.Litakamilika mwakani
Na Ramadhan Mkoma, Gazeti la Uhuru
KATIKA hatua ya kuwapatia maeneo ya kudumu ya kufanyia biashara, serikali imeamua kuwajengea jengo la ghorofa tano ‘machinga’ mjini Dar es Salaam.
Ujenzi huo ni mpango wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wa kuwa na jengo la kisasa litakalofahamika kwa jina la ‘Business Park’ na kutumiwa na wafanyabiashara hao.
Meya ya Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa, alibainisha hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee.
Kwa mujibu wa Kimbisa, ujenzi wa jengo hilo litalogharimu sh. bilioni 10, unatarajiwa kuanza mwezi ujao na litajengwa jirani na uwanja wa mpira wa Karume, Ilala, mbele ya mtaa wa Lindi, huku sehemu ya jengo ikiwa imepita juu ya barabara ya Kawawa.
Alisema ujenzi unatarajiwa kuchukua miezi tisa hadi 12 kukamilika na kufuatiwa na ujenzi wa majengo mengine ya aina hiyo sehemu mbalimbali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam.
Pia Kimbisa aliwaonyesha waandishi wa habari mchoro wa jengo hilo la kisasa, ulioandaliwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo litahusika na mradi huo.
Jengo hilo, lenye ukubwa wa mita za mraba 20,000, litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja na wengine wanaofikia 5,000 wataweza kuendesha shughuli zao mbalimbali katika eneo hilo.
Alisema mbali na machinga, pia jengo hilo litakuwa na huduma mbalimbali, ikiwemo migahawa na benki ambayo pia itatumika kutoa mikopo kwa wafanyabiasha hao.
Kulingana na Kimbisa, tayari serikali imeridhia mradi huo kwa kukubali kuudhamini na kwamba kinachoendelea sasa ni taratibu za utekelezaji wa mradi huo, ambao umelenga kuboresha mazingira ya wafanyao biashara ndogo ndogo jijini.
Akifafanua, Kimbisa alisema mbali na shughuli za kibiashara, jengo hilo pia linatarajiwa kuwa kivutio kwa watalii watakaofika kupata mahitaji mbalimbali katika jengo hilo la kisasa.
Pia, alisema kuwepo kwa jengo hilo kutarahisisha utaratibu wa serikali wa kuwapatia mikopo machinga kwa kuwa watakuwa katika maeneo rasmi na yenye mazingira bora ya kibiashara.
Msanifu wa Majengo kutoka NSSF, Deogratius Mponeja, alisema mradi huo umekuja wakati muafaka, na hasa ikizingatiwa mahitaji ya maeneo ya kufanyia biashara kwa wafanyao biashara ndogo ndogo.
Mponeja alitaja baadhi ya mataifa ambayo wafanyabiashara wake wamenufaika kupitia mradi kama huo kuwa ni China, Malaysia na Uganda.
Wakati huo huo, Meya Kimbisa amewasihi wafanyabiashara walioko katika maeneo maalum kuendelea kufanya shughuli zao katika sehemu hizo ili kuepuka adha inayoweza kujitokeza iwapo watarejea mitaani.
Alisema serikali haitarudi nyuma katika juhudi zake za kuwaondoa katika maeneo yasiyokuwa rasmi kwao na wakati huo huo, ikielekeza nguvu zake katika ujenzi wa miundombinu ya kudumu kwa ajili yao.