Yumo Walid Kabourou
Maprofesa wadondoka
Wawili wa zamani warudi
Na Bakari Mnkondo, Dodoma
HATIMAYE Watanzania watakaoiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki wamepatikana katika matokeo ambayo yamerudisha sura mbili tu za zamani huku maprofesa wakikataliwa.
Wabunge wa zamani waliofanikiwa kurudi ni George Nangale na Kate Kamba.
Akitangaza matokeo hayo jana jioni, Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Damian Foka alisema wabunge tisa waliotakiwa wamepatikana.
Foka aliwataja washindi kuwa ni Dk. Didas Massaburi aliyepata kura 137, akifuatiwa na Dk. George Nangale kura katika mabano (132) na Dk. Aman Walid Kabourou (130). Kura zilizopigwa ni 244 na iliyoharibika ni moja.
Matokeo hayo ni kwa kundi la wanaume Tanzania Bara ambalo lilikuwa na wagombea tisa, huku watatu ndio wakiwa wanatakiwa.
Katika kundi la wanawake lililokuwa na wagombea wanane, wakiwa wanatakiwa watatu, walioibuka na ushindi ni Sebtuu Mohammed Nassor (135), Janeth Mmari (126) na Kate Kamba (117). Kura zilizopigwa ni 244 na zilizoharibika ni nne.
Foka aliendelea kuwataja washindi katika kundi la kutoka Zanzibar, lililokuwa linahitaji washindi wawili kuwa ni Abdallah Ali Hassan Mwinyi(166), akifuatiwa na Dk. Said Gharib Bilal (126) kati ya kura zote 244 zilizopigwa.
Kwa kundi la wapinzani, lililokuwa na wagombea watano baada ya wawili wa CUF kujitoa, ambapo alitakiwa mtu mmoja, Dk. Fortunatus Masha alifanikiwa kuibuka kidedea kwa kupata kura 202 kati ya 244 zilizopigwa. Moja iliharibika.
Kura walizopata kwa ambao hawakuibuka washindi ni kama ifuatavyo: kundi A, Mohfoudha Alley Hamid (105), Janeth Mbena (80), Hulda Kibacha (57), Dk. Teleza Huvisa (59) na Dk. Rose Maeda(39).
Katika kundi B la Zanzibar, Remedius Kissasi (75), Isack Sepetu (36), Dk. Makame Ussi (25) na Nassoro Mugheiry (60).
Walioshindwa katika kundi la upinzani ni Victoria Mwanjisi wa TLP (15), Meja Jesse Makundi wa TLP (0), Mutamwega Mgahywa wa TLP (5), Profesa Mwesiga Baregu wa CHEDEMA (30).
Katika kundi hilo, wagombea wawili kutoka CUF, Profesa Abdallah Safari na Mohamad Dedes walijitoa.
Walioshindwa katika kundi D ni Goodluck Ole Medeye (51), Evod Mmanda (9), Profesa Samwel Wangwe (115), Dk. Norman Sigalle (124), Dk. Richard Kassungu (21) na Handley Mafwenga (27).Baada ya matokeo kutangazwa wote walioingia katika kinyang’anyiro hicho waliyakubali matokeo na kusema uchaguzi ulikuwa safi.
Hata hivyo, Profesa Beregu, Mgahywa na Victoria ‘waliingia mitini’ hivyo hawakupata nafasi ya kuelezea uchaguzi huo.