Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tanzania inavyoliwa kwenye madini
Tanzania inavyoliwa kwenye madini
By Habari Tanzania | Published  11/7/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKATI makampuni ya madini yameweza kujikusanyia jumla ya Sh2,339.63 bilioni katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali imeambulia Sh72.37 bilioni tu kama mrabaha kutokana madini.

Mbaya zaidi, fedha hizo za mrabaha pia zimemegwa kwa ajili ya kuilipa kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation (Asagbc), kiasi cha Sh38.7 bilioni na kufanya mapato halisi ya serikali katika kipindi hicho kubaki Sh33.6 bilioni tu.

Takwimu hizo zinatokana na hesabu iliyokokotolewa na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini na kutolewa bungeni na Naibu Waziri, Bernard Membe, wakati akijibu maswali ya wabunge.

Hata hivyo, Membe aliweka mkazo zaidi katika kiasi cha fedha ambazo serikali imeilipa Kampuni ya ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uendeshaji migodi ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation (Asagbc), akisema kutokana na ukubwa wa gharama, serikali inafikiria kuangalia upya mkataba na kampuni hiyo.

Kumekuwapo na malalamiko ya muda mrefu juu ya kiwango kidogo cha mrabaha ambacho serikali inayatoza makampuni ya madini, baadhi ya watu wakiulinganisha utaratibu huo na uporaji wa wazi wa rasilimali ya Watanzania.

Akizungumza bungeni mjini hapa jana Membe, alisema serikali inailipa kampuni hiyo fedha nyingi kila mwezi na kwamba kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka huu, imeshalipwa dola za Marekani 31 milioni (zaidi ya Sh38 bilioni).

Kwa mkataba uliopo, serikali inalipwa asilimia tatu ya mapato ya madini, lakini kutokana na kukodi kampuni ya kusimamia uendeshaji na uzalishaji katika migodi hiyo, inatumia asilimia 1.9 ya fedha hizo na yenye ikibakia na asilimia 1.1 tu.

Kiasi hicho cha fedha kilicholipwa kwa kampuni hiyo kimeelezwa kuwa ni kikubwa kuliko gharama zilizotumika kujenga jengo jipya la kisasa la Bunge lililogharimu Sh31 bilioni.

Kutokana na gharama kubwa inayoingia serikali kuilipa kampuni hiyo fedha nyingi kila mwezi, Membe alisema sasa inafikiria kuuangalia upya mkataba wa kampuni hiyo ili kuipunguzia mzigo serikali.

Alisema Juni, 2003, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa niaba ya serikali, iliingia mkataba wa miaka miwili na kampuni hiyo kwa lengo la kuhakiki uzalishaji na gharama za usafirishaji wa dhahabu pamoja na uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa nchini na kwamba mkataba huo ulimalizika Juni mwaka jana.

Hata hivyo, Naibu huyo Waziri wa Madini na Nishati, alisema baada ya mkataba huo kumalizika BoT haikuitisha tenda nyingine kama ilivyofanya mwaka 2003 na ikaipatia tena kampuni hiyo mkataba wa miaka miwili zaidi kwa kutumia kifungu namba 2.4 cha mkataba huo kinachoruhusu BoT kuongeza muda wa mkataba iwapo inaridhika na utendaji kazi wa kampuni hiyo.

Membe alikuwa akitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Aziza Sleyum Ally, aliyetaka kujua kampuni gani iliyopata tenda hiyo na kama ni kampuni hiyo iliyomaliza mkataba wake na je tenda hiyo ilitangazwa lini na ilipitishwa na nani.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.