Na Ramadhan Semtawa
HADI sasa hujiita Rais wa Iraq akizingatia madaraka yake aliyoyapata baada ya kufanya mapinduzi mwaka 1979.
Anajiita Rais licha ya kwamba Iraq imekwishapata Rais mwingine ambaye ni Mkurd, Jalala Talaban.
Tangu mwaka 1998 alituhumiwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwamba alikuwa akitengeneza silaha za maangamizi na mara kwa mara aliwatimua waangalizi wa Shirika la Nguvu za Atomic la UN (IAEA).
Amehukumiwa kifo kwa tuhuma za mauji ya Wakurd 148 na wapinzani wake wengine katika makosa ambayo kama kila moja lingekuwa na kesi yake basi muda wa kuzisikiliza hadi kutoa maamuzi ungechukua hata miaka kumi.
Ni mmoja wa Marais wa mataifa ya Kiarabu ambaye alionyesha ubabe au ushujaa wa kusimama hadharani kutunishia msuli mataifa makubwa ya maagharibi yakiongozwa na Marekani.
Hakuogopa mataifa hayo na kauli zake nzito za kuionya Marekani na washirika mara kwa mara kabla hajapinduliwa katika uvamizi uliofanywa mwezi Machi mwaka 2003, ziliwahi kuchukuliwa kama zilizokuwa zikilingia nguvu za kijeshi ambazo jeshi lake ilikuwa nazo.
Aliyatunishia msuli mataifa makubwa ya magharibi tangu alipoingia nayo katika vita ya Ghuba ya mwaka 1990 baada ya kuivamia Kuwait.
Tangu hapo mataifa makubwa ya magharibi yakiongozwa na Marekani yalijenga picha ya uadui dhidi ya utawala wake na kuanza kuutuhumu kutengeneza silaha za maangamizi.
Huyo si mwingine ni Saddam Hussein (66) ambaye sasa anakabiliwa na adhabu ya kifo.
Wachambuzi wanamuangalia Saddam kama mtu ambaye licha ya kukamatwa na hadi sasa kukabiliwa na adhabu ya kifo, lakini alionyesha msimamo ambao ulikuwa ukilenga kulinda hadhi ya Waarabu.
Bila kujali kama jeshi lake kikiwamo kikosi maalum cha Jamhuri, Saddam mara kwa mara alikuwa akiionya Israel na Marekani kwamba zingepata kipigo iwapo zingethubutu kuivamia nchi yake.
Saddam hadi sasa bado ni ajenda muhimu nchini Marekani hasa katika kipindi hiki ambacho Wamarekani wamefanya uchaguzi wa Bunge la Congress.
Wachambuzi wanaamini kwamba, Saddam na silaha za maangamizi na suala zima la uvamizi wa Marekani nchini Iraq huenda ukawa kipimo kikubwa cha utawala wa Bush.
Tayari katika kampeni zilizomalizika siku mbili zilizopita kabla ya kura kupigwa juzi, Bush amekuwa akitetea hatua yake ya kumuangusha Saddam madarakani.
"Ilikuwa ni lazima tumuondoe Saddam, sasa hivi Iraq inaelekea kuzuri, ingawa bado kunahitajika jitihada zaidi za kujenga amani na usalama," amesema Bush katika mikutano mbalimbali ya siku za mwisho ya kampeni ainadi wagombea wa Republican.Hata hivyo, wachambuzi wanaangalia vita ya Iraq hasa ya kumng'oa Saddam na hali ya mambo ilivyo nchini Iraq kwa sasa, kama ambayo imemshushia hadhi Rais Bush kwa kiasi kikubwa.Rais Bush wakati akiingia vitani dhidi ya Iraq mwaka 2003 alisema Saddam alikuwa akimiliki silaha za maangamizi.Lakini hata alipomkamata Saddam katika mji wa Tikrit alikozaliwa Agosti 2003, hakuna silaha zozote za maangamizi ambazo zilizopatikana.Hatua hiyo na mauaji ya wanajeshi wa Marekani kila siku nchini Iraq, imekuwa ikiibua hasira miongoni mwa Wamarekani ambao wanataka majeshi yao yarudi nyumbani.
Saddam Hussein ni nani na ametokea wapi?
Alizaliwa Aprili 28, 1937, Ad Dawr, Tikrit katika maeneo ya mashambani, kaskazini mwa jiji la Baghdad.
Saddam, ambaye aliishi akitaka kujionyesha kama ni mbabe katika mataifa ya Kiarabu dhidi ya mataifa ya magharibi, alianza kujijengea himaya zaidi mwaka 1980.
Jina la Saddam linamaanisha mpiganaji ambaye yuko tayari kwa mapambano mara moja.
Saddam hakupata fursa ya kumuona baba yake kwani alifariki wakati kabla hajazaliwa.
Akiwa na umri wa miaka 10, Saddam alikimbia kutoka kwa baba yake wa kambo kisha kwenda kuishia kwa mjomba wake, Khairallah Tulfan, mjini Tikrit.
Saddam akiwa na umri wa miaka 12, alihamia jijini Baghdad akiwa rafiki mkubwa wa Rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser, ambaye alitaka kujenga dola imara ya mataifa ya Kiarabu.
Katika mwaka 1960, Saddam alioa mtoto wa shangazi yake , Sajida.
Alibahatika kupata watoto watatu ambao ni Uday na Qusay ambao waliuawa Julai 22 katika mji wa kaskazini mwa Iraq, Mosul.
Historia ya kisiasa inamuonyesha Saddam kwamba mwaka 1950, alijiunga na chama cha Baath Arab Socialist.
Saddam alihusika katika harakati za kumuua Rais Abdel Karim Qassim wa Iraq, mara mbili, mara ya kwanza, jaribio hilo halikufanikiwa na Saddam akakimbilia Misri.
Mpiganaji huyo alikaa Misri akiendesha mapambano akiwa uhamishoni hadi pale uongozi wa Rais huyo ulipoondolewa madarakani mwaka 1963.
Mwaka huo Baath ikachukua madaraka ya dola lakini muda mfupi chama hicho kikaondolewa madarakani na Saddam akakamatwa na kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Baada ya kutoka, Saddam hakuacha harakati zake, kwani mwaka 1968 alihusika katika jaribio jingine la mapinduzi.
Mnamo mwaka 1979, akiwa na miaka 42, Saddam alichukua madaraka ya dola akiwa Rais wa Iraq.
Kwa msaada wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu, Marekani na mengine ya Ulaya, Saddam aliingiza nchi yake katika vita na Iran.
Vita dhidi ya Iran ilisababisha athari kubwa za kiuchumi ambayo ni pamoja na hasara katika usafirishaji mafuta kutoka katika nchi zote ambapo hasara inayokadiriwa ni dola 100 bilioni.
Mara baada ya vita ya Iran, mwaka 1990 Saddam aliivamia Kuwait akianza kujenga uadui na mataifa ya magharibi ikiwamo Marekani ambayo ilimpika.
Kilichofuata ni kushutumiwa na UN kwamba anatengeza silaha za maangamizi, mwaka 2002, Rais Bush alimtuhumu Saddam kwa kuficha silaha za sumu na kuita nchi hiyo kama mhimili wa uovo pamoja na Korea kaskazini na Iran.
Katika kuvutana ndipo ilipofika Machi, 2003 vikosi vya Marekani na Uingereza vipatavyo 250,000 viliingia nchini Iraq kumng'oa Saddam.
Machi 19, ndege aina ya F-117 za Marekani zilipiga eneo ambalo Saddam aliaminika kufanya mkutano na maafisa wa ngazji za juu wa jeshi na wasaidizi.
Aprili 7 ndipo majeshi ya washirika yalipofanikiwa kuukamata mji wa Baghdad baada ya kudondosha mabomu kutoka ndege za kivita, lakini mara zote hakukamtwa kwani alitoroka.
Hatimaye Saddam alitiwa mikononi mwa majeshi ya washirika ilipofika Agosti mwaka 2003 huo ukawa ndio kupanda na kushuka kwa Saddam ambaye sasa anasubiri adhabu ya kifo iwapo rufaa yake itakataliwa.