Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mimba, ndoa za wanafunzi zamtisha waziri mkuu
Mimba, ndoa za wanafunzi zamtisha waziri mkuu
By Habari Tanzania | Published  11/6/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, ameshtushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi wa shule za msingi, wanaokatisha masomo kwa ajili ya kuolewa ama kupewa mimba mkoani Dodoma.

Kutokana na hali hiyo, ameagiza wazazi waliowaachisha watoto wao masomo kwa ajili ya kuwaoza, wawarejeshe mara moja shuleni ama watachukuliwa hatua, na kwa wale waliowapa mimba ameamuru wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.

Lowassa alitoa agizo hilo wakati alipokuwa akihutubia wananchi wa Kijiji cha Mnase, mkaoni hapa, muda mfupi baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijiji hicho, pamoja na kupokea taarifa za elimu na kilimo za mkoa wa Dodoma zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa, William Lukuvi.

Awali wakati akitoa taarifa ya elimu ya mkoa, Lukuvi alimwambia Lowassa kuwa asilimia 26 ya wanafunzi walioanza darasa la kwanza mwaka 2000, wameshindwa kumaliza shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kukatishwa masomo kwa ajili ya kuozwa ama kutiwa mimba. Alianisha kuwa kati ya wanafunzi walioanza shule ya msingi mwaka 2000, walioacha kwa sababu ya utoro ni 1,376, mimba 175, ugonjwa 33, vifo 100 na 118 waliacha kwa sababu ya kukosa ada na michango mbalimbali.

Akizungumza na wanakikiji cha Manase, Lowassa, alisema kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha ya baadaye ya watoto na maendeleo ya taifa kwa ujumla, hivyo akawataka wazazi kuhakikisha kuwa wanawasomesha watoto wao. “Inasikitisha kuona makabila ambayo hayajaendelea ndiyo ambayo hayataki kuendelea. Jamani ndugu zangu bila ya kuwapa elimu watoto wenu mtaendelea kubaki kama mlivyo, hivyo jitahidini kuhakikisha wanamaliza masomo yao,” alisisitiza Waziri Mkuu Lowassa.

Alisisitiza agizo la Rais Jakaya Kikwete, la kutaka watu wote waliowaachisha watoto shule, wakamatwe na kuwarejesha shuleni mara moja. “Inasikitisha mkoa wa Dodoma ni moja ya mikoa ambayo hadi sasa haijatekeleza agizo la Rais. Sasa nawakumbusha tena wakamateni watu wanaowaachisha watoto shule na kuwarejesha shule mara moja,” aliongeza.

Awali kabla ya kuzungumza na wanakijiji wa Manase, Lowassa alikagua shamba la miti la Mlebe lenye hekari 110 ambalo linamilikiwa na wanakijiji hicho. Alitoa Sh1 milioni ili kuwasaidia wanakijiji hao waongeze miti katika shamba hilo.

Lowassa, pia aliweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Mnase inayojengwa kwa nguvu za wananchi na kuchangia Sh5 milioni kuendeleza ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi sasa madarasa matatu yameshajengwa.

Lowassa pia aliwataka wanakijiji hao kuachana na kilimo cha jembe la mkono na badala yake watumie jembe la kukokotwa na ng’ombe, ili waweze kujiongezea mazao na kupambana na umasikini.

Kutokana na hali ya hewa ya Mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu, aliwashauri wakulima kulima kwa wingi mazao ya mtama na uwele na kwamba serikali itawasaidia mbegu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.