Waandishi Wetu, Arusha na Tanga
MVUA zinazonyesha sehemu mbalimbali nchini, imeanza kusababisha madhara kwa kuharibu miundombinu na kuharibu mali za watu.
Mkoani Manyara, migodi zaidi ya 17 ya madini ya Tanzanite Mererani inayomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo la kitalu B, imesitisha uchimbaji kutokana na kujaa maji.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wamiliki wa migodi hiyo na viongozi wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Arusha (Arema) walisema migodi iliyojaa maji ni ile ambayo inapakana na kampuni ya wawekezaji ya Tanzanite One.
Katibu wa Arema, Isaya Latema, aliiomba serikali ifanye uchunguzi juu ya chanzo cha maji hayo, kwani wanahisi wanafanyiwa hujuma ili washindwe kuendelea na kazi hiyo.
Baadhi ya wamiliki wa migodi hiyo, ambao waliomba kutotajwa majina yao, walisema kuwa tatizo hilo hadi sasa limewasababishia hasara ya zaidi ya Sh50 milioni.
Hata hivyo, Kampuni ya Tanzanite One, imekanusha kuhusika kumwaga maji hayo katika migodi ya jirani.
Rais wa kampuni ya Tanzanite One na Mtendaji Mkuu, Ian Harebottle, alisema si kweli kuwa kampuni yake inamwaga maji katika machimbo hayo bali wao ndio walioingia katika eneo la Tanzanite One na kukutana na maji yaliyopo chini.
"Kwanini tufanye hivyo, wakati wote sisi tunataka kuimarisha uhusiano mzuri na wachimbaji wadogo na tumefikia hata hatua ya kutoa wataalam wetu kuwasaidia wapate madini?" alihoji Harebottle.
Alisema mara kwa mara, wachimbaji hao, wamekuwa wakitoa tuhuma hizo lakini kila baada ya uchunguzi kufanyika, hubainika kuwa madai yao si ya ukweli.
"Sisi wakati wote tumekuwa tukitaka ukweli wa suala hili ujulikane...haiwezekani tupeleke maji kwao kwani wao eneo walilopo ya kitalu B lipo juu yetu na pia hata mwelekeo wa kuchimba ni tofauti," alisema Harebottle.
Hata hivyo, alisema tatizo la msingi lililopo kwa wachimbaji hao ni kutokuwa na teknolojia ya kisasa ya kuchimba hasa baada ya kufika katika maeneo ya maji ambayo pia yapo katika eneo lao la kitalu C.
Afisa madini Kanda ya Kaskazini, John Nayopa, alisema ofisi yake tayari imeanza uchunguzi juu ya tatizo hilo.
"Tayari kuna maafisa wapo Mererani wanachunguza hilo nadhani muda si mrefu taarifa itatolewa," alisema Nayopa.
Mkoani Tanga, mvua hizo pia zimesababisha shughuli za utembezaji watalii na wageni kwenye mapango ya Amboni kusimama kwa muda usiojulikana, hadi hapo hali itakapokuwa shwari kutokana na eneo hilo kujaa maji na miundo mbinu kuharibika.
Mkuu wa Kituo cha Amboni, Misara Bwire, alitoa taarifa hiyo juzi na kubainisha kwamba wamelazimika kusimamisha shughuli kuanzia juzi kwa kuwa mto Mkurumuzi, uliopo jirani na mapango hayo, umejaa maji ambayo sasa yanaingia ndani ya mapango hayo hivyo kuharibu baadhi ya maeneo.
Alisema maji hayo yaliyosababisha mafuriko, yameharibu barabara inayoingia mapangoni, ikiwa ni pamoja na kung'oa vibanda vinavyotumika kwa ajili ya wageni kupumzika na mabango yanayoelekeza shughuli zinavyofanyika kwenye eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa kituo alisema wamelazimika kusimamisha shughuli na uongozi wao unajaribu kufanya kila jitihada kutafuta utaratibu wa kuwasiliana na wizara husika ili kuangalia namna ya kupata fedha za kuyafanyia ukarabati maeneo yaliyoharibika.
"Kwa kweli hali ilivyo wakati huu siyo nzuri, hivyo kiusalama tumeamua kusimamisha shughuli za utembezaji wageni ndani ya mapango kwa kuwa maji ni mengi na mengine yanaingia ndani ingawa siyo kwa kiasi kikubwa, mvua ikizidi hali inaweza kuwa mbaya zaidi," alisema
Ametoa wito kwa wageni wenye mpango wa kufanya safari za kutembelea mapango hayo kusubiri hadi mvua zitakapopungua ili kuweza kuyafanyia ukarabati mapango hayo.