*Asema Iddi Simba aliweka pamba masikioni
*Adai viongozi wengi nchini hawapendi kusoma
*Na kwamba wanaozomea wabunge ni wahuni
*Aunga mkono Kikwete kubadilisha mawaziri
Na Juma Pinto, London
MBUNGE wa Kwela (CCM), Bw. Chrisant Mzindakaya
amesema aliamua kutoa bomu la kashfa ya sukari
mwaka 2001 kutokana na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Idd Simba kuweka pamba masikioni.
Bw. Mzindakaya ambaye aliongoza ujumbe wa wabunge wenzake wanane waliofanya ziara ya kutembelea Bunge la Uingereza House of Commons na la Uskochi la House of Lords, alisema hayo katika mahojiano maalum na kipindi cha TV cha Tanzania Vision kinachorushwa hapa Uingereza katika chaneli ya Sky 183 na kufanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi.
Mbali na Bw. Mzindakaya ambaye alikuwa mkuu wa msafara, wabunge wengine waliokuwa kwenye msafara huo ni Bw. Khalifa Khalifa, Bi Shally Raymond, Bw. John Shibuda, Bw. William Ngeleja, Bibi Amina Chifupa Mkapakanjia, Bi Aziza Ally, Bw. Chacha Wangwe na Katibu wa msafara, Bi Justina Shauri.
Mbunge huyo mkongwe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayefikisha miaka 40 ya kuwa bungeni mwishoni mwa mwezi ujao, alisema aliweka mambo hadharani ya kashfa ya sukari kutokana na Waziri aliyehusika kutokubali makosa.
Mbali na kuwa mbunge kwa miaka 40, Dkt. Mzindakaya aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa kwa miaka 13 na Naibu Waziri kwa
miaka tisa. Alisema mara nyingi makosa makubwa yalifanywa kwa waliopewa nafasi ya kukosoa na si kwa wanaokosolewa.
Alisema mtu yeyote mwenye heshima na anayejua anachokifanya, hatasita kusema ukweli wa jambo ambalo
ana uhakika nalo na analolifahamu na wanaohusika japo watanuna kwa kusema ukweli, basi itakuwa kwa muda tu.
“Mara nyingi mimi nilivyojifunza kwa Tanzania, demokrasia ni kubwa na nimeona kwa marais wote watatu hadi wa sasa, Jakaya Kikwete, wanatafuta watu wa kuwasaidia kwa kukosoa mambo, lakini kwa njia ya kusaidia kujenga na si kubomoa, kwa maana ya majungu,” alisema Dkt. Mzindakaya.
Mbunge huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa kwa kuibua kashfa hiyo ya sukari mwaka 2001, alisema kuna kuibua makosa makubwa ya kiutendaji katika Serikali na anaamini kabisa, mbunge yeyote au mwananchi akiwa na ushahidi wa jambo na kuliibua, basi nchi na Rais watamshukuru.
Alisema anapotaka kuibua jambo, kwanza lazima alifanyie utafiti, lakini pia kabla ya kufanya lolote na mhusika, anapaswa kuambiwa kwamba hili jambo linavyofanyika sivyo, lakini itatokea anayehusika kushindwa kuelewa na kuleta ubishi, ndipo suala litakapotoka hadharani.
Dkt. Mzindakaya alisema katika suala hilo, kama Waziri wa Viwanda na Biashara aliyehusika kipindi kile angeelewa, lile jambo lisingetoka hadharani, kwani kabla ya kutolewa kashfa ile hadharani, Waziri aliandikiwa barua, aliambiwa, lakini aliendelea na msimamo wake wa kushikilia kosa lake.
Aliendelea kusema jambo kubwa ni kukosoana na kurekebishana ndani kabla ya kutoa jambo hadharani tena ikitiliwa maanani wote ni wa chama kimoja , lakini kufikiwa kwa hatua hiyo, kulitokana na mhusika (Waziri) 'kutokuwa na masikio'.
“Unamwambia mhusika, hivi sivyo, lakini ingekuwa hivi ndivyo, lakini yeye anashikilia msimamo wake, basi ndipo unapoamua kuweka mambo hadharani ili umma uweze kuelewa,” alisema.
Sakata hilo la sukari liliingia bungeni, Dkt. Mzindakaya akaja na hoja binafsi dhidi ya Bw. Simba. Akatoa taarifa kuhusu kile alichokiona kuwa ni kashfa kwa waziri huyo, Serikali na hata CCM.
Aliweka shinikizo la kutaka Bw. Simba, kwanza ajiuzulu nafasi yake ya uwaziri, na pili aliombe radhi Bunge kwa kulidanganya wakati alipokuwa akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara yake, alipolitafunatafuna suala zima kuhusu sakata ya sukari.
Awali Bw. Simba alilieleza Bunge bayana, kwamba hatajiuzulu kwani hakuona kama katenda kosa lolote. Kauli yake haikuweza kumwokoa na wala haikuweza kukiokoa chama chake. Upinzani mkali ukaendelea ndani ya CCM na nje, wakimtaka ajiuzulu.
Miezi mitatu baada ya kuendelea kwa shinikizo, hatimaye Bw. Simba akaamua kujiuzulu uwaziri, akisema bayana kwamba amelazimika kuchukua uamuzi huo kwa ajili ya kuinusuru Serikali yake kusambaratika na chama chake kustawi.
Kiongozi huyo wa msafara wa wabunge waliokaa hapa Uingereza kwa wiki moja na kurejea Tanzania Jumatatu wiki hii, alisema hayo kutokana na swali aliloulizwa kuwa kwa nini suala hilo halikuzungumzwa ndani ya vikao vya Bunge kabla ya kulitoa nje kwa kuwa iliyekoselewa ni wizara ya Serikali inayoongozwa na CCM na yeye (Mzindakaya) akiwa mwanachama wake.
Ziara ya wabunge hao ni kati ya ziara ambazo Spika wa Bunge la Tanzania, Bw. Samuel Sitta aliamua kuziandaa kwa lengo la wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea mabunge mbalimbali duniani, kujifunza jinsi wenzao wanavyoendesha mabunge yao.
Akizungumzia tofauti iliyopo sasa na ya miaka 40 iliyopita ndani ya Bunge la Tanzania, Dkt. Mzindakaya alisema kipindi cha sasa wasomi ni wengi na kiwango cha uelewa kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, hali inayofanya wao, wazee, kuzidi kujifunza na kujiendeleza ili kwenda na wakati.
“Watanzania hatupendi kujiendeleza kwa kusoma na hili mtu akishapata digrii yake na cheo, basi hawapendi kujiendeleza tena wanaona ndio wamemaliza na hii ndiyo kasoro kubwa sana,” alisema.
Alisema hata baadhi ya viongozi wa Serikali, wamekuwa na kasumba hiyo, lakini pamoja na uzee alionao bado anapenda kusoma na kujifunza na hata akisafiri, anasema amekuwa akinunua vitabu vya kusoma na kujifunza, "lakini wengine watarudi na masanduku matatu ya nguo".
Mkongwe huyo alisema mtu mwenye kuhitaji maendeleo na kujua mambo yanavyokwenda kwa wakati katika dunia ya sasa ni lazima asome, kwani inahitaji wasomi ili kujua mambo mengi, "bila kusoma hakuna jipya utakaloweza kujua".
Kuhusu suala la wafanyabishara mbalimbali na watu wenye uwezo kifedha Tanzania kuingia katika ulingo wa siasa na hasa katika nafasi za ubunge, Dkt. Mzindakaya alisema wao ndani ya CCM wameliona hilo na wanalifanyia kazi.
“Rais ameliona hili, hivyo katika vikao vyetu vya ndani ya chama tunajitahidi kuangalia utaratibu mzuri wa kupata wabunge ili kuondokana na hali hiyo ya watu kutumia fedha kupata vyeo,” alisema Dkt. Mzindakaya.
Akizungumzia tabia ya baadhi ya wananchi kuzomea wabunge wao, pindi wanapotambulishwa kwa Rais au Waziri Mkuu katika mikutano ya hadhara kwenye majimbo yao, Dkt. Mzindakaya alisema kuzomea kiongozi si tabia ya Watanzania, ni mambo ya kihuni.
Alisema hatua hiyo ilikuwa ikitokea mwaka jana, kutokana na makundi mbalimbali ya kampeni kupandikiza baadhi ya watu na hiyo inawezekana wanaofanya mambo hayo ni wanachama wenzao kutoka ndani ya CCM.
Mbunge huyo mkongwe, alisema tatizo lingine linalosababisha hatua hiyo ni kura za maoni ndani ya chama, ambapo mgombea aliyeshindwa kwenye kura hizo anakuwa na kundi lake, lililokuwa naye pamoja, hivyo kutoa dukuduku lao moyoni kwa kuzomea katika mikutano ya hadhara.
“Ni kazi ya chama kuhakikisha kwamba tunarudisha umoja na kuvunja makundi mara baada ya kura za maoni, kwa kufanya hivyo, tutaleta umoja na ushirikiano mzuri na si kubakisha makundi na kuanza kuzomea, hali ambayo si utamaduni wetu Watanzania,” alisema.
Kuhusu mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni kwa mawaziri kuhamishwa wizara, Dkt. Mzindakaya alisema Rais Kikwete alitumia busara kubwa kwa mawaziri wahusika kuhamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine.
“Ni jukumu la waziri aliyehamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine kujiuliza kwa nini amehamishwa katika wizara yake na kujiuliza kama amepelekwa pale kwa mazuri au kwa kupewa onyo la kazi,” alisema.
Alisema yawezekana Rais alitoa uhamisho huo kwa kuona fulani nikimpeleka wizara hii anaweza kuwa muhimu zaidi kuliko pale alipokuwa mwanzo na mwingine anaweza kupelekwa wizara nyingine kwa onyo tu, vyote vinawezekana.
“ Rais hafanyi kosa kumpa mtu madaraka, anayekosa ni yule aliyepewa jukumu na kushindwa kutekeza majukumu yake, hivyo kwa Rais kufanya mabadiliko ni vitu vya kawaida katika kutafuta ufanisi wa shughuli za Serikali.
Kuhusu mafanikio ya ziara yao katika mabunge hayo, Dkt. Mzindakaya alisema wamejifunza mengi sana na kubwa zaidi waliloliona ni kwamba mabunge ya nje demokrasia yao imeshika hatamu kubwa zaidi, tofauti na Bunge la Tanzania.
“Hapa tumeona Waziri Mkuu anajibu swali na watu wanaingilia hotuba yake, sasa kwetu hatujafikia hatua hiyo kwani bado tuna heshima kubwa, lakini yote kuna mambo mengine tumejifunza na tutayapeleka kwa wenzetu,” alisema Dkt. Mzindakaya.
Alisema mtu kusoma si kukaa darasani tu, lakini hata safari ambazo wabunge sasa wameanza kwenda kutembelea sehemu mbalimbali duniani ni somo tosha, "hivyo tumejifunza mengi na tunatarajia kuwapelekea wenzetu kile ambacho tumenufaika nacho na kukifanyia kazi".
Kuhusu matarajio yake baada ya miaka mitano ijayo, iwapo atagombea ubunge katika jimbo lake, Dkt. Mzindakaya alisema atatoa msimamo wake muda ukifika, kwani ana mawazo yake ambayo anayafikiria