Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sarakasi ubunge wa Afrika Mashariki
Sarakasi ubunge wa Afrika Mashariki
By Habari Tanzania | Published  11/4/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Alfred Lucas na Martha Mtangoo, Dodoma

MATOKEO ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, yalitangazwa jana mjini hapa, huku baadhi ya wasomi maarufu na wabunge katika Bunge lililomaliza muda wake, wakitupwa nje.

Mmoja wa walioonja shubiri ya siasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, Profesa Samwel Wangwe.

Mpinzani wa muda mrefu wa sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyeamua kurejea katika chama hicho miezi miwili iliyopita, Dk. Amani Kabourou, amekuwa miongoni mwa washindi.

Pamoja na Dk. Kabourou, wengine walioshinda ni Dk. Didas Massaburi aliyepata kura 157; na Dk. George Nangale (132).

Mbunge aliyemaliza muda wake katika Bunge la Afrika Mashariki, Dk. Norman Sigalla, alipata kura 126 na hivyo kutupwa nje.

Wagombea wengine walioshindwa katika kundi hilo na kura zao kwenye mabano ni Gooduck ole-Medeye (51), Evod Mmanda (9), Dk. Richard Kasungu (21) na Dk. Handley Mafwenga (27).

Kwa upande wa wanaume kutoka Zanzibar, walioshinda ni Dk. Abdallah Hassan Mwinyi aliyepata kura 166; na Dk. Said Gharib Bilal aliyepata kura 126.

Kundi la tatu la wanawake lilikuwa na nafasi tatu, kati ya hizo, moja ilikuwa ya Zanzibar. Washindi ni Sebtuu Mohammed Nassor (135), Kate Kamba (117) na Janet Mmari aliyepata kura 126.

Katika kundi la wapinzani lilikuwa na nafasi moja. Aliyeshinda ni Dk. Fortunatus Masha wa UDP, aliyepata kura 202 na kuwazidi wapinzani wenzake, akiwamo Profesa Mwesiga Baregu (CHADEMA) aliyeambulia kura 30.

Mara baada ya kutangazwa, Spika wa Bunge aliwapongeza Dk. Masha wa UDP aliyeshinda kwa upande wa upinzani akisema kwamba alisoma naye Tabora na kwamba kwa sasa watashirikiana vema.

Baada ya matokeo hayo, ukumbi ulilipuka kwa shangwe na vigelegele, lakini aliyeonekana kuwa na furaha zaidi ni mke wa Dk. Masaburi, Janet, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).

Bunge la Afrika Mashariki linaundwa na wabunge tisa kutoka kila nchi, kati ya nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Kwa upande wa Tanzania kulikuwa na majina 30 ya wagombea ubunge wa Afrika Mashariki, na yaligawanywa katika makundi manne.

Kundi la kwanza ni la wanawake ambalo lilitakiwa kutoa wabunge watatu. Wawili walitakiwa watoke Tanzania Bara, ilhali mmoja atoke Zanzibar.

Walioshiriki kinyang’anyiro hicho ni Mahfoudha Hamid, Sebtuu Nassor, Janet Mmari, Janeth Mbene, Hulda Kibacha, Dk. Tereza Huvisa, Kate Kamba, na Dk. Rose Maeda.

Kundi la pili ni la wabunge kutoka Zanzibar. Kundi hilo lilitakiwa litoe wabunge wawili.

Walioshiriki kinyang’anyiro hicho ni Remidius Kissasi, Profesa Said Gharib Bilal, Issack Sepetu, Abdallah Ali Hassan Mwinyi, Dk. Makame Ali Usi, na Nassor Juma Mugheir.

Kundi la tatu ni la wanachama kutoka kambi ya upinzani. Kundi hilo lilitakiwa litoe nafasi moja tu.

Waliowania kutoka kundi hilo ni Profesa Baregu (CHADEMA), Victoria Mwanjisi (TLP), Jesse Makundi (TLP), Mutamwega Mgaywa (TLP), na Dk. Masha (UDP).

Kundi la nne lilikuwa ni la wagombea kutoka Tanzania Bara. Hili ndilo kundi lililokuwa gumu zaidi, kuliko makundi mengine. Kundi hili lilitakiwa litoe wabunge watatu.

Walioshiriki ni Dk. Masaburi, Evod Mmanda, Dk. George Nangale, Profesa Wangwe, Dk. Sigalla, Richard Kasungu, Dk. Kabourou, na Dk. Handley Mafwenga.

Wabunge waliokuwa kwenye Bunge lililomaliza muda wake ni Mahfoudha, Kibacha, Kamba, Dk. Nangalle na Dk. Sigalla.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.