RAIS Jakaya Kikwete amekubali kuanzia leo (Jumanne Nov. 7, 2006) kujiuzulu kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ukiwaona Ditopile-Mzuzuri ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya raia
Alikuwa akijibu barua ya Ditopile-Mzuzuri aliyoiandika Jumapili Nov. 5 mwaka huu, siku moja kabla ya kufikishwa mahakamani, akimuomba Rais akubali kjiuzulu Ukuu wa Mkoa.
Rais alieleza: “kuomba kwako kujiuzulu wadhifa wako wa Mkuu wa Mkoa ni uamuzi wa busara na hekima. Unatoa fursa kwa taratibu stahiki za kisheria kufanyika bila ya vizuizi visivyokuwa vya lazima. Ni heshima kwa taifa letu linalozingatia utawala wa sheria”.
“Hivyo napenda kukuarifu kuwa nimekubali ombi lako la kujiuzulu wadhifa wa Mkuu wa Mkoa. Kwa mara nyingine tena pole kwa yote. Usiache kumshukuru na kumuomba Mungu”, Rais Kikwete ameeleza katika barua hiyo.
Rais Kikwete yuko safarini katika nchi za Asia.
Katika barua yake ya kuomba kujiuzulu, Ditopile-Mzuzuri alisema tukio lililotokea “linakingana na dhamira yangu ya wajibu wa kazi yangu ya Mkuu wa Mkoa”.
Aliomba kuwajibika na kutoa nafasi kwa mkondo wa sheria kuchukua nafasi yake vyema na kuacha serikali kufanya kazi yake kwenye murua upasao kwani “nikiendelea kuwepo madarakani itaathiri imani ya wananchi kwa serikali yetu”.
Source:
http://www.kikweteshein.com