MAKAMPUNI sita kutoka nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Australia, India na Israel, yameonyesha nia ya kuwekeza kwenye mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma.
Hata hivyo pamoja na makampuni hayo kujitokeza bado serikali haijaamua kuutoa mradi huo kwa mwekezaji, ikitafuta kwanza tafsiri sahihi ya kumpata mwekezaji ambaye atazingatia maslahi ya taifa na ya kwake.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Benard Membe, alipokuwa akijibu swali ya mbunge wa Masasi, Raynald Alfons, aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kuyatumia makaa ya mawe ili kuzalisha nguvu za umeme.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa kulinda maslahi ya taifa, kama vile bei ya umeme endelevu, utunzaji wa mazingira na ukubwa wa mradi huo ambao unaunganishwa na uendelezaji waa mradi wa chuma wa Liganga, serikali inabidi iwe makini katika kupata mwekezaji atakayezingatia masuala hayo muhimu kwa taifa.
Hata hivyo, Membe, alisema serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), iliunda kamati ya wataalamu ili kupitia mapendekezo na kupendekeza njia nzuri za kumpata mwekezaji ambaye atazingatia maslahi ya pande zote mbili.
Alisema mradi huo wa Mchuchuma umeingizwa katika mpango wa maendeleo wa Mtwara Corridor ambao upo chini ya Wizara ya Miundombinu na mpango wa Power Sector Master Plan (PSMP) wa miaka 25 Aliongeza kwamba mradi huo unaainisha vyanzo muhimu ikiwemo nishati mbadala ya uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe, ukubwa wa mradi, makisio ya gaharama na wakati muafaka wa kutekeleza mradi. .