Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete leo anakwenda Cape Town, Afrika Kusini ambako atahudhuria mkutano utakaojadili ukuaji wa Uchumi katika Afrika.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo unaofahamika kama World Economic Forum on Africa 2006.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu mjini Dar es Salaam jana ilisema mkutano huo ambao ni wa siku tatu unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 650 wakiwepo wakuu wa nchi na serikali, wafanyabiashara, wasomi na vyama vya kijamii kutoka nchi 36.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni "kuelekea ukuaji wa uchumi" ambapo viongozi hao wa serikali, mawaziri, wafanyabiashara wa kampuni za Afrika na kimataifa ambayo yameanzisha shughuli zao barani Afrika, watafanya tathmini ya ukuzaji wa uchumi katika Afrika. Mkutano huo pia utajielekeza katika kujadili mfumuko wa bei za bidhaa na athari zake katika uchumi wa Afrika.
Viongozi pia wataainisha vipaumbele vitakavyofanya ukuaji kuwa endelevu, watatathimini vyanzo vipya na kujadili changamoto za kukuza miundombinu inayohitajika katika kuendeleza Afrika.
Hadi jana viongozi wengine waliokuwa wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo ambao umebatizwa "Davos ya Afrika" ni Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji.
Ujumbe wa Rais katika mkutano huo ni Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Cyril Chami.
Kutoka gazeti la Uhuru