Na Angella Milinga (RCT)
BODI ya Biashara ya Nje (BET) imeanza mkakati wa kuhamasisha Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa ndani ili kuinua uchumi wa taifa.
Katika mkakati huo, BET inakusudia kutumia Tamasha la Uhuru litakalofanyika Desemba 2 hadi 23, mwaka huu katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, kuimarisha kampeni hiyo ya nunua bidhaa za Tanzania jenga Tanzania.
Wakati wa tamasha kila mkoa, wilaya, wizara, mashirika ya umma, mashirika binafsi, taasisi zisizo za serikali na mtu mmoja mmoja watakuwa na fursa ya kuonyesha mafanikio yao na bidhaa walizozalisha ili kuhamasisha Watanzania kuzipenda.
Kaimu Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Halmashuri ya Biashara ya Nje(BET), Edwini Rutegerukwa alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake.
''Tumehamasisha washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani, wafanyabiashara wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi, kushiriki katika tamasha hilo ili kufahamiana, kuweka mtandao wa pamoja wa ushirikiano na kuwezesha kujenga soko la ndani na kuhamasisha ununuzi wa bidhaa za Tanzania," alisema.
Rutegerukwa alisema shughuli za uuzaji na ununuzi zitachukua nafasi kubwa katika maonyesho hayo.
Alisema tamasha limeazimia kushirikisha taasisi zote zinazojikita katika kupunguza umaskini kwa kinamama, vijana na wasiojiweza chini ya SIDO, TAWOMA, HOT, TANCRAFT na makampuni mengine mengi.
Rutegeruka aliongeza kuwa BET inawaomba wadau wote kutoka sekta mbalimbali za uchumi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kuunga mkono tamasha hilo kwa kushiriki kuchangia ufanikishaji.
Akitoa ufafanuzi alisema Nchi ya Kenya, Uganda na Misri watashiriki katika tamasha hilo na kiingilio chake ni Sh1500 kwa watu wa zima na Sh500 kwa watoto wadogo