na maandamano hayo yafanyike katika hali ya amani na utulivu.
Masharti mengine ni mkutano huo kuelezea masuala ya Chama na sera zao, bila kuingiza mambo ambayo huenda yakasababisha vurugu na kuvunjika kwa hali ya amani.
Maandamano hayo yatafanyika kuanzia Komba Wapya kupitia Mwembeladu na kumalizikia uwanja wa Demokrasia Amani kwenye mkutano wa hadhara, badala ya kuanzia Darajani hadi Uwanja wa Lumumba walipokuwa wameomba CUF.
Pilikapilika zote hizo za CUF ni kutaka kujibu kwa vitendo kauli ya Karume kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar, ambayo tayari wamesema inaweza kuchochea vurugu.
Kauli hiyo, imetafsiriwa na CUF kuwa ni kinyume na kauli ya Rais Kikwete aliyotoa, wakati alipolihutubia Bunge Oktoba 30 mwaka jana na kuahidi kulishughulikia kikamilifu suala la mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar na kuhakikisha muafaka unapatikana.
Taarifa ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumatatu wiki hii, ilieleza kuwa mbali na Dar es Salaam na Unguja, maandamano hayo yatafanyika pia Novemba 18, mwaka huu kisiwani Pemba ambako ni ngome ya CUF.
Profesa Lipumba alisema maandamano hayo yana lengo la kupinga kauli alizoziita za uchochezi, zilizotolewa na Karume Novemba 2 na 4, alipokuwa akihutubia maadhimisho ya mwaka mmoja wa ushindi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema maandamano hayo yananuia pia kufikisha ujumbe kwa Karume kuwa kauli zake hazitawakatisha tamaa wafuasi wa CUF katika kutumia njia za amani kudai haki ya Wazanzibari kupewa nafasi ya kuchagua serikali wanayoitaka kupitia uchaguzi huru na wa haki.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, maandamano hayo yatawashirikisha Watanzania wote wapenda amani bila kujali itikadi za kisiasa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Kikwete na kukemea kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi, ambazo zinaweza kuliingiza Taifa katika vurugu na fujo.
Aliongeza kuwa chama chake bado kinaamini kuwa malengo ya Rais Jakaya Kikwete aliyoayatoa kwenye hotuba yake kwa taifa bungeni Desemba 30 mwaka jana, ni muongozo sahihi wa kuijenga Tanzania inayojali, kuheshimu na kufuata misingi ya demokrasia.
Alisema hotuba hiyo ya kwanza na ya kipekee kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ilikuwa na mwelekeo mzuri katika kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya kisiasa badala ya kuongeza chuki na mifarakano.
Hata hivyo, wakati CUF wanaafikiana na kauli za Rais Kikwete na kupinga za Karume na baadhi ya viongozi wa Zanzibar, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Ali Mohamed Shein ameibuka mwishoni mwa wiki iliyopita kisiwani Pemba na kupigilia msumari wa mwisho kuwa hakuna lolote linalotarajiwa visiwani humo bali kusubiri Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.