Na Grace Msovela, Arusha
KATIKA hali ya kutatanisha, polisi imehifadhi jina la babu wa Kihindi anayetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi.
Sambamba na tukio hilo, kijana anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mama yake mzazi.
Tukio la babu wa Kihindi kubaka lilitokea mjini Arusha, ambapo mwanafunzi wa shule ya msingi ya Uhuru, anayesoma
darasa la pili (jina limehifadhiwa) alidai alibakwa na mtu aliyemtaja kuwa ni “babu wa kihindi” ila hamfahamu jina.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, tukio la kubakwa kwa mwanafunzi lilitokea Jumamosi saa 11 jioni, maeneo ya barabara ya Uhuru, wakati mtoto huyo akiwa anakwenda nyumbani na mwenzake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Matei Basilio, alisema wakiwa njiani inadaiwa waliitwa katika nyumba ya Mhindi, na hatimaye kumbaka mtoto huyo.
Hata hivyo, Kamanda Basilio alisema ni mapema kumtaja jina mtuhumiwa kwa sababu bado upelelezi haujakamilika, mpaka wathibitishe kama ni kweli babu huyo alihusika kumbaka mtoto huyo ndipo watatoa taarifa kwa usahihi.Kutoka Dodoma, Kulthum Mchatta anaripoti kuwa Nguja Mpali (23) mkazi wa kijiji Mbala, nje kidogo ya manispaa ya Dodoma, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kumbaka mama yake mzazi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dodoma, Omari Mganga, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba kijana huyo anadaiwa kumbaka mama yake mwenye umri wa miaka 45 ambaye alikuwa na wiki mbili tangu ajifungue.
Mganga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jumamosi jioni wakiwa nyumbani kwao Mbabala.
Alisema kijana huyo alirudi nyumbani akitokea kwenye mizunguko yake ambapo inadaiwa alimwomba mama yake ampe ugali na akamjibu kwamba hakukuwa na chakula, jibu ambalo linasemekana lilimkasirisha na kuamua kumshika mama yake kwa nguvu na kumbaka.
Kamanda alisema kuwa mama huyo alipiga kelele zilizowafanya majirani kwenda eneo la tukio, lakini wakakuta ameshabakwa.
Alisema majirani hao walimkuta mama katika hali mbaya na wakamchukua kumpeleka hospitalini ambako amelazwa, huku kijan akiwa anashikiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.Kwa mujibu wa mama mzazi, mtoto wake ana tabia ya ulevi na uvutaji wa bangi ambazo ndizo zimemfanya kufanya kitendo hicho.
Katika tukio lingine, Fred Chuhuva mkazi wa Nairobi, Kenya alikutwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni ya New Generation.
Mganga alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi katika kijiji cha Haneti, katika wilaya mpya ya Chamwino, Dodoma.