SERIKALI imesema imegundua kuwepo kwa madini ya aina mbalimbali katika Wilaya ya Lushoto, mkaoni Tanga na inaandaa utaratibu wa kuwaruhusu wachimbaji wadogo kuanza kuyachimba hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Madini na Nishari, Benard Membe, alieleza hayo bungeni jana, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo, aliyetaka kujua ni lini taarifa ya wataalamu waliopelekwa Lushoto kutafiti upatikanaji wa madini itatolewa.
Akijibu swali hilo, Membe, alisema taarifa ya utafiti huo ulioanza Machi 2005 na kukamilika Agosti mwaka huu imeshatolewa na kwamba inapatikana katika Ofisi za Geological Survey of Tanzania (GST) zilizopo mkoani Dodoma.
Alibainisha kuwa uchunguzi huo uliofanywa katika miamba iliyopo kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya ya Lushoto, ulibaini kuwepo kwa madini ya aina mbalimbali katika maeneo hayo kama dhahabu, nikel, vito, mable, gemestone, oxide na shaba.
Alisema kufuatia uvumbuzi huo, wachimbaji wadogo hivi karibuni wataanza kuruhusiwa kuchimba madini hayo.
Alisema Machi mwaka jana, wizara yake ilituma wataalamu kutoka ofisi za GST kwenda kufanya utafiti wa awali wa madini Lushoto, hasa yaliyoko nje ya hifadhi ya misitu, ili kuyatenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Aliongeza kuwa serikali inakusudia kuiangalia upya sheria ya uchimbaji wa madini ili kuwawezesha wachimbaji wazawa kumiliki asilimia 100 ya uchimbaji wa vito, badala ya asilimia 25 ya sasa na nyingine kuachiwa wageni.