Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha wenye Mabasi ya Mikoani nchini (TABOA), Mohamed Abdullah, amewataka wadau wa usafirishaji wa barabarani kutoa ushirikiano kwa mkakati uliotangazwa na Polisi katika kupunguza ajali za barabarani.
Abdullah alisema jana kuwa ni wakati mwafaka kwa watumiaji wa barabara kuwa na utamaduni wa kutumia barabara kwa kuzingatia misingi ya sheria zote za barabarani.
Pia alishauri wadau wa barabara wachukue utaratibu katika kuepukana na athari zinazoendana na ubovu wa barabara.
“Kwa kutumia nafasi yangu kama mwenyekiti wa TABOA, nitoe pongezi za dhati kwa serikali kwa kuunda chombo cha kudhibiti uendeshaji mbovu na wa kizembe barabarani,” alisema Abdullah, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya mabasi ya Scandinavia Express.
Aliongeza kuwa TABOA inaahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa chombo hicho.
Mwishoni mwa wiki Mkuu wa Jeshi la Polisi , Inspekta Jenerali Saidi Mwema, alisema mkakati wa Polisi kwa sasa unaendana na kuwashirikisha wadau kama Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Barabarani (SUMATRA) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Mwema alitaja baadhi ya mikakati kuwa ni kutumia askari kanzu na kukamata wanaofanya makosa barabarani na kuwawajibisha askari na makamanda wa ngazi mbalimbali, wakiwemo wa mikoa, ambao wanahusika moja kwa moja na kukithiri kwa ajali katika maeneo yao.
Timu ya Polisi, kwa kushirikiana na wadau wengine wa usalama barabarani, ilifanya utafiti kwa miezi tisa na kupata picha halisi ya hali ya usalama barabarani, ambayo Mwema alisema inaonyesha hali ni mbaya.
Pia Mwema, alisema suala la usalama barabarani sasa hivi ndilo linafuatiliwa kwa karibu kutokana na kusababisha vifo na madhara mengi, baada ya kupatikana mafanikio kwa upande wa ujambazi wa kutumia silaha.