Na Tausi Ally
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Kapteni Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (58), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la mauaji ya dereva wa daladala, Hassan Mbonde.
Pamoja na mamia ya watu kufurika mahakamani, eneo la mahakama lilijaa ukimya wakati mkuu huyo wa mkoa akipandishwa kizimbani.
Ditopile anayekabiliwa na shtaka la mauaji kwa kutumia bastola, alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3.09 asubuhi, akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliojaa kwenye magari mawili ya polisi aina ya Land Rover Defender.
Saa 3:54 asubuhi, Ditopile aliingizwa mahakama ya wazi, huku akiwa amevalia suruali yenye rangi ya kaki na shati la rangi mchanganyiko, miwani na mkononi wake wa kushoto ukiwa umefungwa bandeji.
Baada ya dakika mbili, Hakimu Michael Luguru, aliingia mahakamani na Mwendesha Mashtaka, Mrakibu wa Polisi, Germanusi Muhume, alimsomea Kapteni Ditopile shtaka la mauaji linalomkabili. Wengine waliokuwepo ni Mrakibu wa Polisi Naima Mwanga na Inspekta Raphael Rutaihwa.
Muhume alidai kuwa, Novemba 4, 2006 majira ya saa 1:00 usiku katika eneo la njia panda ya Bagamoyo na Kawe wilayani Kinondoni, Ditopile alimuua Hassan Mbonde.
Baada ya kusoma mashtaka, Muhume alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaiomba mahakama ipange siku nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza shtaka linalomkabili. Mahakama Kuu ndio yenye uwezo wa kusikiliza mashtaka ya mauaji.
Kabla Hakimu Luguru, hajaaihirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, mwaka huu, mawakili wanaomtetea mtuhumiwa, Dk Ringo Tenga, Losan Mbwambo, Cuthbert Tenga na Samwel Mapande, walidai kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa aliumizwa mkono, hali iliyosababisha polisi kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufanyiwa matibabu.
Mawakili hapo hao waliiomba mahakama imruhusu mteja wao aonane tena na daktari wake ili kumpima afya yake.
Dk Ringo, aliomba mahakama imruhusu mtuhumiwa huyo afikishwe hospitali kwa kuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu na pamoja na kisukari na kwamba, juzi shinikizo lilipanda hadi kufikia 180.
Wakili huyo alidai kuwa mteja wake pia ameshtushwa na gazeti moja lililoripoti kuwa, 'Ditopile Kunyongwa' akidai kwamba limemhukumu na kuongeza kuwa linaweza kumpeleka pabaya mtuhumiwa, hoja ambayo iliungwa mkono na upande wa mashtaka.
Baada ya Hakimu Luguru kuahirisha kesi hiyo majira ya saa 4:07, Ditopile aliingizwa kwenye gari ndogo ya saluni yenye vioo vya giza na kuondoka eneo la mahakama.