Na Abdallah Bawazir, Dodoma, Gazeti la Mwananchi MKUTANO wa Tano cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaanza leo mjini hapa, ambao pamoja na mambo mengine utajadili miswada sita ya sheria.
Tayari baadhi ya wabunge, akiwamo Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wengine wamewasili mjini hapa kuhudhuriamkutano huo wa wiki mbili.
Mkutano huo pia utachagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na kuridhia mikataba sita ya kimataifa na kujibu maswali 201 ya wabunge.
Afisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zullu, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, miswada ya sheria itakayojadiliwa ni pamoja na ule unaohusu Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa.
Sheria hiyo mpya inakusudia kuubadili mpango wa sasa wa akiba unaoendeshwa kwa ajili ya wafanyakazi wa serikali za mitaa, taasisi zinazohusiana nazo na wachangiaji wengine ili uweze kutoa mafao mazuri zaidi kwa wanachama.
Muswada mwingine unahusu Biashara Haramu ya Fedha ambao unakusudia kupendekeza muundo madhubuti na hatua za kupambana na tatizo la biashara hiyo.
Pia utakuwapo muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ikiwamo ya kupambana ulaghai katika michezo ya kubahatisha.
Marekebisho hayo pia yanakusudia kuwafanya wabunge wa kuteuliwa na Rais na wajumbe wanaoteuliwa na waziri kuwa wajumbe wa halmashauri za wilaya wanazoishi.
Muswada mwingine ni wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Huduma za Mawasiliano ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani wanaoishi vijijini.