Na Mwandishi Wetu, Mwanza
HOSPITALI ya Rufaa ya Bugando, inakabiliwa na upungufu madaktari bingwa 32, hali inayosababisha daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 100,000.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Stephen Kebwe, katika sherehe za Chuo Kikuu Kishiriki cha Bugando, zilizofanyika chuoni hapo.
Alisema Hospitali hiyo ina madaktari bingwa 18 tu kati ya madaktari bingwa 50 wanaoitajika na hivyo kulazimisha daktari mmoja kutoa huduma kwa wagonjwa 100,000.
Aliongeza kuwa madaktari hao hutoa huduma kwa wagonjwa hao wengi kutokana na hospitali hiyo kupokea idadi kubwa ya wagonjwa.
"Hospitali yetu inahudumia wagonjwa zaidi ya milioni 13 kwa mwaka hivyo madaktari bingwa hujikuta wakitoa huduma kwa wagonjwa zaidi 100,000 idadi ambayo ni kubwa," alisema Dk Kebwe na kuongeza kuwa idadi hiyo inazidi hata ule wastani wa daktari mmoja wa Kitanzania kuhudumia wastani wa wagonjwa 25,000 kwa mwaka.
Alisema kutokana na hali hiyo, jitihada kubwa zinatakuwa zichukuliwe na wadau wa afya kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuwapata madaktari bingwa wengi zaidi watakaosaidia kulikabili tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Bugando (Buchs), Askofu Aloysius Balina, alisema chuo hicho kinatarajia kuanzisha kozi za uzamili za udaktari, ikiwa ni moja ya njia ya kukabiliana na upungufu wa madaktari bingwa nchini.
Alisema mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwezi huu kwa ushirikiano na Chuo na Hospitali ya Bugando (BMC).