Na Juma Pinto, London
MALKIA wa Uingereza, Elizabeth II ameahidi kutembelea Tanzania atakapopata nafasi ya kufanya hivyo wakati wowote katika kipindi kijacho.
Malkia alisema hayo juzi wakati Balozi wa Tanzania nchini hapa, Bibi Mwanaidi Maajar alipokwenda katika Kasri la Malkia lililoko Buckingham Palace, kukabidhi hati za utambulisho kwa kiongozi mkuu huyo wa Uingereza.
“Kwanza alinipongeza kwa kuwa hii ndio nafasi yangu ya kwanza kuchaguliwa kumwakilisha Rais, pili alitaka kujua natoka mkoa gani katika Tanzania na kumwambia mkoa wa Kilimanjaro,” alisema Balozi Maajar.
Balozi alisema baada ya hapo, Malkia alimwambia alishafika huko kipindi cha nyuma, hivyo kumwahidi angependa tena kuitembelea Tanzania na kuangalia Mlima Kilimanjaro pindi atakapopata nafasi ya kufanya hivyo.
“Kweli ni mama mchangamfu na ana nguvu zake, anayeonekana mwenye afya, alifurahi sana na alipenda kujua mengi kuhusu Tanzania ya sasa...Ubalozi tutajitahidi kufanikisha ziara yake muda ukifika,” alisema Balozi Maajar.
Balozi Majaar ambaye ni mwanamke wa kwanza kuongoza Ubalozi wa Tanzania hapa Uingereza, alisema kulikuwa na watalii wengi wakipiga picha, "lakini kwa kweli nimefarijika sana kwa mapokezi mazuri ambayo Malkia Elizabeth alituonesha mimi na ujumbe wangu tulipofika Buckingham Palace."
Katika utambulisho huo, Balozi Maajar alitumia usafiri wa gari maalumu linalovutwa na farasi huku akifuatana na mumewe, Bw. Maajar na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi, Bi. Radhia Msuya.
Maofisa wengine wa Ubalozi waliofuatana na Balozi ni Mwambata wa kijeshi, Brigedia Jenerali Mwanga, Mkuu wa Idara ya Uhamihaji, Bw. Sylvester Ambokile na Mshauri wa Masuala ya Sheria, Bw. Carol Kitana.
Msafara huo ulianzia ubalozi wa Tanzania uliopo Bond Street, katikati ya Jiji saa sita mchana, na kuvutia watu wengi, hali iliyofanya watu kuacha shughuli zao na kuanza kupiga picha.
“Malkia wa Tanzania anakwenda kumwona Malkia Elizabeth, Buckingham Palace," alisikia mmoja wam walioshuhudia msafara huo akisema mara baada ya Balozi Maajar kuanza safari yake ubalozini kuelekea Buckingham Palace.
Mbali na magari mawili ya farasi, pia Balozi Maajar alisikindikizwa na pikipiki za Polisi zilizokuwa zikisimamisha magari ili kupisha msafara wake.
Mara baada ya kumaliza utambulisho, Balozi alirudi ofisini na kupokewa na wafanyakazi kwa nyimbo.
Katika tafrija fupi iliyofanyika ubalozini hapo, mabalozi kadhaa wa nchi za Afrika wakiwamo wa Kenya, Algeria, Zambia, Malawi na nchi nyingine za SADC na Waziri wa Utalii wa Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe, walijumuika.