Washangaa baada ya kufika benki
Na Shomi Mtaki, Mbozi
WATUMISHI wa idara kadhaa za serikali wamelalamika kukatwa sh. 5,000 kila mmoja kwenye mshahara bila ridhaa yao, kwa kilichoelezwa kwamba ni kuchangia Mfuko wa Tiba ya Kansa ya matiti.
Kilio hicho kimetolewa na watumishi wa idara za elimu, afya na utawala kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, kufuatia kukata kila mtumishi sh 5,000 kutoka katika mishahara yao bila kuwashirikisha, ili kuchangia mfuko huo.
Watumishi hao waliwaambia waandishi wa habari jana mjini Vwawa kuwa kitendo kilichofanywa na uongozi huo ni kinyume na taratibu kwani walitakiwa kushirikishwa kabla ya kuwakata fedha hizo.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake, Benjamin Matiti alisema walishtushwa na taarifa ya meneja wa benki ya NMB, tawi la Mbozi, kuwa ucheleweshwaji wa mishahara yao uliotokea mwezi uliopita unatokana na kuwepo makato katika mishahara, hivyo alihitaji ufafanuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Levenson Chilewa, kabla ya kuwalipa.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo walilazimika kuandamana hadi ofisi ya mkurugenzi ambaye katika kikao cha pamoja na watumishi, wengi wao wakiwa walimu, mkurugenzi aliwaeleza kuwa uamuzi wa kuwakata mishahara ulifikiwa kwa pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi vilivyopo wilayani Mbozi.
Matiti aliongeza kuwa kufuatia majibu ya mkurugenzi walikwenda ofisi ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambako, hata hivyo, hawakumkuta katibu wala mwenyekiti ambao wengetoa maelezo kuhusu makato hayo.Kitendo cha viongozi wa CWT kutokuwepo ofisini kimewajengea hisia kwamba huenda wamejificha ili kukwepa malalamiko ya walimu.
Habari zaidi kuhusiana na tatizo hilo zimeeleza kuwa kabla ya fedha kukatwa, walimu wakuu walipokea barua kutoka Ofisi ya katibu tawala zikieleza kuwa walimu watapaswa kuhamasishwa ili wachangie sh. 2,000 na si kwa kuwakata mishahara.
Walimu na watumishi wanaolalamikia uamuzi wa kukatwa mishahara bila idhini yao ni wa idara za elimu, afya na utawala ambao wanadai wanahofu kulivalia njuga suala hilo kuogopa kuchukuliwa hatua za kulipizwa kisasi na viongozi wao.
Katibu wa CWT wilayani hapa, Victor Mtumbo ambaye alidai yuko safarini, akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa simu, alikana kuhusika na maamuzi hayo na kwamba yeye hakuitwa kwenye kikao kilichotajwa.Hata hivyo alikiri kupokea barua iliyoagiza walimu wahamasishwe ili waweze kuchangia sh 2,000 na si kuwakata kutoka katika mishahara yao.
Mkurugenzi Chilewa, akizungumzia suala hilo, alikanusha vikali madai ya watumishi hao kuwa ametumia nguvu kukata kiasi hicho cha fedha bila kuwashirikisha wahusika.Alisema alikutana hivi karibuni na viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi wilayani ili kujadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha kituo cha uchunguzi wa kansa ya matiti.
Chilewa alisema katika kikao hicho walikubaliana kila mfanyakazi akatwe sh 5,000 kutoka katika mshahara wake ili kuwezesha upatikanaji wa kiasi cha zaidi ya sh. milioni 30 zitakazotumika kuendeshea kituo cha utafiti wa kansa ya matiti.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hii umebaini kuwa baada ya mkurugenzi kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na kupitisha maamuzi hayo, viongozi hao hawakurudi kwa wanachama wao kuwaelimisha juu ya maamuzi waliyopitisha, hali ambayo imezua manung’uniko kwa wafanyakazi kuona kwamba wameonewa.