KAMPUNI ya simu za mkononi ya Celtel Tanzania imetoa zaidi ya vitabu 1,600 kwa shule 16 za sekondari za Pemba, Unguja, Lindi na Mtwara.
Hayo yameelezwa na Meneja Mauzo wa Celtel Tanzania, Deogratius Kwiyukwa katika hafla maalum ya kukabidhi msaada wa vitabu kwa shule nne za sekondari za Lindi na Mtwara.
Katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani Lindi hivi karibuni, jumla ya shule nne za sekondari za mikoa ya Lindi na Mtwara zilikabidhiwa zaidi ya vitabu 400 kupitia mradi wa Celtel wa ‘Build our Nation’.
Meneja Mauzo wa Celtel alifafanua kuwa mbali na shule nne za Lindi na Mtwara, pia Celtel imetoa vitabu kwa shule 12 za visiwani Zanzibar ambapo kila shule imepata zaidi ya vitabu 100 vyenye thamani ya sh. milioni moja.
“Katika kipindi kisichozidi wiki mbili, Celtel imetoa zaidi ya nakala 1,600 za vitabu kwa shule 16 za sekondari za visiwani Zanzibar (Pemba na Unguja) na za bara (Mtwara na Lindi),’’ alifafanua Kwiyukwa.
Alieleza kwamba Celtel itaendelea kusaidia shule za sekondari kote nchini kwenye mikoa yote 26 Tanzania bara na mitano ya Tanzania visiwani kupitia mradi wake wa ‘Build Our Nation’.
Kwa upande mwingine, wakizungumza muda mfupi mara baada ya kupokea msaada huo wa vitabu kutoka Celtel wakuu wa shule zilizonufaika na vitabu wameishukuru Celtel kwa kuwakumbuka na kutoa mchango muhimu katika sekta ya elimu.
“Kwa hakika tumekuwa tukikabiliwa na uhaba mkubwa wa vitabu suala ambalo limekwamisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kitaaluma katika shule zetu,” alisema Hamisi Sakilu, Mkuu wa Shule ya Sekondari Chaume.
Naye Mkuu wa mkoa wa Lindi, Said Sadiki alisema kuwa wanauchukulia msaada huo kwa uzito mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa kitabu kimoja kinaweza kutumiwa na wanafunzi wengi na kwa muda wa miaka mingi na hivyo kuwa na manufaa makubwa kwa jamii nzima.
Mradi wa ‘Build Our Nation’ ulizinduliwa rasmi Mei 2004 na umegawanywa katika awamu nne kwa mwaka, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi huipa Celtel orodha ya shule zenye uhaba mkubwa wa vitabu nchini na kisha shule moja huchaguliwa kutoka kila mkoa katika kila awamu ya mradi na kupatiwa msaada wa vitabu wenye thamani ya sh. milioni moja.
Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19322
Na Mwandishi Wetu