Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Kutoka kwa Wasomaji  »  Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
By Habari Tanzania | Published  10/31/2006 | Kutoka kwa Wasomaji | Rating:
BURIANI TANZANIA ... AU KILA LA HERI AFRIKA MASHARIKI?
Na Mlenge Fanuel

"Mtu akikushauri jambo la kijinga, huku anajua jambo hilo analokushauri ni la kijinga, na wewe ukakubali, basi atakuona, wewe zuzu!"
-- Mwalimu Julius K. Nyerere, 1994/5

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tafadhali isome barua hii ya wazi ya kukufikishia ujumbe kwamba Tanzania haiko tayari kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki (East African Federation, EAF) wala “Soko la Pamoja” la Afrika Mashariki, na kwamba Watanzania hatutaki Tanzania ijiunge na Shirikisho hilo.. Yatakuwa ni maafa makubwa kwa Tanzania na Watanzania iwapo Tanzania itajiunga na EAF hasa kwa mpangilio ulioko wa “fast track”. Ndiyo maana nimeanza na nukuu ya Mwalimu Nyerere, ambaye tayari baadhi ya watu, hasa wa nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda, wameanza kumsingizia kwamba kwa kujiunga na EAF tutakuwa "tunamuenzi" Mwalimu Nyerere, huku wakijua fika ushauri wanaotupa wa kujiunga na Shirikisho na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki hauna manufaa yoyote kwa Tanzania, wakidhania sisi Watanzania ni mazuzu tunaoendekeza wema wa mshumaa kuwaangazia wengine huku wenyewe unateketea, kwa minajil ya kupata misifa isiyo na tija.

Ni kweli Mheshimiwa Rais umeunda Tume ya Kupokea Maoni kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini inatia mashaka iwapo huo siyo tu ni utaratibu uliouweka kuhalalisha maamuzi yaliyokwishafikiwa ya kuidumbukiza Tanzania kwenye EAF. Hii inatokana na muonekano kwamba Tanzania kujiunga na EAF kumeshaamuliwa tayari -- kutaka watu tujadili siyo kiinimacho tu? Mheshimiwa Rais, palikuwa na muswada uliopelekwa Bungeni wa Tanzania kujiunga na EAF, ambao Waheshimiwa Wabunge waliukataa, na serikali ikabidi iuondoe. Lakini mchakato wa Tanzania kujiunga na EAF ukaendelea tu, na kupuuza maoni ya Wabunge wetu tuliowachagua watuwakilishe. Ikiwa sikusikiliza vibaya, katika Bunge la Bajeti 2006/2007, Mheshimiwa Waziri wa Afrika Mashariki aliliambia Bunge kwamba patakuwa na KURA YA MAONI kuhusu Afrika Mashariki. Matokeo yake tumeletewa Tume badala ya kura ya maoni! Kana kwamba hiyo haitoshi, iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa wewe Mheshimiwa Rais wetu, ulimhakikishia Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwamba utafanya kila unaloweza kuhakikisha kufanikiwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, kwenye mkutano wenu uliofanyika Mwanza. Je, maoni tunayotoa Watanzania kukataa kujiunga na shirikisho si "kilio cha samaki -- machozi yanakwenda na maji?" Wenyewe "wenye nchi" mshaamua mloamua?

Pana maswali mengi mheshimiwa Rais ambayo ukitupatia majibu utakuwa umetuwezesha Watanzania tulio wengi kuelewa kuhusu mustakabala wa maisha yetu na Tanzania yetu:

* Je, Ni sera ya CCM Tanzania kujiunga na EAF au Soko la Pamoja la Afrika Mashariki?

* Je, Ilikuwa kwenye ilani ya Uchaguzi 2005 ya Chama Tawala CCM Tanzania kujiunga na EAF?

* Je, Nani aliyependekeza Tanzania ijiunge na EAF? (Inabidi tumfahamu ili tuweze kumpamba maua iwapo Tanzania itafanya tunalodhani ni kosa la maisha la kujiunga EAF kumbe ikathibitika EAF ni manufaa tele kwa Tanzania ; vinginevyo inabidi tumfahamu ili tuweze kumzomea na kumuimbia nyimbo za kumsimanga pindi machungu ya EAF yatakapoanza kudhihirika muda si muda iwapo Tanzania itafanya kosa la maisha kujitumbukiza kwenye EAF. Vinginevyo itakuwa kama mikataba ya madini -- hatuelezwi nani aliwaalika na kuingia mikataba na 'wawekezaji' kwenye migodi.)

* Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameshajitangaza kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki -- ikiwa na maana yote mengine yanayojitokeza sasa ni kuhalalisha na kusafisha njia ya Museveni kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki, hasa ukitilia maanani Rais wa Kenya na wewe Rais wetu mko kimya, ikielekea mmekubaliana na matamshi ya Museveni. Si hivyo?

* Kutokana na maneno yanayosemwa na Wakenya na Waganda, Wanyarwanda na Warundi, inaonekana kama vile serikali ya Tanzania HAINA UBAVU wa kusema HAPANA kwa EAF -- kila mara Tanzania inazomewa inapohoji maslahi yake kwenye EAF -- au inapotaka kutumia uhuru wake ISIJIUNGE na EAF. Hivi karibuni Waziri wa Afrika Mashariki wa Tanzania alisemwa kwenye vyombo vya habari kwamba hahudhurii vikao vya Afrika Mashariki -- na kumfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu ajitokeze kumtetea -- na baadaye Waziri yule akaondoshwa toka Wizara ya Afrika Mashariki kwenye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri uliyoyafanya hivi karibuni Mheshimiwa Rais. Ina maana Tanzania ni kama mbwa anayeelekea kwenye mdomo wa chatu EAF -- amefyata mkia, anatoa kilio cha mwisho, na hana la kufanya zaidi ya kufanywa asusa na kumezwa -- au si hivyo?

* Ni kwa nini Kiswahili SIYO lugha rasmi EAC, na badala yake ni kiingereza?

* Kama shida ni ushirikiano, kwa nini Tanzania isijiunge na Msumbiji na Zambia , na kutengeneza shirikisho?

* Kwa nini EAF inaharakishwa namna hii?

* Ni nini Tanzania inahitaji kwenye EAF ambacho haiwezi kukipata bila kuwemo kwenye shirikisho hilo ? (Mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na watu fulani kupata posho za vikao vya EAC na baadhi kuandikwa kwenye vitabu vya historia, vitu ambavyo havimsaidii Mtanzania mpiga kura wako anayesubiri neema tele na maisha bora...)

* Pana bidhaa zipi za Tanzania hazifiki kwenye soko Kenya au Uganda , ambazo EAF itazifanya zifike sokoni?

* Nani atakuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Afrika Mashariki, na ni upi mchango wa EAF kwenye uvamizi dhidi ya DRC?

* Mheshimiwa Rais, hivi "Usalama wa Taifa" wa Tanzania una majukumu gani makubwa zaidi ya kulinda (uhuru) "Sovereignty" ya nchi yetu? Kwa nini "Usalama wa Taifa" haukupi picha kamili ambayo itakufanya usijisumbue hata kuja kutuuliza iwapo tunataka uhuru wa nchi yetu uondoke kupitia "soko la pamoja" na "Shirikisho la Afrika Mashariki", badala yake tukaendelea kulijenga taifa "letu changa" na kuulizana maswala ya maendeleo kama vile tutanufaikaje na maliasili tulizojaaliwa nchini mwetu?

* Kwa kuitumbukiza Tanzania kwenye "Soko la Pamoja" la Afrika Mashariki, huoni kwamba utakuwa umekiuka kiapo ulichokula cha kuulinda uhuru wa, na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ?

* Kulikuwa na sababu gani ya kupambana na Idd Amin aliyetaka kipande "kidogo tu" cha nchi yetu, ikiwa leo tunaigawa sandakarawe nchi nzima kwa kisingizio cha soko la pamoja?

* Tanzania itaondoka SADC? (Tayari nchi nyingine za Afrika Mashariki zimeanza kutuamuru tutoke SADC. SADC imeweka bayana kwamba wakati umefika wa kuchagua kati ya EAF au SADC.) Unadhani itakuwa ni busara kuondoka SADC? Kwa nini usitoe tamko kwamba Tanzania ya kesho ni ndani ya SADC?

* Je sisi wananchi wa Watanzania tutaulizwa kuhusu kujiunga na "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ni uamuzi uliofikiwa tayari kwamba tutajiunga na soko la pamoja la Afrika Mashariki?

* Huo Mkataba wa EAC/EAF uko wapi ili tuweze kuuona na kuusoma? Ni Watanzania gani waliousoma na kuuridhia kwamba SASA tunaanza kuwa kwenye mchakato wa kuelekea kwenye Shirikisho? (Inaripotiwa kwamba Tume yako ni sehemu tu ya taratibu ‘chovu’ za mchakato huo...)

Watanzania tutafanyaje ili kuondoka kwenye EAF, iwapo Tanzania ijajikaanga yenyewe kwa kuingia kwenye EAF? Vipengele vya kujiondoa kwenye EAF viko wapi? Hautakuwa ni uhaini kuzungumzia kujitoa EAF, kama ambavyo si ruksa kuzungumza kujitoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ?

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, maswali hayo na mengine mengi yanaleta changamoto kwako binafsi kwamba zawadi kubwa kuliko zote unazoweza kutupa sisi Watanzania, ni kutukabidhi Tanzania yetu yenye "sovereignty" ileile au zaidi ya uliyokabidhiwa pale utakapoacha madaraka mwaka 2010 au 2015, panapo majaaliwa.

Kwa taarifa yako Mheshimiwa Rais , Tanzania ndiye "Mbuzi wa Shughuli" kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Na mbuzi huyu amepangwa "kuchinjiwa kwenye maji" ili hata ukelele wake wa mwisho usisike. Hawatarudia makosa ya Jumuia ile iliyokufa 1977, kwa kutuacha bado tunafurukututa. Kujiunga kwa Tanzania EAF kwafanana na Punda wa kwenye hadithi moja iliyochapishwa Tanzania ambamo Simba baada ya kujeruhiwa, alishindwa kuwinda; na Sungura, Fisi na Punda wakaenda kumpa pole. Kumbe Fisi na Sungura walikuwa na lao jambo.
"Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mimi", alianza kusema Sungura.
" Asante sana kwa kunijali, siwezi kukula wewe rafiki yangu. Sasa nimefahamu wewe ni rafiki yangu wa kweli katika kipindi hiki kigumu cha dhiki!" alijibu Simba.
Fisi naye akajitoa aliwe na Simba, ambaye pia alikataa kumla, akitoa sababu zilezile.
Sasa Punda akawa njia panda: "Nikikaa kimya nitaonekana mbaya kwa Simba. Kwanza Simba mwenyewe kakataa kuwala wenzangu, na mimi atakataa... acha nijisemee tu kwamba najitolea anile..." aliwaza.
Akaropoka, "Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mi..." Kabla hajamaliza maneno yake alirukiwa na kuraruliwa palepale.
Kenya, Uganda , Rwanda na Burundi zina ajenda kadhaa kwenye EAF: mbali na zile "rasmi" zinazotangazwa hadharani. Ili ajenda zao zitimie, lazima "Punda" Tanzania awemo kwenye EAF ili aweze "kuliwa". Mheshimiwa Rais, ni wajibu na heshima kwako kuhakikisha Tanzania haijiungi na EAF kwa kuwa Tanzania haina ajenda mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na posho za vikao kwa baadhi ya watu.

Kwanza Tanzania siyo lazima ijiunge au ikubaliane na kila kitu kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wachache wanaounga mkono kujiunga na shirikisho la afrika mashariki, wanadai upo umuhimu wa kujiunga kwa vile "dunia nzima mwelekeo ni kujiunga pamoja, kama vile Jumuia ya Ulaya, EU". Kama sababu ni hiyo, kwa nini tusibakie SADC tuliko? Hivi tulipigania uhuru wa kusini mwa Afrika ili iweje? Watanzania tulitoa damu zetu, mali na uhai wetu, kukomboa Ndugu zetu walio Kusini mwa Afrika, sasa ukombozi umepatikana, pana wakati gani muafaka zaidi ya huu kuendeleza undugu wetu? Majirani zetu wa Afrika Mashariki tutaendelea kushiriana nao, kama tunavyoendelea kushirikiana na majirani zetu wengine. Kutojiunga kwenye shirikisho siyo maana yake tutakuwa maadui!

Tanzania lazima ikae mbali na EAF, hata ikibidi kwa miongo kadhaa ijayo, ikiwa si moja kwa moja. Kwanza , Muungano wetu wenyewe una "mipasuko" ambayo haijasilibwa bado. Kabla ya kuulizwa kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, tuulizwe basi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar . Tanganyika na Zanzibar , mara baada ya kupata Uhuru, hazikutimiza miaka mitano, "zikaishia" na kuwa Taifa moja Tanzania . Sasa jamani, Tanzania hata miaka hamsini haijafikia, nayo "iishie", tena kusikoeleweka? Tanzania ina manufaa tele SADC, kuliko kwenye shirikisho la Afrika Mashariki. Hivi, wakati tulipokuwa "Mstari wa Mbele wa Ukombozi Kusini mwa Afrika", majirani zetu wa Kenya na Uganda walikuwa wapi? Leo hii tukiwakubalia kuondoka SADC, watatuona timamu kweli?

Mheshimiwa Rais Kikwete, kiasi inaeleweka ikiwa unaona pana ugumu wa wewe kuonekana unakwenda tofauti na Watawala wetu waliotutangulia, ambao huenda wanapendelea kuona EAF ikizinduliwa, Tanzania ikiwemo. Lakini mheshimiwa Rais, ndiyo maana kukawa na kikomo cha utawala cha vipindi viwiliviwili! Kwa kuwa umechaguliwa kwa ushindi "wa kishindo", imani yetu Watanzania imekuwa kwako kwamba utaweza kuipeleka Tanzania kule tunakotaka. Na tunakotaka sisi Watanzania siyo kwenye "soko la pamoja la afrika mashariki" wala EAF. Huo Muungano tu wa Forodha wa Afrika Mashariki unatekelezwaje? Matatizo na mizengwe iliyoko panaashiria nini pindi tukiwagaia nchi hii yote kwenye Shirikisho au "soko la pamoja"? Siyo maafa, Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Rais Kikwete, kwenye Jumuia ya Ulaya --EU, Uingereza na Jamhuri ya Ireland SIYO mataifa yaliyoko kwenye "Mkataba wa Schengen" wa Jumuia ya Ulaya, mkataba unaoondoa mipaka na vizuizi baina ya nchi za Jumuia ya Ulaya kwenye masuala ya Uhamiaji, japo Uingereza na Jamhuri ya Ireland ni wanachama kamili wa Jumuia ya Ulaya. Hii haikuzuia Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani na nchi nyinginezo za EU zilizokubali kusaini kuendelea na "Makubaliano ya Schengen". Kadhalika , Iceland , Norway na Uswisi zimesaini "Mkataba wa Schengen" japo nchi hizo SI zanachama Jumuia ya Ulaya. Kila taifa linaangalia maslahi yake kama taifa. . Ulipoanzishwa umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki takriban karne moja iliyopita, Tanganyika haikujiunga mpaka ilipoona vema kwamba itakuwa ni kwa maslahi yake kujiunga. Hii haikuzizuia Kenya na Uganda kuanzisha Umoja wao wa Forodha. Tanganyika ilijiunga baadaye! Hata ile Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ilianzishwa baada ya kupita MIAKA HAMSINI tangu kuanzishwa ule Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, japo nchi hizi zote tatu zilikuwa zinatawaliwa na Mkoloni mmoja takriban muda wote huo. Haraka ya sasa hivi ya nini? Wanajua wakituachia muda, tukienda hatua kwa hatua, hawataweza tena kuigeuza Tanzania koloni lao. Tanzania iendelee kuwa mwanachama wa SADC, na kuendelea kuwa imesaini kwa muda makubaliano ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki mpaka pale SADC itakapoanzisha Umoja wa Forodha wa SADC, ambapo Tanzania itajitoa kwenye Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Au busara zaidi, ni vyema Tanzania ikajitoa SASA HIVI toka Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, na kuelekeza nguvu zake kwenye SADC. Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi zinaweza kuendelea na Umoja wao wa Forodha, Soko la Pamoja na Shirikisho (waliite vyovyote wapendavyo), bila Tanzania kuwemo.

* Mheshimiwa Rais, ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania ni zaidi ya Jumla ya eneo lote la ardhi ya Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi ukizichanganya pamoja -- bila kuzungumzia rasilmali zilizoko. Halafu wanasema tuchanganye ardhi yetu na zao, halafu tugawane sawasawa kwa jina la "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki". Hivi tukikubali ujuha huo, ni kwa nini wasituone sisi mazuzu?

Swali kuu tunaloulizwa Watanzania na Tume yako mheshimiwa Rais ni iwapo Watanzania tunaona bado kuna sababu za Tanzania kuendelea kuwa nchi huru ambayo ni "dola", wakati ambapo kuna shinikizo nchi yetu igawe uhuru wake kwa kisingizio cha "soko la pamoja" na "shirikisho la Afrika Mashariki". Tuchukulie kwa mfano, tume itawahoji na kupokea maoni toka kwa watu laki mbili. Kati yao 80% wakasema Tanzania ijiunge kwenye "Soko la Pamoja" na "Shirikisho la Afrika Mashariki", 20% wakasema tusijiunge. Je, Mheshimiwa Rais, hiyo itakuwa na maana uamuzi utakuwa umesilibwa wa Tanzania kufikia mwisho wake, kwa kujiunga na Soko la Pamoja na Shirikisho la Afrika Mashariki? Je, hutatumia busara kama ilivyotumika kwenye Tume ya Nyalali ya Vyama Vingi pale Tanzania ilipoangalia maslahi ya taifa, na kuruhusu mfumo wa vyama vingi, bila kuangalia asilimia zilizotokana na tume? Ikiwa kweli kabisa umedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye mwisho wake machinjioni Afrika Mashariki, kwa nini usiweke KURA YA MAONI kwa kila Mtanzania kupiga kura yake, badala ya kutumia Tume, angalau basi kuchelewesha kwa muda mauti ya Taifa Tanzania? "Soko la Pamoja" na pacha wake "Shirikisho la Afrika Mashariki" maana yake ni mwisho wa uhai wa Taifa la Tanzania . Ikiwa Tanzania itajinyonga (Mungu apishie mbali!) kwa kusaini mkataba wa "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ule wa "Shirikisho la Afrika Mashariki", basi Watanzania tutasahau "maisha bora kwa kila Mtanzania" na itabidi tujiandae kwa "Bora Maisha kwa kila Mtanzania", na kwamba wewe Rais wetu, Jakaya Kikwete, utakuwa umefeli vibaya kabisa jukumu lako la msingi tulilokupa -- kulinda uhuru na umoja wa Taifa la Tanzania na kubakisha Taifa la Tanzania kuwa dola huru kwa manufaa ya Watanzania mpaka pale utakapomkabidhi madaraka ya Urais wa dola la Tanzania huru Mtanzania mwingine.

Kwa kuandika barua hii, imani yetu Watanzania kwako Rais wetu kwamba utaweza kuhimili mashinikizo yote ya nje, na kutusikiliza sisi raia zako, tunaotaka tubakie na taifa letu huru la dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Mwenyezi Mungu akujalie. Amin.

Ndimi,

Mlenge Fanuel
Raia na Mwananchi wa Tanzania,
Simu: +255 75 4372902,
Email: mlenge@yahoo.com,
Dar es Salaam, Tanzania.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Njimba)
    Rating
    Ndugu yangu Mulenge, umesema yote ambayo Mheshimiwa Jakaya Kikwete kama ana masikio na mapenzi Na nchi yake atasikia. WASIWASI WANGU HII BARUA ITAMFIKIAJE?
    Mimi kwa sasa niko Kenya, jinsi hawa jamaa walivyoniandama pale alipoingelea Kenya, Marekani, kwa kweli ilionyesha wazi kuwa hawa jamaa sio wavumilivu na hawana mapenzi hata kidogo. Labda anataka ajinunue kwa kukubali kuwa nao kwenye muungano. Lakini kwa vile nilivyoona hata akija hapa sidhani kama atapokelewa vizuri. Anyway, tuyache hayo. SWALI TUFANYE ILI ASIKIE KILIO CHETU? TUFANYEJE ILI ASIKIE YOTE HAYA? MASWALI NI MENGI, KILA KITU KIKO WAZI, ILA HAKUNA ANAYESIKIA. TUFANYEJE WATANZANIA WENZANGU? HAWA VIONGOZI WANA NINI? MPAKA SASA SIAMINI NI KIKWETE ANAYEWEZA KUTUPELEKA KWENYE SHIMO HILI. TAFADHARI MUHESHIMIWA RAISI SIKIA KILIO CHETU. NI NCHI NA RASIMALI ZETU TUNAJIVUNIA, TUACHIE TAFADHARI.
     
  • Comment #2 (Posted by Mashami Kaaya)
    Rating
    I Definetely agree with the writer.
     
  • Comment #3 (Posted by JOSEPH T KAAYA)
    Rating
    nakubaliana kabisa na ndugu aliyeandika ujumbe huu,huu ni ujumbe muafaka kwa wakati muafaka,Je Museveni tunayetaka kujiunga naye ni yule anayevamia DRC,si yule aliyeshindwa kutuliza ghasia kaskazini mwa Uganda kwa miaka 20,Je mwai Kibaki siyo yule ambaye tangu awe rais nchi yake haijatula mara ODM mara vipi,hiyo siyo kwamba inaonyesha wananchi wake hawaridhishwi hasa viongozi wenzake,Rwanda na Burundi kila kukicha suluhisho tena tunasuluhisha sisi watanzania? ni nini tunataka huko ambacho hatuwezi kupata SADC,ninachomwomba rais tusiiende haraka kwani wanataka kutuvuruuga na kwa kweli tusijejilaumu baadaye,lakini rais tunakutegemea ukitunyanyasa ujue wote tutaona kwamba tulikosea kukupa urais.
     
  • Comment #4 (Posted by Anyosisye Njobelo)
    Rating
    Kikwete hana la kulaumiwa yeye ni kichwa chetu alichofanya ni kutoa yale aliyoongea na wenzie kuhusu umoja huu. Kazi iko kwetu tushiriki kwenye maoni hayo na kwa maelezo ya barua ya wazi tuna nafasi ya kukataa wala Kikwete hawezi kulazimisha. Umoja ni muhimu lakini tuangalie ni umoja wa aina gani. Vyote fanyeni Kenya nimefika na Uganda vile vile suala la ardhi ni kero kubwa kwao. Sisi ardhi ni mali ya taifa wao ni mali ya watu hii ina maana wanataka kuja kupora ardhi. Kamati iliyopewa kazi hii iangalie kwanza iwaelimishe watanzania wajue ni nini na baadaye watoe maoni. Nawaomba wasomi wa Tanzania tushiriki kikamilifu tusitegemee walioko vijijini hawajui tuko wapi na tunaenda wapi. SACCOS zenyewe hawazijui wanahitaji elimu yake wakati wenzetu wa Kenya wako mbali sasa tunataka kuchanganya maji baridi na unga kupata ugali aaah hapana. Kuna wengine hata muungano wa Tanzania hawauelewi sasa tunawabebesha wa Afrika Mashariki. Mwl Nyerere alipowaomba kuungana wangekubali ilikuwa rahisi kwa sasa ni maji marefu. Ukabila wao utatusambaratisha. tukitaka umoja huo anzia siasa ziwe sawa fuatia na sera za ardhi kila mtu yake halafu ukabila kisha mila ziangaliwe vizuri pia kuna watu wanatwanga wake zao utadhani wanakoboa mahindi wakati sisi tunapiga vita.Suala hili tusiposhiri sisi wasomi kutoa maoni kwenye tume tutalaumiwa na tusijelaumu mtu si Kikwete wala Lowasa hawa wanasubiri kutoka kwetu
     
  • Comment #5 (Posted by Richard)
    Rating
    i think the writer is preoccupied with what he thinks he wants but not how the future of globalization and competitiveness,thye main gola of east africanication i think is having an economical muscle as a block,collective bargaining in world foras including collective marketing of destination as tourist mecca and the investment dollars which are chasing huge global markets.Tanzania willremain weak econimicaly even without joining EAF but it stand to gain a lot .only strategic economist can explain that.
    Thanks
     
  • Comment #6 (Posted by washawasha)
    Rating
    Hongera sana muheshimiwa kwa kumuandikia barua iliyo wazi mkuu raisi wa nchi yetu hii ya Tanzania,muheshimiwa raisi tungependa kwa nia moja ama nyingine Tanzania kuwemo katika umoja huu ambao kwa kiingereza naweza kusema (Sucks)hatuukubali kwa njia moja ama nyingine hivi raisi matatizo yetu ndani ya nchi tumeyamaliza vipi mpaka tutake kuwa na uhusiana na mtu ambaye ana matatizo kama cc?
    Muheshimiwa raisi ningependa na ningekusifu sana iwapo ungedeal na matatizo tuliyonayo halafu huo muungano baadae,
    Muheshimiwa raisi ningependfa ujue kwamba COBRA mdogo sumu kali hivyo usitudharau na kusema cc ni wadogo kisiasa.
    Muheshimiwa raisi tusingependa kuyarudia hayo yaliyoelezwa na mwenzetu mmoja kati ya cc wapinga umoja huo ambao ni unyonyaji kwe2
    Muheshimiwa tunapenda ulifikirie hili suala kiundani zaidi
    Mungu ibariki Tanzania,
    Mungu walani wote wasioitakia mema Tanzania,
    AMIN.
     
  • Comment #7 (Posted by Phares)
    Rating
    Hongera Mwandishi, hakuna msomi atakeyesoma hii article halafu apingane nayo kama anaitakia mema Tanzania. Ni kweli kuwa dunia inaungana, EU, N. America and S. Amerika hata Asia wote wanaunanga. Tatizo hapa EAF sio kuungana bali ni hii kasi ya ajabu na usiri wa Muungano wenyewe. Kwa nini tusijiunge kibishara kwanza then later tukiona kuna mapungufu ndipo ifanyike referandum ili wananchi wa nchi zote waamue. Hii haraka haraka huwa haina baraka siku zote. Tafadhali viongozi wetu nendeni taratibu, sio kila mwananchi aliyewapa kura anatambua faida na hasara za EAF hivyo ni vema wapewe muda wa kutosha na nafasi ya kuamua.
     
  • Comment #8 (Posted by muta)
    Rating
    Hongera mwandishi ila umemtwisha mzigo mkubwa kanga bure. Kikwete si chochote wala lolote bali caricuture.
    Kwa mtu makini hawezi kukubali kukurupuka. Kwa wale wanaosema kuwa tutatengeneza soko kubwa kwa bidhaa zipi tunazozalisha. Haya yangesemwa na wachina ningeelewa. Mbona Nigeria ina watu milioni 120 na mafuta juu lakini i hoi?
    Hawa watawala wetu ni wapuuzi hamna jinsi ya kuwaita. Hawana uchungu nasi wala nchi yetu bali matumbo yao. Ni kazi kwetu wananchi kuchukia shirikisho na kutoshirikiana na hawa watu wao wanaotaka kutulazimisha kushirikiana nao.
    Ni upuuzi. njoo kagera nenda kigoma uone warundi na wanyarwanda walivyovuruga nchi yetu. Nenda arusha uone wakenya wanavyoongoza mazoezi ya ujambazi hadi dar es salaam. EAF ni upuuuuuuuuuuuuuuuuuzi mtupu.

     
  • Comment #9 (Posted by kimito)
    Rating
    Ahsante mheshimiwa Mlenge. Kwa kuongezea tu ni kuwa hawa jamaa wa kenya hawajatueleza ni kwanini walivunja EAC 1977,kwa sababu hatuwezi kusahihisha kosa kwa kukataa au kutosema ukweli.Watanzani tulitaabika sana na umasikini huu ni sehemu ya kuvunjika kwa EAC kwa sababu tuliwaamini sana wenzetu tukawa mishumaa.
    Pili,nini kifanyike! hizi tume mara nyingi zinawekwa kukidhi matakwa ya wakubwa.Hivi siku hizi wasomi kama wa vyuo vikuu wanafanya nini,maana kwa nchi za wenzetu mitaani ni maandamano hadi ujumbe ufike ikulu. Siku hizi chuo kikuu kama UDSM WASOMI WANAJADILI BONGO FLAVA,natamani miaka ya 70 na 80 ingerudi.
     
  • Comment #10 (Posted by Fredy)
    Rating
    Binafsi nimefarijika kwamba angalau kuna watanzania ambao wana uchungu na nhi yao na wanaweza kutanabaisha mambo mbalimbali yanayolihusu taifa kwa ukaribu na unyeti mkubwa kama hili.
    Ni kweli kuna tofauti kubwa kati ya nchi hizi za Africa mashariki, na kusema kuziunganisha pamoja kitakachotokea ni kwamba kuna wa kuumia sana na kuna wa kufaidika saaana! But we stand the chance of loosing a lot, for sure!!! Nasikia Kenya Airways inang'ara sana kutokana na kwamba tulikuwa tukichangia uendeshaji wa shirika(ikiwemo ununuzi wa ndege) na baada ya shirikisho kuvunjika wakachukua kila kitu na sie tulibaki tukifuta makalio.sasa vingzi sijui walikuwa wanawaznini maskini ya Mungu, wakenya wakajifaidia za kana kwamba vitu vya Tz havina mwenyewe..... Huu ndio ulimbukeni wenyewe ndugu mwandishi; wanataka kutufaidi 'mupya' kabisa ndugu mwandishi!! Tafadhali viongozi wetu na wataalam mbalimbali zingatieni mustakabali wa nchi kwa manufaa ya wanchi wote.
     
Submit Comment


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.