Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tatizo la ukosefu wa ajira lisigeuzwe mtaji wa kisiasa
Tatizo la ukosefu wa ajira lisigeuzwe mtaji wa kisiasa
By Habari Tanzania | Published  11/9/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Tonny Adams

JITIHADA zote za kutokomeza umasikini nchini zitagonga mwamba iwapo tatizo la ukosefu wa ajira litaendelea kuchukuliwa kisiasa, badala ya kulikabili kisayansi kwa kujenga utamaduni wa kulifanyia utafiti unaohitajika kila inapobidi.

Kwa kujenga na kuendelea kuimarisha msingi wa takwimu (statistical base) za ajira na nguvu kazi, mamlaka zinazohusika na zoezi hilo zitaweza kubainisha kiwango halisi cha ukosefu wa ajira kilichopo nchini (the current official rate of unemployment) wakati wowote itakapohitajika kufanya hivyo.

Kupata ajira ni haki ya kimsingi ya kila Mtanzania. Ni wajibu wa Serikali kutengeneza mazingira muafaka (enabling environment) yatakayo mhakikishia kila Mtanzania fursa ya kuweza ama kujiajiri mwenyewe au kuajiriwa.

Tatizo la ukosefu wa ajira nchini lisije likageuzwa kuwa mtaji wa kisiasa hususan inapobainika kwamba mara nyingi Watanzania waliokosa ajira na wanaoishi katika mazingira yenye kiwango kikubwa sana cha ukosefu wa ajira (a regime of high unemployment rates), hususan wale wenye kiwango duni cha elimu na wasio na ujuzi wa stadi zozote za kiufundi, ni watu wepesi sana kuswagwa kisiasa kwa manufaa ya wanasiasa wenye upeo finyu na wenye dhamira ya kuimarisha himaya zao.

Hivi sasa kila utakaye muuliza kuhusu kiwango halisi cha ukosefu wa ajira nchini, atakujibu hakifahamu. Hata hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2006/07 iliyowasilishwa Bungeni Juni mwaka huu, haikuwa hata na ibara moja iliyotoa ufafanuzi wa kina kuhusu kiwango cha ukosefu wa ajira nchini. Wizara hiyo ndiyo Wizara mama inayoshughulikia masuala yote yanayohusu soko la ajira hapa nchini.

Karibu nchi zote ulimwenguni zilizopata mafanikio makubwa ya kiuchumi, kila zilipotoa malengo ya kijumla ya uchumi mpana (macro economic objectives) katika mipango yake ya maendeleo, mbali na kutoa malengo ya kasi ya kukua kwa uchumi au Pato la Taifa na kudhibiti mifumuko ya bei, nchi hizo pia zilitilia mkazo malengo ya kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira na kuimarisha zaidi kiwango cha tija katika uzalishaji mali (labour productivity) pamoja na kuboresha zaidi matumizi ya rasilimali zilizopo lakini zilizodumaa na hazitumiki (idle Resources enhanced exploitation) kwa maendeleo makubwa zaidi katika nchi.

Kwa kutokuwa na kipimo cha kiwango halisi cha ukosefu wa ajira nchini, Serikali itakuwa inakwepa wajibu wake. Kiwango hicho ndicho kitakachoiwezesha Serikali kuandaa sera sahihi zaidi na muafaka zitakazohusu maendeleo ya sekta nyingine zote katika uchumi hadi marekebisho ya mitaala ya elimu katika nyanja mbalimbali ili hatimaye elimu itakayotolewa nchini iwe na uwezo wa kutoa wahitimu walioiva na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za utandawazi uliotawaliwa na nguvu za teknolojia za kisasa na stadi adimu za kiufundi.
Katika kile kinachoashiria kwamba mfumo wa utayarishaji wa mipango yetu ya maendeleo, mara nyingi na kwa kiasi kikubwa umekuwa ukitokana na shinikizo za wafadhili wa nje (The Debt Trap), na wakati mwingine maagizo kutoka taasisi za fedha za kimataifa (the Monetarist School), hususan Shirika la Fedha la Kimataifa
(The IMF) na Benki ya Dunia (The World Bank) zaidi kuliko mahitaji yatokanayo na vipaumbele vyetu wenyewe na msukumo wa fikra za wasomi wetu nchini, msisitizo katika malengo ya kijumla (macro economic objectives) ya mpango wa maendeleo kwa mwaka 2006/07 umejikita zaidi katika mwelekeo huo.

Matatizo yetu ya kiuchumi ya kimsingi ni yale yanayohusiana na mifumo iliyopindika na isiyowiana ya kiuchumi (structural imbalances, the legacy of the colonial past), zaidi kuliko yale yanayohusiana na utengemano katika sera za fedha (monetary stability).

Kwetu sisi, tatizo nyeti zaidi la kiuchumi ni kutokuwapo kwa uwiano maridhawa katika mifumo ya uchumi baina ya sekta mama za viwanda na kilimo kwa upande mmoja na sekta za miundo mbinu na huduma za kijamii kwa upande mwingine. Zaidi kuliko kuwapo kwa kukithiri kwa ujazi wa fedha nchini (excessive money supply in circulation).

Lakini kama itakavyobainika katika malengo ya kijumla (macro economic objectives) ya mpango wa maendeleo kwa mwaka 2006/07, msisitizo umejikita zaidi katika kudhibiti ujazi wa fedha nchini (restrict money supply), kwa lengo la kudhibiti mfumuko wa bei (curb inflation rate) na wakati huo huo kuimarisha zaidi kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na kodi na vyanzo vingine vya ndani.

Hatua zote hizo zikitarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Kasi hiyo ya kukua kwa uchumi itatokana na nini ni suala lililoachwa wazi. Ufafanuzi wa kina kuhusu suala la ajira halikujitokeza kabisa katika malengo hayo.

Kwa kawaida, malengo ya kijumla ya mpango wowote wa maendeleo yatapaswa kugusia maeneo manne muhimu yafuatayo:
Kwanza, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi; Pili, kudhibiti mfumuko wa bei nchini; Tatu, kudhibiti na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini; Nne, kuongeza kiwango cha ufanisi na tija katika uzalishaji mali (labour productivity). Kwa ujumla, hivyo ndivyo viashiria vitakavyomwezesha yeyote kubainisha ama kukua au kudorora kwa uchumi kwa mujibu wa sera zilizopo.

Ni kutokana na malengo hayo ya kijumla (macro economic objectives) kwamba matatizo ya kimsingi ya kiuchumi yatakayopimwa mafanikio yake ni pamoja na haya yafuatayo:Kwanza, tatizo la kudorora kwa uchumi (economic stagnation). Iwapo kasi ya ukuaji uchumi ni ndogo kuliko ilivyotarajiwa au uzalishaji umezidi kuporomoka ama hakuna ongezeko lolote katika kasi ya ukuaji wa uchumi. Kwamba ukuaji wa uchumi umebaki palepale bila ya ongezeko lolote.
Pili, tatizo la mfumuko wa bei. Iwapo uwanda wa viwango vya bei nchini umezidi kuongezeka mfululizo kadri siku zilivyopita kwa kipindi kirefu au kinyume chake. Na kwanini hali iliendelea kuwa hivyo. Tatu, tatizo la ukosefu wa ajira na matumizi finyu ya rasilimali zilizopo (Idle resource use and unemployment). Na kwanini hali iliendelea kuwa hivyo. Nne, tatizo la uwezo mdogo wa ushindani katika soko la kimataifa (noncompetitiveness across countries). Vipimo vya ushindani vikiwa ni viwango vya tija katika uzalishaji kimataifa (labour productivity).

Utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya nchi utapimwa kwa kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kufanikisha malengo hayo manne ya kijumla (macro economic objectives). Viwango vya ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na kodi na vyanzo vingine vya ndani au kiwango cha akiba za fedha za kigeni za kutosheleza mahitaji ya miezi isiyopungua saba ya bidhaa za nje ni malengo ya ziada yaliyo nje ya malengo ya kimsingi ya uchumi mpana (the core macro economic objectives). Kwa mfano, kuvuka lengo lililowekwa la ukusanyaji wa mapato ya Serikali hakumaanishi moja kwa moja kwamba uchumi umekua kwa kasi iliyokusudiwa. Hali kadhalika, kufanikiwa kwa lengo la akiba ya fedha za kigeni zitakazotosheleza mahitaji ya miezi saba ya bidhaa za nje hakumaanishi kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi imefanikiwa kama ilivyokusudiwa.Malengo ya kijumla ya mpango wa maendeleo kwa mwaka 2006/07 ni haya yafuatayo:Kwanza, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ifikie asilimia 5.9% mwaka 2006; ifikie asilimia 7.3% mwaka 2007; na hatimaye ifikie asilimia 7.7% mwaka 2008;
Pili, kudhibiti kasi ya upandaji wa bei isizidi asilimia 4% (kwa bei za 2001) ifikapo Juni 2007, kwa kigezo cha NCPI.

Tatu, ukusanyaji wa mapato ya ndani ufikie asilimia 14.5% ya Pato la Taifa mwaka 2006/07; ufikie asilimia 14.7% ya Pato la Taifa mwaka 2007/08; na hatimaye ufikie asilimia 14.8% ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2008/09;
Nne, ongezeko la ujazi wa fedha (kwa tafsiri pana ya M2), uwiane na kasi ya ukuaji uchumi sambamba na kasi ya mfumuko wa bei;
Tano, kujenga akiba ya fedha za kigeni itakayotosheleza mahitaji yasiyopungua ya miezi saba ya bidhaa za nje.

(Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha Bungeni 2006/07, ibara ya 23; Bajeti ya Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji , ibara ya 109 kwa mwaka 2006/07). Ni dhahiri kwamba malengo ya viwango vya ukosefu wa ajira nchini, pamoja na viwango vya tija katika ushindani wa uzalishaji mali hayakujitokeza katika malengo yaliyotajwa hapo juu. Na badala yake msisitizo umeelekezwa katika ujazi wa fedha na mapato ya ndani ya Serikali pamoja na mahitaji ya fedha za kigeni kwa manunuzi ya bidhaa za nje.Badala ya mpango kuelekezwa katika malengo ya kimsingi na ya kijumla (core macro economic objectives), umeelekezwa badala yake katika malengo ambayo ni matokeo ya malengo ya kimsingi ambayo yangepaswa kuwamo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.