KAMPUNI ya Microsoft ya nchini Marekani, inayomilikiwa na Bill Gates, imesema imeanza mpango wa kuvisaidia vituo vya watoto waishio katika mazingira magumu, ili kupata ufahamu wa kompyuta utakaowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Mkurugenzi Mwandamizi wa masuala ya kijamii wa kampuni hiyo, Akhtar Badshah, aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.
Badshah alisema tayari vituo viwili hapa nchini vimeanza kunufaika na msaada huo.
Alivitaja vituo walivyovisaidia kuwa ni kituo cha vijana cha Miracle Corner of the World, Manispaa ya Moshi na kituo cha Mkombozi Center and School Education.
Badshah alisema kuwa amekuja hapa nchini akiwa na ujumbe wa watu watatu kuangalia maendeleo ya vituo hivyo.
“Nimefurahishwa na utendaji wa vituo hivyo na tunaahidi kuendelea kusaidia vituo vingine zaidi vya hapa nchini,” alisema.
Badshah alieleza kuwa Kampuni ya Microsoft imekuwa ikilisaidia Bara la Afrika tangu mwaka 2003 ambapo wameshafanya miradi 65 ambayo imegharimu dola za Kimarekani milioni 40.