Na Richard Kilumbo,Kyela SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaban Simba, amesema waislamu nchini wanakusudia kujenga shule za sekondari 105 nchi nzima na kuwataka waislamu kupitia misikiti yao kuanza kuweka mikakati kwa kila wilaya kuwa na sekondari moja ya Kiislamu.
Akizungumza na waumini wa kiislamu hivi karibuni katika Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Kyela, alisema shule hizo zitawapa nafasi waislam ya kuendelea na masomo na kuufuta ujinga kwa nguvu zao zote.
Alishangazwa kuona waislamu wengi ‘wamepiga teke’ suala la elimu na badala yake wanafundisha elimu moja, na kusema kwamba hali hiyo inawakwamisha katika mambo mengi na kushindwa kuwasilisha ujumbe wa Mungu ipasavyo. Sheikh Mkuu alisema kuwa ujenzi wa shule hizo nchi nzima ni hatua za mwanzo za kuanzia katika kmapambano dhidi ya na adui ujinga ambao alidai umewakumba waislam wengi.
Aliwataka waislamu kuwapa kipaumbele wanawake katika suala zima la elimu kwa kuwa wanawake wakielimishwa wanakuwa wameuelimisha umma kwa ujumla. Pia aliwataka waislamu kuwa mfano katika jamii inayowazunguka kwa kujenga tabia njema ya kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali kama alivyokuwa akifanya Mtume wao.