Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Kikao cha tano cha Bunge la Jamhuri, Wabunge wamepeleka mawazo ya nani Bungeni?
http://www.habaritanzania.com/articles/1631/1/Kikao-cha-tano-cha-Bunge-la-Jamhuri,-Wabunge-wamepeleka-mawazo-ya-nani-Bungeni?
By Prosper Kwigize
Published on 10/31/2006
 
Wakati Tanzania ikigubikwa na masuala makuu matatu ambayo yamekuwa yakiwatoa jasho viongozi, yaani elimu, kilimo na afya yaliyopewa jina moja la mpango wa EKA kwa kifupi, bila kusahau utata wa masuala ya umeme, mikataba ya madini na mzozo wa ziwa Victoria na umasikini wa watanzania ulioibua filamu ya mapanki (darwin’s Night mare) viongozi, hususani wawakilishi wa wananchi katika vyombo vya maamuzi bado hawajajua lipi la kufanya na wapi lifanyike

Wakati Tanzania ikigubikwa na masuala makuu matatu ambayo yamekuwa yakiwatoa jasho viongozi, yaani elimu, kilimo na afya yaliyopewa jina moja la mpango wa EKA kwa kifupi, bila kusahau utata wa masuala ya umeme, mikataba ya madini na mzozo wa ziwa Victoria na umasikini wa watanzania ulioibua filamu ya mapanki (darwin’s Night mare) viongozi, hususani wawakilishi wa wananchi katika vyombo vya maamuzi bado hawajajua lipi la kufanya na wapi lifanyike.
 
Wiki hii kikao cha tano cha bunge kimeanza mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine watajadili miswada sita ya sheria, Mkutano huo pia utachagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na kuridhia mikataba sita ya kimataifa na kujibu maswali 201 ya wabunge.
 
Hoja hapa ni je hawa wabunge ambao waliaminiwa na wananchi walioacha shughuli zao zote jumatano ya desemba 14 mwaka 2005 na kwenda kupanga foreni kuwapigia kura waliowapenda kupitia katika uchaguzi wa siri, wamepeleka nini bungeni?
 
Mimi kwa uchunguzi wangu baadhi ya wabunge hata hawakuwahi kufanya ziara rasimi katika majimbo yao tangu kikao cha nne cha bunge kilichomalizika mwishoni mwa mwezi wa nane, na isitoshe wengine tangu wachaguliwe hawajaenda kuwashukuru wananchi waliowahangaikia na kuwapatia nafasi hiyo adimu ya ubunge.
 
Wakati wabunge wanawaza namna ya kukaa Dodoma, kupokea propaganda za hapa na pale za wagombea wa ubunge wa afrika mashariki, hivi ni waanchi wangapi hata hawajui wala kuelewa lolote juu ya kwanini wawepo wabunge hao? Naamini wapo wengi ambao hata wanatamani kusema hakuna sababu ya kuwa nao kwani faida zao hazirudi chini kwa wananchi wanaounda jumuiya hiyo.
 
Hoja nyingine hapa ni je hawa wabunge ambao wanakimbia Dodoma wakitokea Dar es salaam badala ya kutokea Majimboni mwao ambapo mheshimiwa sana Rais Jakaya Kikwete aliagiza waende kuishi na wananchi wanajua nini juu ya wananchi na majimbo yao?
Kama wengine hata kushukuru wapiga kura waliishia kata mbili tatu tu huku baadhi ya maeneo wakiyaruka wanaenda kuuliza nini bungeni katika maswali hayo 201 ambayo yataulizwa bungeni katika kikao hicho cha tano tangu serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani?
 
Wabunge wetu wengi hata ofisi hawana wala hawajui watakuwa nazo lini, wamekuwa wapita njia wakiogopa hata kukaribisha wadau makwao kwa hofu ya kuhojiwa, majumba yao yamekuwa kama zahanati ambapo wagonjwa humgoja mgaga asiyetimiza wajibu wake na kuuacha msururu mkubwa kwa kudai ana kazi nyingi, hana muda wa kuwasikiliza hana na silaha kubwa ni kuwataka waandike barua ambazo hata hivyo hazina pa kupelekwa.
 
Wabunge wengi hujidai kuwa wanao makatibu katika majimbo yao, ambao hawana hata ofisi wala vitendea kazi, makatibu hawa wamekuwa wakibeba lawama kubwa kujaribu kulinda heshima za wabunge wazembe na wasiojua kwa nini wamekuwa wabunge, hivi tunategemea hawa makatibu watawajibika kwa lipi wakati wao wenyewe hawana mpango wa kazi sambamba na waajili wao (wabunge)?
 
Huenda swali langu hapo juu likawa na jibu, kuwa wabunge hawa maswali wanayoenda kuuliza bungeni yametungwa na makatibu wao au wananchi waaminifu kwao, hii haitoshi kuridhisha mwananchi kwani hoja inabaki palepale kuwa je maswali au hoja hizo hazijatokana na wananchi walio wengi majimboni.
 
Huko Dodoma wabunge naamin mko katika harakati nyingi rasimi na zisizo rasimi, na moja ya mambo yanayowatoa jasho ni pamoja na kuridhia mikataba ya kimataifa ambayo yawezekana wengi wenu hawaijui na wamekuwa vipepeo tu kwa kukubali mawazo ya wachache wanaojua.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo huridhia na kupitisha mikataba mbalimbali bila hata kuwashirikisha wananchi ambao mara zote ndio wahanga wa mikataba hiyo, mfano Tanzania iliridhia mkataba wa kimataifa wa haki za biadamu, haki za watoto, haki za wanawake na mingine mingi, wabunge hukaa, hupata posho na hubadili mazingira kwa kukaa Dodoma badala ya Dar es salaam na majimboni mwao, Je! Mikataba yote hii inaeleweka kwa wananchi mnaowawakirisha Bungeni?
 
Tujiulize sote (sisi na ninyi wabunge) leo hii mko Dodoma ambako kama nilivyosema hapo juu mtarithia mikataba sita ya kimataifa, mtajadili miswaada sita ya sheria na mtauliza maswali 201 na inawezekana wengi wenu hamna hata maswali mmesubiri kuuliza maswali ya nyongeza, je hayo mwaswali, hoja za mikatyaba na sheria wananchi wenu waliowaba dhamana mmewahusisha?
 
Kazi kwenu sisi wadau wa siku moja yaani siku ya kupoteza muda kwa ajili yenu ambao mnatusahau baada ya siku mbili za kuonja uhondo wa bungeni na kulewa kwa mashangingi na kusahau majukumu yenu tunawasubiri majimbo ambapo najua mtakuja mbio mkidhani bado tunausingizi, lah mtakuta tu macho na mtakosa pa kujificha.
 
Mkataba wenu kwetu ni kutusikiliza, kukusanya mawazo yetu ya kitaifa na kuyapeleka Bungeni ambapo tunaamini yatapatiwa majibu lakini sasa mmesahau haraka jukumu hili na mmeanza kupeleka mawazo yenu huko, mmetumwa na nani hayo?
 
Mwisho kwa leo natoa wito kwa wabunge kuwa; achane mawazo ya kale kuwa wananchi hawaa cha kuwatuma, badala yake msaidieni sana mheshimiwa rais katika harakati zake za kuhakikisha maisha bora kwa kila mtanzania yanapatikana, na hayatapatikana kwa ubaguzi na kiburi chenu, kwa tabia hiyo mtawabana lini wakuu wa idara za halmashauri, wa-DC, ma-DED na wakuu wa mikoa ma-RC ambao wanategemea kupata changamoto kutoka kwenu?