Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa aomba Tanzania ipewe dawa za ‘ARV’
Lowassa aomba Tanzania ipewe dawa za ‘ARV’
By Habari Tanzania | Published  06/1/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu
 
WAZIRI MKUU Edward Lowassa amesema Tanzania hivi sasa inahitaji dawa za kurefusha maisha (ARV’s), mafunzo na vifaa ili kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi kwa upana zaidi.
 
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dar es Salaam jana ilimkariri Lowassa akisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya wananchi na watumishi wa sekta ya afya na vifaa, hasa mashine za kupima virusi vya ukimwi (VVU) ili kukabiliana na ugonjwa huo.
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema licha ya upatikanaji wa dawa, kunatakiwa pia kuwe na uhakika wa upatikanaji wa chakula, kwani wanaotumia dawa hizo pia wanahitaji kula vizuri.
 
Aliyasema hayo juzi alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu na Watoto (UNICEF) Ann Venemen ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya UKIMWI (UNAIDS), Peter Piot katika hoteli ya Intercontinental, jijini New York, Marekani.
 
“Idadi ya watu wanaopata dawa za kurefusha ni dogo ukilinganisha na idadi ya watu walioathirika nchini na tena tunahitaji kutoa mafunzo kwa watumishi zaidi ya 10,000 ili waweze kuongeza ujuzi katika mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU),” alisema Waziri Mkuu.
 
Aliwashukuru viongozi hao kutokana na kazi nzuri inayofanywa na mashirika yao katika maeneo mbalimbali yakiwemo elimu, afya na ukimwi.
 
Naye Mkurugenzi wa UNICEF alimweleza Waziri Mkuu kuwa ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kuhamasisha wananchi na suala zima la vita dhidi ya ukimwi na kuongeza: “Ukizunguka na kuzungumza na watu ndipo unapoweza kuona mabadiliko halisi.”
 
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba alipokuwa nchini Tanzania mapema mwaka huu, alizuru mkoa wa Mwanza na alipoongea na vijana wa kijiweni aliwauliza ni kitu gani ambacho wangependa wafanyiwe endapo wangepata nafasi ya kushiriki vita dhidi ya UKIMWI na wengi wao walimjibu wangependa kupima afya zao.
 
“Nilipowauliza wangapi wako tayari kupima kama watapatiwa nafasi hiyo, vijana wapatao 40 hadi 50 waliokuwapo katika kundi hili walinyoosha mikono yao… kwa kweli nilishangazwa na utayari waliokuwa nao wa kutaka kujua afya zao, na hili limetokea kutokana na juhudi za serikali kuhamasisha watu juu ya upimaji,” alisema Mkurugenzi wa UNICEF.
 
Naye Piot alimweleza Waziri Mkuu kwamba kasi ya maambukizi miongoni mwa vijana imeanza kupungua katika nchi zote tatu za Afrika Mashariki, hasa katika maeneo ya mjini.
 
“Pia, tumeingia katika kipindi ambacho watu wameanza kujadili mambo ambayo zamani yalionekana kuwa mwiko… hali hii imeongeza uwazi katika suala la vita dhidi ya ukimwi na hivyo kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi,” alisema Piot.
 
Leo asubuhi Waziri Mkuu atakutana na Mkurugenzi wa Utawala wa UNDP, Kemal Davis na pia atahudhuria kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ambaye pia ni Rais wa Congo, Dennis Sassou-Nguesso atahutubia ili kuhitimisha uenyekiti wa nchi hiyo katika Baraza la Usalama. Congo ilishika kiti tangu Mei Mosi, Mwaka huu wakati Tanzania ilishika kiti hicho Januari, mwaka huu.
 
Mchana, Waziri Mkuu atakutana na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kujikinga na maafa ya Tsunami, Robert Piper na jioni atakutana na baadhi ya kampuni zinazotaka kuwekeza nchini Tanzania.
 
Kesho atahudhuria chakula cha mchana kilichoandaliwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Ian Leeason kujadili masuala ya watu wanaoishi na virusi kabla ya kukutana na Charles Grey na wawakilishi wa kampuni zinazojishughulisha na usambazaji wa dawa za kurefusha maisha.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.