Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Ramadhan Semtawa  »  Dar hatarini kuzama baharini
Dar hatarini kuzama baharini
By Ramadhan Semtawa | Published  11/8/2006 | Ramadhan Semtawa | Unrated

Na Ramadhan Semtawa

MAENEO ya fukwe za Bahari ya Hindi katika jiji la Dar es Salaam, yako hatarini kumezwa na maji baada ya maji ya bahari kuongezeka kutokana na ongezeko la joto duniani.

Onyo hilo limo katika ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambalo limeanisha maeneo ambayo yanakabiliwa na kitisho hicho, likiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Maeneo mengine yatakayoathirika na tatizo hilo ni fukwe za za bahari ya Hindi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, vikiwemo visiwa vya Comoro, mji wa Durban, Afrika Kusini na Beira, Msumbiji.

Iwapo janga hilo litazikumbuka fukwe za jiji la Dar es Salaam, litaathiri zaidi hoteli kubwa za kitalii na hata baadhi ya ofisi za mashirika ya kimataifa, ofisi za balozi mbalimbali na shughuli za watu binafsi.

Maeneo mengine yanayoweza kuathirika na janga hilo ni pamoja na nyumba za mabalozi, makazi ya watu binafsi, ikiwemo nyumba za kifahari zilizopo katika fukwe na maeneo ya karibu na mlango wa bahari unaopita karibu na kituo kidogo cha polisi cha Salender.

Tofauti na janga la Tsunami ambalo ni la muda, ongezeko la kina cha bahari litakuwa ni janga la kudumu ambalo litahitaji kazi ya ziada na kugharimu fedha nyingi kwa ajili ya kuhamisha makazi yaliyopo ufukweni.

Ripoti hiyo inaonya pia kwamba, visiwa ambavyo havina mwinuko, hasa katika mwambao huo wa bahari, huenda vikapotea kabisa ifikapo mwaka 2080.

Licha ya ripoti ya hiyo ya WMO kuonya kuhusu mafuriko, lakini inasisitiza kwamba baadhi ya maeneo duniani yatakuwa na ongezeko kubwa la joto kutokana na kupuuzwa kwa utekelezaji wa mkataba wa Kyoto, Japan ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa kemikali na gesi za viwandani kwa asilimia tano.

Joto hilo litayeyusa barafu katika vilele vya milima na maeneo mengine ya bahari yaliyofunikwa na barafu na kuongeza kiwango cha maji katika bahari na kufanya maji hayo kuzifunika baadhi ya fukwe.

Akizungumzia hali hiyo ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Martin Lukando, alikiri kuwepo kwa tishio hilo na kusema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikilifuatilia suala hilo kwa makini.Lukando alisema hadi sasa vipimo vya kina cha maji katika Bahari ya Hindi vinaonyesha kwamba hali bado ni ya kawaida.

Alisema hatua nyingine ambazo hadi sasa zimekuwa zikichukuliwa ni pamoja kuimarisha mfumo wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na vituo vya kimataifa vya majanga kama ya Tsunami."Ni kweli taarifa hizo zipo, hata mimi nimezipata, tumeanza kuchukua hatua, kwa mfano, tuna utaratibu wetu wa kupima kina cha maji kila siku, hadi sasa kina kiko kawaida, " alifafanua Lukando.

Wakati TMA ikichukua hatua hizo, wanasayansi na wanazamzigira kutoka nchi zaidi ya 100 ikiwemo Tanzania, wako jijini Nairobi katika mkutano wa 12 wa dunia kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, ambao moja ya mada kuu ni namna ya kuibusuru dunia na mafuriko hayo.Mkutano huo wa 12 wa Umoja wa Mataifa ulifunguliwa jana mjini Nairobi na Makamu wa Rais wa Kenya, Moody Awori, ambaye alizitaka nchi zote zinazohusika na uharibifu wa hali ya hewa kushirikiana na nchi zingine ili kulikabili suala hilo linalotishia kuiangamiza dunia.

Tanzania inawakilishwa na ujumbe mzito katika mkutano huu, ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, wawakilishi kutoka wizara za serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na mashirika yasio ya kiserikali.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.