Imeathiriwa na matatizo makubwa manne
Uti wa mgongo wa majambazi mbioni kuvunjwa
SUMATRA yaagizwa kusimamia nauli
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema bajeti ijayo ya serikali haitakuwa nzuri kutokana na nchi kuathiriwa na matatizo ya ukame, njaa, umeme na upandaji wa bei ya mafuta.
Alisema hayo wakati akilihutubia Taifa jana kwa njia ya redio na televisheni katika utaratibu aliojiwekea.
"Bahati mbaya bajeti imeandaliwa wakati uchumi wa nchi umetikiswa na matatizo ya ukame, upungufu wa chakula, umeme na bei kubwa za mafuta," alisema Rais Kikwete akizungumzia mwelekeo wa bajeti ya serikali ya mwaka 2006/2007.
Alifafanua kuwa, hali hiyo inaweza kuwa na athari kwa bajeti hiyo itakayowasilishwa bungeni tarehe 15 mwezi ujao.
Bajeti hiyo itakuwa ya kwanza tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani Desemba, mwaka jana.
"Ni dhahri kwamba hali hii inaweza kuwa na athari kwa mwenendo mzima wa bajeti ya mwaka ujao, ukuaji wa pato la taifa, na hasa uzalishaji katika sekta ya kilimo na viwandani," alisema na kuongeza:
"Pia inaweza kuathiri akiba ya pesa za kigeni, mapato ya serikali na hivyo kupunguza kwa kiasi fulani uwezo wetu wa kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo tuliyobuni."
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema ni dhamira ya serikali kuhakikisha hatua mbalimbali zinachukuliwa kupunguza makali ya athari hizo.
Kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, Rais Kikwete alisema kutakuwa ndio mwanzo wa safari ya miaka mitano ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na masuala mengine ya kitaifa.
"Tutaanza kuchukua hatua za kuongeza kasi ya kukuza uchumi na kupambana na umasikini wa kipato kwa Watanzania," alisema.
Akizungumzia hali ya ujambazi, Rais Kikwete amesema mapambano dhidi ya ujambazi na majambazi yenyewe yanaendelea kwa ari, nguvu na kasi.
"Hatutalegeza uzi hata kidogo. Tayari tumewanyima majambazi fursa ya kutamba kama ilivyokuwa siku za nyuma na kila siku tunazidi kuwabana zaidi na kupata ushindi... mwelekeo wa ushindi ni mzuri na sasa tunakaribia kuvunja uti wa mgongo wa ujambazi," alisema Rais Kikwete na kuvipongeza vyombo vya usalama na wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema serikali itaendelea kuviimarisha vyombo vya usalama kwa nyenzo na utaalamu viweze kufanya kazi zake kwa ukamilifu na ufanisi.
Kuhusu hali chakula, Rais Kikwete amesema upatikanaji wake ni tatizo kwa sababu bado kuna wananchi wanaoishi kwa kutegemea chakula cha msaada kutoka serikalini na kwa wafadhili.
Alisema chakula kilichokuwepo katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula kilisaidia kukabiliana na tatizo la njaa na kama kisingekuwepo hali ingekuwa mbaya zaidi.
Kwa sasa, alisema Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Joseph Mungai, ameshaanza kuchukua hatua kuhakikisha Hifadhi hiyo inakuwa na akiba ya kutosha wakati wote bila kujali kama nchi imepata mvua au la.
"Ni jambo lililo wazi kuwa, kilimo chetu bado ni duni na hakina tija ya kutosha. Hali hii inasababisha matatizo kila tunapokosa mvua hata kama kwa msimu mmoja kama ilivyokuwa safari hii...
“Tumedhamiria kuchukua hatua za dhati kuboresha kilimo chetu. Kwa ajili hiyo tuko mbioni kukamilisha mkakati kabambe wa kuendeleza kilimo chini," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete amesema tatizo la umeme halijaisha, ingawa kumekuwepo na unafuu katika siku za hivi karibuni ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miezi iliyopita.
"Bado hali katika bwawa la Mtera ni mbaya, ingawaje kina kimepanda kwa mita tatu tu hadi kufikia mita 690 tangu msimu wa mvua uanze. Kina hicho ni pungufu kwa mita nane na msimu wa mvua ndio umefika ukingoni," alisema.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete amesema mgao wa umeme utaendelea hadi hapo hatua za dharura za kuongeza uzalishaji wake kwa kutumia gesi zitakapokamilika.
"Tayari utaratibu wa kuipatia TANESCO mitambo mipya ya megawati 100 itakayofungwa pale Ubungo umekamilika. Uagizaji wa mitambo hiyo utafanyika wiki chache zijazo baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi," alisema.
Wiki ijayo, alisema TANESCO na serikali zinatarajiwa kukamilisha mazungumzo kuhusu uagizaji kutoka nje wa mitambo ya kukodisha ya megawati 100, huku maandalizi ya awali ya mradi wa umeme wa Kinyerezi na ule wa makaa ya mawe Kiwira yakiwa yanaendelea vizuri.
Akizungumzia upandaji wa bei za mafuta, Rais alisema ni tatizo linaloathiri nchi zote duniani na Tanzania haina uwezo wa kulizuia, kwani haizalishi mafuta, na uchumi wake hauwezi kuhimili kutoa ruzuku ya bei ya nishati hiyo.
"Napenda kuitumia nafasi hii kuwaonya watu wenye tamaa ya utajiri iliyokithiri wasitumie fursa hiyo kudhulumu. Si sawa, si haki na ni kukosa utu kufanya hivyo. Kwa kweli si jambo jema hata kidogo kwa mtu au kampuni kutumia shida za wananchi kupata utajiri wa haraka haraka," alionya Rais Kikwete.
Alizitaka Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kusimamia ipasavyo bei za mafuta na nauli za mabasi na vyombo vingine vya usafiri kuhakikisha taratibu zinazingatiwa.