UJUMBE mzito kutoka Zanzibar unatarajiwa kuondoka visiwani humu Novemba nane kuelekea nchini Israel katika jitihada za kutafuta chanzo kingine cha umeme.
Taarifa zilizopatikana jana zimesema, hatua hiyo inachukuliwa ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa na chanzo chake cha umeme, badala ya kutegemea umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pekee ambao umekuwa na matatizo.
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Juma Is-haka Bakar amethibitisha kuwapo kwa safari hiyo itakayowajumuisha wataalamu wa nishati na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Silima Mkindwi.
Meneja huyo aliwataja wataalamu hao kuwa ni Meneja Uzalishaji, Mohammed Sheha; Meneja Uzalishaji Msaidizi, Salum Masoud na Meneja Uzalishaji Pemba, Mohammed Suleiman Khatib.
Alisema kwamba wataalamu hao watakuwepo Israel siku sita kujifundisha teknolojia ya uzalishaji umeme kupitia mawimbi ya bahari.
“Mradi huu una umuhimu mkubwa kama utafanikiwa kwa vile Zanzibar itakuwa na chanzo cha umeme cha uhakika,” alisema meneja huyo.
Alieleza kwamba, utafiti wa awali unaonyesha Zanzibar inaweza ikanufaika na umeme utokanao na mawimbi ya bahari.
Alisema hivi sasa Kisiwa cha Unguja kinatumia umeme kutoka gridi ya taifa Kidatu, lakini umeanza kuathirika kutokana na vyanzo vyake vya maji kupungua na Zanzibar kulazimika kuingia katika mgawo.
Alieleza kwambam Zanzibar hivi sasa inatumia megawatt 36 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani kwa Kisiwa cha Unguja, wakati huko Pemba umeme unaotumika unazalishwa kutoka katika vinu vitatu vilivyopo katika eneo la Wesha.
Zanzibar ilichelewa kuingia katika utaratibu wa mgawo wa umeme kutokana na kutetea mkataba wa kibiashara na TANESCO, lakini mapema mwezi uliopita, walilegeza masharti na mgawo huo kuanza kuingia Zanzibar.
Meneja huyo alisema kwamba hivi sasa Zanzibar inakatiwa umeme kuanzia saa 12:00 asubuhi na kulazimika kuigawa Zanzibar katika kanda nne na kupokezana mgawo kwa saa nne.
Tangu kuanza kwa mgawo wa umeme Zanzibar, harakati nyingi za kiuchumi na kibiashara zimeathirika na kuzua malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara.
Wakizungumzia tatizo hilo, baadhi ya wananchi walisema Zanzibar si ya kutegemea chanzo kimoja cha umeme kwa vile mahitaji yake si makubwa.
Othman Machano, mfanyabiashara katika eneo la Mlandege alisema, Shirika la Umeme Zanzibar lilifanya makosa kutoyaimarisha majenereta yake ya kuzalisha umeme yaliyopo eneo la Mtoni na badala yake kutegemea umeme kutoka Kidato peke yake.
Alisema serikali lazima ichukue mkakati madhubuti kwa vile hali ya upatikanaji umeme kutoka Kidatu inazorota siku hadi siku