Na Mwandishi Wetu, Muheza
WATAHINIWA zaidi 350 wa shule nne za Sekondari Wilayani Muheza wameshindwa kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha pili kwa siku mbili kufutokana na mvua kubwa kuonyesha na kusababisha mafuriko.
Kufuatia maafa hayo, Afisa Elimu Mkoa wa Tanga, Andrew Mpalile, amelazimika kuiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kutunga mitihani mingine ili kufidia pengo hilo.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Abdulaziz, alipotembelea Kijiji cha Miyanga kushuhudia eneo lililokumbwa na maafa, baada ya kutokea mfauriko na kusomba nyumba na mali za wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shule ambazo watahiniwa hawakuweza kufanya mitihani ni Magila, Mbaramo, Kerenge na Muheza Muslim na mitihani ambayo haikufanywa ni ya Hisabati, Civics, Historia na Kiingereza.
“Watahiniwa zaidi ya 350 wameshindwa kufanya mitihani na kwa kuwa hiyo ni dharura ya kimaafa, Idara ya Elimu Mkoa wa Tanga, imelazimika kuwasilisha ombi maalumu kwa wizara kuomba watungiwe mitihani mingine ili kufidia pengo,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Kondo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kuanzia juzi, watahiniwa hao waliweza kuendelea kufanya mitihani mingine ya kitaifa kama kawaida baada ya mvua kupungua.
Abdulaziz aliyeambatana na ujumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tanga, alishuhudia maafa makubwa yaliyotokea baada ya mvua hiyo ambapo licha ya Kaya 152 kukosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kusombwa pia, ilielezwa kuwa zaidi ya magunia 64 ya mahindi, sita ya mpunga, mifugo na ekari 40 za mazao mbalimbali, zimesombwa na mafuriko hayo.
Abdulaziz aliuagiza uongozi wa serikali ya Wilaya ya Muheza kukihamisha Kitongoji cha Miyanga kutoka katika eneo kilichokuwepo na kukipeleka eneo lingine kwa kuwa limezungukwa na mito miwili ya Furahisha na Kihuhwi.
“Kama mnavyoona Kitongoji kimezingirwa na maji na kutoka na jiografia iliyopo, ni hatari kuendeleza makazi eneo hili hivyo nauamuru uongozi kuwatengea eneo lingine litakalokuwa salama zaidi,”alisema Abdulaziz.
Serikali imeahidi kupeleka magunia 31 ya mahindi kwa ajili ya waathirika na mahema 30 yalianza kujengwa juzi na wataalamu kutoka makao makuu ya wilaya ili kuwahifadhi watu waliokosa mahali pa kuishi.