Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BUNGE limepitisha mkataba wa kuondoa viza kati ya Tanzania na Msumbiji na kinachosubiriwa sasa ni ridhaa ya Rais ili utekelezaji wake uanze.
Lengo la kuu la mkataba huo ni kuondoa matumizi ya viza kwa hati za kusafiria za kidiplomasia, utumishi wa umma na za kawaida kwa wananchi wa nchi hizo mbili na kuanzia sasa watakuwa wanatembeleana bila ya kikwazo hicho.
Nchi hizo mbili ziliingia mkataba huo wa kuondoa matumizi ya viza Oktoba 10, mwaka jana na ulikuwa unasubiri kuridhiwa na Bunge.
Akisoma mkataba huo bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai, alisema hatua hiyo itazidi kuimarisha husiano baina ya Tanzania na Msumbiji.
Alisema ibara ya tisa ya mkataba huo, inahitaji kukamilika kwa taratibu za kisheria ili makubaaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba yaweze kutumika.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuhusiana na mkataba huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Kusila, alitahadharisha kuwa wakati wa utekelezaji wake, vyombo vya ulinzi na usalama viwe makini ili kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.
Alisema kuna uwezekano wananchi wasio waaminifu wa pande zote mbili wakatumia fursa hiyo kuendesha uhalifu kama biashara ya dawa za kulevya, uingizaji wa silaha kinyume cha sheria na ujambazi.
Kamati hiyo imependekeza vituo vya uhamiaji katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji ambao ni mrefu viongezwe na Watanzania wahamasishwe kutumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza.