Watalii wengi hufika nchini kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali wakiwemo wanyama, na kuchangia pato la taifa.
Kwa upande mwingine wanyama hao wamekuwa tatizo kubwa kwa wakazi wa maeneo ya karibu na walipohifadhiwa. Mwandishi wetu Namsembaeli Mduma aliyekuwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa mkoani humo anaelezea zaidi.
Mkoa wa Lindi una eneo la Kilomita za mraba 67,000. Kati ya hizo 18,000 ni hifadhi ya Selous.
Eneo hilo kama linavyojulikana kwa lugha ya kigeni Selous Game Reserve ndilo pori kubwa duniani lililowekwa chini ya urithi wa dunia na UNESCO.
Pori hili lina wanyama wengi na baadhi yao wamo katika hatari ya kutoweka duniani. Wanyama hao ni pamoja na tembo, faru, mamba na mbwa mwitu. Pori hili limetenga karibu hekta 800 kwa ajili ya vitalu vya kuwinda na Watalii ambao pia hufanya utalii wa picha.
Njia zinazotumiwa na watalii hao kufika katika eneo hilo ni pamoja na barabara kutoka Dar es Salaam kupitia Utete na ile ya ndege ambayo huishia kwenye viwanja vyake.
Katika wilaya ya Kilwa kuna pori la ukubwa wa kilomita za mraba 50. Pori hili ni hifadhi inayopendekezwa na linajulikana kama mto Nyange.
Umuhimu wa pori hili ni viboko wengi idadi inayofikia 450 katika bwawa la mto huo. Wanyama wengine wanaopatikana hapo ni chui, tembo, nyati, simba, kongoni na jamii ya ndege na nyani.
Mbali na mapori hayo, yapo ya wazi na yale ambayo hayakutengwa kwa ajili ya hifadhi za Wanyamapori au Misitu.
Kutokana na taarifa ya sekta hiyo ya maliasili kwa Waziri Mkuu, maeneo haya ya wazi ndimo wananchi huwinda wanyamapori kwa ajili ya kitoweo na kujistarehesha.
Kuna mapori mengine yaliyotengwa kwa ajili ya jamii vijijini na yapo kando kando ya Hifadhi ya Selous.
Wananchi hushirikishwa katika uhifadhi na papo hapo hufaidika na mapato ya uwindaji wa wanyama unaofanywa na wenyeji na Watalii.
Vijiji vya wilaya ya Liwale vimetengewa maeneo ya aina hii.
Mpango huo unategemewa kuanzishwa katika wilaya ya Kilwa pia.
Lakini, pamoja na watalii kuvutiwa na wanyamapori, wamekuwa wakiharibu mazao mashambani na hivyo kusababisha hasara kubwa.
Mfano wanyama kama nguruwe, tembo, boko na nyani ndio hasa wanaoelezwa kuwa kero kubwa katika maeneo ambayo wanavijiji wapo mmoja mmoja au wapo katika sehemu za mbali mbali kwenye maeneo makubwa.
Ukiachilia wanyama hao, wapo wakali ambao nao wanaelezewa kuwa tatizo kubwa kwa watu na mifugo yao. Wanyama hao ni kama simba na wengineo.
Maelezo ya maofisa wa wanyama pori kwa Waziri Mkuu yanasema kuwa wanyama hawa wanapata urahisi wa kuwaingilia watu vijijini kutokana na ulinzi mdogo wa askari wa Wanyamapori, kufuatia uchache wao na ukosefu wa zana za kisasa zakutosha.
Miaka ya 1980, mkoa wa Lindi ulikuwa na askari wa wanyama pori takriban 40 lakini sasa imeporomoka hadi kufikia 25 tu. Uchache huo ndio unaosababisha jitihada za kuwadhibiti wanyama hao waharibifu kukwama.
Kutokana na takwimu za mwaka 2004, watu 30 waliuawa na simba katika mkoa huu na wilaya zilizoathirika zaidi zilikuwa Liwale na Lindi.
Watu na mifugo hushambuliwa zaidi na wanyama hao wakali nyakati za kiangazi ambapo kuna kuwa na ukame wa maji na malisho.
Hali hiyo inawasukuma wanyama hao wa porini kuingia katika makazi ya watu hasa ya karibu nao na kuleta tafrani au kuua kabisa.
Kwa kuwa utalii ni moja ya hazina kubwa ya mkoa huu, jitihada mbalimbali hufanywa na Serikali kuhakikisha haipotei, uhifadhi wa mazingira unapewa kipaumbele zaidi, kwa kuwaelimisha wananchi juu ya upandaji wa miti na utunzaji wa ile mioto ya asili.
Kuna fukwe za bahari kama vile Mitema na Mchinga katika wilaya ya Lindi na Jimbize, Masoko Pwani na Mto Kiswere wilayani Kilwa.
Vivutio vingine ni Majengo ya kale ya kihistoria wilayani Kilwa kama vile magofu ya Kilwa Kivinje, Kilwa Kisiwani, na Siongo Mnara. Magofu haya yalijengwa na Waswahili, Waarabu na Wareno kati ya karne ya 14 na 19.
Mapango mengine ni ya Nang’oma wilayani Kilwa ambayo ndimo Wamatumbi walijificha wakati wa vita vya Maji-Maji kati ya Wajerumani na Wamatumbi hao.
Katika pango hili, kuna mapango madogo madogo ambamo walizikwa watu waliouawa vitani.
Siku hizi mapango haya yanahifadhiwa na jamii inayoyazunguka.
Katika kijiji cha Tenganduru wilayani Lindi kunapatikana mabaki ya mnyama aliyeitwa Dinosaur aliyeishi miaka 65-208 milioni iliyopita.
Mabaki mengine ya wanyama hao yalichukuliwa na kupelekwa Berlin katika jumba la Makumbusho kabla ya Tanganyika kupata uhuru wake.
Mbali na wanyamapori, mkoa huo umejaliwa misitu mikubwa ya asili aina ya miombo yenye ukubwa wa Hekta 4, 272,000 na misitu ya kupandwa aina ya Pine Hekta 2000 ambayo ipo kwenye miinuko ya Tarafa ya Rondo.
Misitu ya mikoko imeenea katika eneo la pwani ya Bahari ya Hindi kwa Hekta 26,500. Hii inafanya mkoa wa Lindi kuwa wa tatu hapa nchini kwa kuwa na eneo kubwa la misitu hiyo baada ya mikoa ya Tabora ambao una hekta 53,600,000 na ule wa Rukwa wenye Hekta 4,900,000.
Kati ya Kilomita za mraba 42,720 za misitu ya asili ya miombo, kilomita za mraba 5,893 ni misitu ya hifadhi ambapo asilimia 87 iko cini ya Serikali Kuu wakati asilimia 13 ipo chini ya Serikali za Mitaa (Halmashauri za wilaya).
Eneo lililobaki ni la kilomita za mraba 36,827 ambazo ni maeneo ya misitru isiyohifadhiwa.
Msitu wa Rondo wenye Hekta 2000 ni msitu pekee wa miti laini kwenye mkoa huu. Msitu huu pamoja na mikoko yote ina hadhi ya hifadhi.
Tunapozungumzia misitu hatuna budi kuzungumzia upandaji miti. Kutokana na takwimu za mkoa huo upandaji wa miti katika wilaya za Ruangwa, Nachingwea, Kilwa, Liwale na Lindi ulikuwa kama ifuatavyo; kuanzia Julai 2002 hadi Juni 2003 na Julai 2003 hadi 2004.
Kilwa ilipanda miti 320,900 ambapo miti 312 ilipona, mwaka uliofuata ilipanda miti 500,000 na ilipona 330,000.
Lindi ilipanda miti 662,250 na ikapona 660,436. Mwaka uluofuata ilipanda miti 1,000,000 na ikapona 630,000.
Kadhalika wilaya ya Nachingwea kwa miaka ya mwanzo ilipanda miti 600,000 ambapo ilipona 542,815.
Kipindi kilichofuata ilipanda miti 1,000,000 na ilikua 750,000. Ruangwa ilipanda miti 1000,000 kipindi cha kwanza na ikaota 500,000 wakati miaka iliyofuayta ilipanda miti 1000,000 tena na iliyokua ilikuwa 500,000.
Pamoja na kukua kwa sekta hii mkoani humo, inakumbwa na vikwazo mbalimbali kama vile uvunwaji wa miti usio halali, kutoonwa na jamii kuwa ni zao la kilimo na biashara kama mengine.
Hata hivyo,sekta hiyo ya misitu inamwelekeo wa kupunguza umasikini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2005 na kuufuta kabisa ifikapo mwaka 2025.
SOURCE: Nipashe