Na Mwandishi Wetu, Dodoma SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inatoka kwenye kundi la nchi masikini sana duniani kwa kuboresha sekta zote muhimu.
Sekta zinazotarajiwa kuboreshwa ni kilimo, miundombinu, elimu, afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mitaji yenye riba nafuu na kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Batilda Burian, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Abdallah Njwayo,
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani kufuta aibu ya Tanzania kuitwa nchi masikini sana duniani.
Alisema tathmini ya hivi karibuni inaonyesha kuwa Tanzania itafikia viwango vya malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, inatekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (Mkukuta) na kwa Zanzibar (Mkuza).
Lengo kuu la mkakati huo ni kuondoa umasikini ili kufikia malengo ya muda mrefu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020.
Hata hivyo, Burian alisema serikali pekee haiwezi kufanikiwa katika vita ya kupambana na umasikini ila jitihada hizo zinahitaki kuungwa mkono na wananchi wote, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni binafsi, taasisi na asasi mbalimbali.
Akielezea sababu za umasikini wa Tanzania, Naibu Waziri huyo, alisema sababu za ndani ni kutokuwepo kwa mitaji ya kutosha kuwekeza katika miundombinu, teknolojia duni ya uzalishaji,
Nyingine alisema ni utoaji huduma, uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula na biashara na viwango vidogo vya elimu katika fani mbalimbali.
Waziri alitaja sababu nyingine ni idadi kubwa ya wategemezi katika kaya, kukithiri kwa tabia ya uzembe na uvivu, urasimu usio wa lazima katika asasi za umma na binafsi na athari zitokanazo na maradhina majanga mbalimbali.
Sababu za nje alizitaja kuwa ni deni la taifa ambalo ni kubwa na linatumia rasilimali nyingi ili kulilipa, kupanda kwa bei ya mafuta na bei duni kwa bidhaa ghafi za Tanzania zinazouza nje hivyo kusababisha urari mbaya katika biashara ya kimataifa.