SHIRIKA la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), lina mpango wa kununua ndege tatu kwa ajili ya kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwenye hifadhi.
Kati ya ndege hizo tatu, moja yenye uwezo wa kuchukua abiria 14 itafanya safari zake ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya usafiri kwa watalii watakaohitaji kwenda kutembelea hifadhi za kusini za Mahale iliyopo Kigoma, Katavi iliyopo Mpanda na Ruaha mkoani Iringa.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Zubein Mhita, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliyetaka kufahamishwa mipango ya serikali wa kupanua wigo wa utalii kwa kuzingatia bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Mhita pia alisema kuwa wamiliki makampuni ya uwindaji wa kitalii wameruhusiwa kuendesha biashara ya utalii wa picha kwa miezi ambayo uwindaji wa kitalii haufanyiki.
Alisema hatua hiyo ina lenga kutanua wigo wa utalii hasa kwa kutoa fursa za kuendeleza utalii wa picha kwa maeneo yale yasiyokuwa na hifadhi za taifa.