Na Salma Said, Zanzibar
WAFANYABISHARA wa Kitanzania 15 wanashikiliwa na polisi nchini Msumbiji kwa siku tano sasa bila ya kufikishwa mahakamani.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Msumbiji mmoja wa wafanyabishara, Abdallah Seif Abdallah (34), amelieleza Mwananchi Jumapili kwamba ni siku ya tano tangu wawekwe chini ya ulinzi wa polisi wa nchi hiyo bila ya kujua sababu za kukamatwa kwao.
“Kinachotushangaza tumekamatwa bila ya sababu zinazofahamika," alisema mfanyabishara huyo na kuongeza, " mapaka sasa hatujui tutaachiwa lini”
Wafanyabiashara hao hufanya biashara za nguo, simu na vifaa vyake, vitanda na sofa set.
Mbali ya Watanzania hao 15, alisema kunaweza kuwa na idadi nyingine waliokamatwa maeneo mengine ya nchi hiyo kutokana na zoezi linalofanyika nchi nzima.
Alisema kwamba walikamatwa wakiwa ndani ya duka lao eneo la Mawingwe na wengine kufuatwa nyumbani walipofikia eneo la Kitekete na kutakiwa kutoa hati za kusafiria.
Alisema licha ya kutoa hati za kusafiria polisi hao waliwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi hivyo wanashindwa kuendelea na shughuli zao za biashara.
Seif alisema wamejaribu kuwasiliana na Balozi wa Tanzania aliyepo Msumbiji kwa njia ya simu, Issa Mohammed, lakini wameshindwa kupata usaidizi kutokana na Balozi huyo kuwaeleza kuwa yeye ni mgonjwa na amefanyiwa upasuaji.
“Tumejaribu kumpigia Balozi wetu, Issa Mohammed lakini ametujibu kuwa yeye anaumwa na amefanyiwa operesheni kwa hivyo hatujui tufanye nini,” alilalamika.
Hata hivyo wafanyabishara hao wameiomba serikali na taasisi zinazohusika ziingilie kati suala hilo ili wajue kama kuna kosa na endapo hakuna kosa juu yao basi wapewe ruhusa ya kurudi nyumbani kwa vile ni muda wa siku tano sasa wako mikononi mwa polisi.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Ali Mohammed (30), Abdallah Juma (23), Mohammed Rashid (32), KhatibYussuf (23), Soud Mpingo (24), Ali Othaman (29), Ramadhan Magirisi (32), Yussuf Khatib (25).
Seif alisema baadhi ya wafanyabishara wenziwe hawajui wako wapi na wao hawajui kama watakaa hapo kwa muda gani hivyo waliiomba serikali kuingilia na kuwapatia ufumbuzi.
“Hatujui tutawekwa mpaka lini na hapa tunapata taabu kwa sababu tumekaa hatufunguliwi kesi wala hatujui kosa letu nini? Hapa tulipo polisi wametushikilia mabunduki mbele wapo na nyuma yetu wapo kama ungelikuwa na simu yenye kuonesha ungewaona walivyokamata bunduki” amesema Seif