Na Peter Orwa
CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU), kimetangaza kufanya maandamano Novemba 16, mwaka huu, kwenda kumwona Rais Jakaya Kikwete, kumweleza kuhusu dhuluma ya maslahi ya wafanyakazi waendeshaji wa vyuo vikuu vya umma nchini.
Hatua hiyo iliafikiwa jana, katika mkutano matawi yote ya RAAWU mkoa wa Dar es Salaam, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Chang’ombe, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa RAAWU, Aldegunda Mgaya, alisema jana ofisini kwake kuwa chama chake kimeamua kulichukua suala hilo kuwa lake na si la vyuo vikuu tena ili kuongeza msukumo wa madai yao.
Mwezi uliopita, Aldegunda katika tamko alilolitoa kwenye vyombo vya habari, alisema RAAWU ingeitisha maandamano iwapo madai yao yasingeridhiwa hadi jana.
Madai ya watumishi waendeshaji wa vyuo vikuu yanatokana na malalamiko dhidi ya utekelezaji wa ripoti ya Tume ya Tume ya Rais iliyoundwa Septemba mwaka jana iliyoshauri waongezewe mishahara kwa asilimia 100 kwa awamu tofauti.
Utekelezaji ulifanyika kwa wanataaluma kama ilivyopendekezwa, na kwamba wafanyakazi waendeshaji hawakunufaika na utekelezaji wa ripoti ya Tume.
Kutokana na hilo, alisema Aldegunda, wawakilishi wa wafanyakazi waendeshaji walifanya jitihada za kufuatilia madai yao hadi kwenye mamlaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumuona Katibu Mkuu Kiongozi na wakaishia kugonga mwamba.
Aldegunda hakufafanua juu ya idadi ya wanachama watakaoshiriki maandamano,wala mpangilio wa mahali yatakapoanzia na kumalizikia, akitamka tu kuwa “ni jambo litakalojulikana baadaye”.
Nalo Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), katika ripoti yake mkutanoni jana, lilisema litaiunga mkono RAAWU iwapo serikali haitaridhia utekelezaji wa madai yake kabla ya tarehe ya maandamano.
“Endapo serikali itaendelea kulipuuza suala hili, Shirikisho litaunga mkono hatua zozote zitakazochukuliwa na wafanyakazi na chama chao (RAAWU) kwa ajili ya kutetea maslahi yao,” ilisema taarifa ya TUCTA.