Madaktari wawili wa Tanzania ni miongoni mwa abiria waliopoteza maisha katika ajali mbaya ya ndege iliyotokea katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja juzi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa leo imewataja madaktari hao kuwa ni Madokta Nakijwa Kanyika wa Hospitali ya Morogoro na mwenzake Moshi Luhiso kutoka Hospitali ya Makandana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madaktari hao pamoja na wenzao walikwenda Nigeria Ijumaa iliyopita kwa shughili za kikazi zilizoratibiwa na Shirika la Afya Duniani, WHO.
Taarifa hiyo imesema miili ya madaktari hao ilitambuliwa na madaktari wenzao walioongozana nao kwenye shughuli hizo za WHO.
Imefafanuliwa kuwa madaktari hao waliosalimika, hawakupanda ndege hiyo iliyopata ajali kwa vile wao walibakia mjini Lagos kwa ajili ya kwenda jimbo lingine.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Serikali kupitia ubalozi wake ulioko nchini Nigeria na Shirika la Afya Duniani wanashirikiana kuandaa taratibu za kusafirisha miili ya madaktari hao.
Imeelezwa kuwa kama mipango itakamilika, miili hiyo itasafirishwa kuja Jijini kesho Jumatano.
Serikali imeeleza kusikitishwa kwake na vifo hivyo na imetoa salam za rambi rambi kwa ndugu na jamaa wa marehemu hao.
Ajali hiyo mbaya ilitokea juzi baada ya ndege hiyo kuanguka na kisha kuwaka moto wakati inaruka.
Ilielezwa kuwa watu zaidi ya 100 waliokuwemo walipoteza maisha yao.