Na Furaha Omary
WANAFUNZI wanne wa sekondari wametiwa mbaroni na polisi mjini Dar es Salaam wakituhumiwa kufanya vurugu kwa kuyapiga mawe magari na kuwajeruhi watu wanane.
Polisi iliwakamata wanafunzi hao wa shule ya sekondari ya Azania, Dar es Salaam, kufuatia kupandwa na hasira na kuanzisha vurugu kwa kurushia magari mawe na kujeruhi watu kutokana na kifo cha mwenzao aliyefariki kwa kukanyagwa na daladala Jumatatu.
Kamishna wa msaidizi wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Abdallah Mssika, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Fred Daima (17) wa kidato cha pili mkazi wa Kurasini, Rashid Ramadhani (15), kidato cha kwanza mkazi wa Buguruni Moto, Kondo Mrisho (19) kidato cha tatu mkazi wa Tabata Kisukuru na Deus John (17) wa kidato cha tatu, mkazi wa Kitunda.
Mssika alisema juzi saa 8 mchana wanafunzi walikwenda kuaga mwili wa mwanafunzi mwenzao, James David (15), wa kidato cha kwanza, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
David alifariki Jumatatu, saa moja asubuhi eneo la Buza, Kitunda baada ya kukanyagwa na basi la daladala, Leyland Daf namba za usajili T969 AGA, likiendeshwa na Salum Mshamu, wakati akienda shule.
Mshamu ameshafikishwa mahakamani kwa mashitaka ya uendeshaji mbaya na kusababisha kifo cha David.
Mssika alisema baada ya kuuaga mwili wa mwenzao wanafunzi walijigawa katika makundi, huku wengine wakiwa na mabango na kupita maeneo ya Faya, Mnazimmoja na Akiba, wakitupia mawe daladala kwa madai wanalipa kisasi kufuatia kifo cha mwenzao.
Alisema katika vurugu hizo daladala 19 ziliharibiwa kwa kuvunjwa vioo na abiria wanane waliokuwamo walijeruhiwa, ambapo walitibiwa na kuruhusiwa.
Majeruhi walitajwa kuwa ni makondakta Mkama Ismail (25), Ibrahim Msangazi (30), Hamis Said (33), Shomari Said (20), mwanafunzi Peter Bulima (10), Yohana Bundana (15), Said Ally (42) na Hassan Mohamed (22).
Mssika alisema wanafunzi hao baada ya kukamatwa walihojiwa ili wawataje viongozi wa vurugu hizo, lakini walikataa na polisi imeamua kuwakabidhi kwa Mwalimu wao Mkuu Msaidizi, Elinazi Mkongo, ili awachukulie hatua za kisheria.
Polisi pia inawashikilia watu watano, wakiwemo wawili waliotoka jela mwezi uliopita, wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wakiwa na silaha na risasi katika matukio tofauti.
Mssika alisema polisi juzi iliwakamata watu hao, ambao walishatumikia kifungo gerezani, wakiwa na bastola wakijiandaa kufanya tukio la ujambazi.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa Kimamba, wilaya ya Kinondoni, wakiwa na bastola yenye namba 358393 aina ya Walther ikiwa na risasi tano kuwa ni Chacha Mwita (33) na Paul Mbusilo (31).
Mssika alisema baada ya kuhojiwa watuhumiwa walieleza kuwa hawamiliki bastola hiyo kihalali ambapo mtuhumiwa Mwita alidai ni ya marehemu kaka yake ambaye alikufa katika tukio la ujambazi mwaka 2002, Mwananyamala Kinondoni.
Watuhumiwa, kwa mujibu wa Mssika, walikiri kutoka gerezani, Mwita akiwa ametoka Oktoba 6 mwaka huu. Alikuwa amefungwa kwa makosa ya mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha. Kamanda amesema polisi itafuatilia kujua sababu za kutolewa gerezani. Mbuliso alitoka Septemba 14, mwaka huu.
Watuhumiwa wengine walikamatwa juzi eneo la Mianzini, Mburahati, wakiwa na ‘shotgun’ ambayo imekatwa kitako na kupunguzwa mtutu, ikiwa na risasi 10. Hao ni Salehe Hamza (36), Andrew Mwambenja (26) na Kajuna Kente (29) .
Mssika alisema baada ya kufuatilia Makao Makuu ya Upelelezi, ilibainika kuwa ‘shotgun’ hiyo inamilikiwa kihalali na Marco Mdeha, mkazi wa Kijiji cha Mpaduka, Kata ya Imeji Mazombe, Iringa, lakini hakuna taarifa za kupotea kwa silaha hiyo. Polisi inaendelea na uchunguzi.